Shule zimefungwa, ni zamu ya wazazi kufunda watoto wao

Shule zimefungwa, watoto wamehitimu muhula wa kwanza wa masomo.

Ni wazi kuwa kila mzazi sasa analo jukumu la kukaa karibu na watoto wake kwa lengo la kuzungumza nao kuhusu yaliyojiri shuleni katika muhula walioumaliza na kupanga watauanzaje muhula wa pili wa ngwe ya lala salama kwa mwaka huu wa masomo wa 2024.

Lakini pia ni muda muafaka kwa wazazi kukaa na watoto hao ambao baadhi wanasoma shule za bweni ili wawafundishe vitu mbalimbali, ikiwemo maarifa ya jamii yatakayowaongoza katika maisha yao ya kila siku.

Kiuhalisia, watu wazima huwa tuna tabia zinazoendesha maisha yetu ya kila siku. Tunasalimia wafanyakazi wenzetu, majirani, wapita njia, ndugu pamoja na kuwajulia hali na kuwauliza kazi na biashara zao zinaendeleje.
Wakati mwingine huwa tunaingia kwenye mitafaruku na kuombana radhi. Yote haya huibua hisia tofauti ambazo tunaweza kukabiliana nazo kwa namna inayokubalika na jamii kwa kuwa ndivyo busara za utu uzima zinatutaka kuwa hivyo.

Watoto pia hupitia michakato kama hii, ila tofauti ni kwamba, wao hawajawa na uwezo wa kukabiliana na hisia hizi kwa kila jambo na watu wanaokutana nao.

Hata hivyo, ili watoto waweze kuwa na mahusiano bora na marafiki zao pamoja na watu wanaowazunguka na kuwa watu wazima, wenye wajibu na busara, basi sisi kama wazazi inatupasa kuwafundisha maarifa mema yaliyopo katika jamii.

Kwanza tuwafundishe kufuata maelekezo. Hili ni jambo muhimu sana kwa watoto kujifunza, hasa wakiwa katika umri mdogo.

Mzazi unaweza kuanza kwa kuwaelekeza kufanya majukumu madogo madogo kama vile kuhifadhi vitu vyao vya kuchezea mahali pamoja baada ya kumaliza kucheza, kuhifadhi viatu, mabegi yao ya shule sehemu maalumu pamoja na vitu vingine vya nyumbani kama vile visu, chumvi sukari, rimoti nk.

Wasisitize mara kwa mara kwamba mtu akiwaelekeza jambo wanatakiwa kumtazama usoni na kumsikiliza kwa umakini. Hii siyo tu ishara ya ukarimu, bali pia huwasaidia kuelewa maelekezo.

Jambo la mwisho ni kuomba radhi. Kukosea ni sehemu ya ubinadamu wetu, hivyo kujua kuomba msamaha ni kitu cha muhimu sana kwa mtoto kujifunza akiwa nyumbani, shuleni na hata katika maisha yake ya kila siku. Mfundishe kuomba msamaha kutoka moyoni, kwa kumaanisha na siyo kutafuta sababu ya kuthibitisha matendo yake.

Tabia huundwa, tujitahidi kutumia muda huu wa likizo kuwajengea watoto wetu umahiri wa kuishi na watu vizuri.

Nasema hivyo kwa sababu kuna watoto wanaosoma shule za bweni, hawa mara nyingi huwa hawajui maana ya kuishi na watu vema kwa sababu ya mazingira.

Utafiti wangu mdogo nilioufanya, nimebaini wazazi wengi, hasa waishio mijini, hupendelea kuwapeleka watoto wao shule za bweni kwa sababu kadha wa kadha, ikiwamo ya kusaka elimu bora.

Lakini wengine wanapata msukumo huo kwa sababu tu hawana wasaidizi wa kazi nyumbani.

Wengi wanaona mazingira ya shule za bweni yanaweza kuwa salama zaidi kwa watoto wao kwa malezi na kusoma.

Lakini kuna siku nilifanya mazungumzo yasiyo rasmi na wenzangu ofisini juu ya hilo, baadhi waliniambia wapo wazazi wanaoamini mtoto anapopata uzoefu wa maisha ya bweni anakuwa kwenye nafasi ya kujifunza stadi za maisha vizuri kuliko anapoishi na familia yake nyumbani.

Wapo pia waliolipinga hilo wakidai shule za bweni si nzuri kwa watoto wenye umri mdogo kwa sababu kuna hatari ya wao kujifunza tabia mbovu zinazoweza kuathiri maisha yao.

Sasa ili kuondoa mkanganyiko huo wa kimtazamo, nilifanya utafiti mwingine mdogo wa kuwalinganisha wale wanaosoma shule za bweni na wale wanaotokea nyumbani kwa kuangalia upande wa makuzi, taaluma na wanavyoweza kumudu maisha nje ya wazazi wao, walimu na wanafunzi wenzao wanaoishi nao shuleni kisha nikarudi kwa wataalamu wenye fani yao wanisaidie kupata majibu.

Anasema shule za bweni zenye wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi, mara nyingi huwapangia wanafunzi ratiba ya nini wanapaswa kufanya kwa muda.

Lakini nilimwambia hiki ukisemacho ni sawa, kwa sababu ametazama upande wa elimu tu, nikamuulizi hivi mafanikio ya kitaaluma yanatosha kuwa kipimo cha makuzi bora ya mtoto? Na je, ufaulu usioambatana na tabia njema itakayokwenda kumjenga kimaisha, inasaidia nini kwa mtoto wakati unadumaza eneo nyeti la makuzi yake?

Kinyume na imani ya wengi wetu, watoto wanaosoma shule kutokea nyumbani mara nyingi huwazidi wenzao wanaosoma bweni kwa stadi za maisha.

Mara zote malezi ya bweni humfanya mtoto aamini watu wengine ndio wenye wajibu wa kumfanyia kazi za mikono. Kuna mwanafunzi mmoja nimezungumza naye ambaye maisha yake yote ya shule amesoma akitokea bweni.

Anasema amemaliza shule hajui hata kupika.

Nikamuuliza akianza kujitegemea atafanyaje, akasema ataajiri mtumishi. Mtoto kama huyu unaweza kujiuliza mwenyewe maisha yake ya baadaye yatakuwa ya aina gani. Wazazi tujitafakari.

Nilipojaribu kulidokeza hilo kwa wenzangu kwenye mazungumzo yetu, baadhi walisema dunia ya sasa si ya jana, sayansi na teknolojia imerahisisha kila kitu.

Zipo nyenzo nyingi za kisasa zinazotumika kwa sasa kwa kazi zote za mikono zifanywazo nyumbani.

Lakini hili ni jibu sahihi kwa makuzi ya mtoto? Huenda jibu likawa hapana, kwa sababu wakati baba na mama wakiyafanya haya, yeye hayaoni kwa sababu anakuwa shuleni.

Kwa sababu familia inayoishi pamoja ni eneo muhimu sana kwa makuzi ya watoto, hasa wale wadogo, sasa kipindi hiki cha likizo ni muafaka kufundishana.

Tusipende kuishi kwa kukariri, tunawaumiza watoto bila sisi kujua, pambana na familia yako kwa kuijengea misingi imara.
Familia ni eneo muhimu kwa mtoto anayeendelea kukua.

Ubora, utaratibu wa malazi na fursa za michezo, mawasiliano ya mara kwa mara ya wazazi na mtoto, hayo ni mambo ya kuzingatia.