Peach Fuzz rangi ya mwaka 2024

Wanamitindo wakiwa katika picha za mavazi yenye rangi ya Peach fuzz. Picha na mtandao

Ni takribani siku 14 tangu tuanze mwaka 2024, umeshajiuliza rangi ya mwaka huu ni ipi? Kama bado wala usiumize kichwa, wataalamu wa rangi, kampuni Pantone tayari imesharahisisha hili kwa kuitangazia dunia kuwa peach fuzz ndiyo rangi ya mwaka 2024.

Kulingana na Pantone, rangi hii hufariji katika nyakati za sasa, na huwafanya watu kupata amani (hata unapokuwa peke yako) kulingana na hali ya jamii.
Rangi iliyotangazwa na kutumika mwaka jana ilikuwa Viva Magenta.

Imekuwa utaratibu wa wataalamu hao kutangaza rangi itakayotumika kila mwaka ambapo rangi hiyo hujumuisha mavazi na shughuli zote za mapambo.
Peach kimsingi ni chungwa iliyokolea sana, kwa hiyo ina hisia ya joto, nishati, na urafiki.


 

Asili ya rangi ya Peach Fuzz

Kwa mujibu wa chapisho la Pantone, asili na maana ya rangi ya peach fuzz ni rangi inayomaanisha huruma na wema wa kutoka moyoni.

Peach inachukuliwa kuwa rangi maarufu katika tamaduni za magharibi kama rangi ya upole, matumaini baada ya vita na ngozi za watu wa euro-centric, wakati katika historia za Mashariki mwa Ulaya huchukuliwa kuwa na mawazo ya nguvu ya bahati nzuri, kutokufa na uzuri wa zamani.

Katika utamaduni wa Kichina, rangi ya peach inawakilisha bahati nzuri na maisha marefu.

Umuhimu unatokana na uhusiano na ‘mti wa peach wa kutokufa kutokana na kupukutisha majani wakati wa kiangazi hivyo kuendelea kumea’.
Peach hutumiwa katika sanaa, rangi hii ina umuhimu mkubwa wa kitamaduni nchini Uchina, ikionyesha maadili yenye nguvu na chanya katika ngano, mila na usemi wa kisanii.

Wakati wa enzi ya uchoraji, wasanii walipenda kutumia rangi za peach kwa sababu zilikuwa nzuri kwa kunasa miale ya mwanga na anga katika picha zao za uchoraji.
Rangi za peach zilisaidia kuwasilisha joto na mwanga wa jua, hasa wakati wa jua au machweo.

Katika mapambo ya sanaa, rangi ya peach ilitumiwa kuunda hisia ya matumaini na kisasa baada ya Vita Kuu ya Dunia.

Iliashiria uboreshaji na uzuri, ikionyesha wakati wa ustawi ulioahidiwa.
Peach ilikuwa maarufu sana inapotumiwa kwenye kioo na kwenye vyombo vya glasi.

Iwe katika mitindo, muundo, au vitu unavyotumia kila siku, pichi iligeuka kuwa kielelezo cha ustawi na uzuri unaohusishwa kushika hatamu kwa miaka ya ishirini.
Wanamitindo wameipokea vyema rangi hiyo wakieleza kuwa ina mvuto na itamfanya anayevaa kuwa na mwonekano wa aina yake.

Akizungumza na Mwananchi, mbunifu wa mavazi Mwamvi Lyaunga, anaielezea rangi hiyo kuwa inang’aa vizuri ikivaliwa mwilini na haichagui rangi ya ngozi ya mwili, hasa ikibuniwa vizuri.

“Peach fuzz ni rangi inayong’aa, hasa wakati wa usiku hasa ubunifu ukifanyika vizuri katika vazi hilo.”

Pia alieleza namna ambavyo unaweza kuvaa vazi hilo na kupata mwonekano wa kipekee, vazi la rangi ya peach huweza kuchanganya na rangi nyeupe, nyeusi na kahawia.

Vitambaa vya maua yenye nakshi ya rangi ya peach navyo hubamba, hasa ukichanganyia kitambaa cha peach plain.

Akizungumza na Mwananchi, Muyonga Jumanne anasema wanaume wengi huwa vipofu wa rangi, ila anaamini kupitia wabunifu wa mitindo anaweza kupata vazi zuri la suti.

Pia kuna baadhi ya nguo kama tisheti na raba za rangi ya peach huleta mwonekano mzuri na wa kuvutia.