Leonarda Cianciulli: Muuaji aliyetengeza keki, sabuni kwa damu na nyama za watu

Muktasari:

  • Moja ya majina maarufu kwenye historia ya Italia ni 'Soap-Maker of Correggio', (mtengenezaji sabuni wa Carregio),  ambaye ni mwanamke muuaji aliyeitwa Leonarda Cianciulli.

Italia. Ushawahi kula keki halafu ikawa tamu kiasi cha kuisifia na kutamani isiishe? Mara nyingi keki hizo hunogeshwa na sukari na baadhi viungo mbalimbali ambavyo mpishi huviweka.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wakazi wa maeneo ya Correggio huko nchini Italia waliokula keki na kuzisifia kwa utamu wake bila ya kujua zilitengenezwa kwa kutumia damu na nyama za watu.

Moja ya majina maarufu kwenye historia ya Italia ni 'Soap-Maker of Correggio', (mtengenezaji sabuni wa Carregio),  ambaye ni mwanamke muuaji aliyeitwa Leonarda Cianciulli.

Mwanamke huyo kutoka Italia amekuwa akitajwa hadi leo kutokana na stori yake ya kikatili ya kuua kisha kuitumia nyama na damu za watu aliowaua kutengeneza sabuni na keki alizokuwa akizigawa na nyingine akaziuza kwa majirani zake.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Leonarda Cianciulli alizaliwa mwaka 1894 huko Montella, Avellino nchini Italia.

Akiwa msichana alijaribu kujiua mara mbili mwaka 1917 lakini ilishindikana kwa kuokolewa.

Alibahatika kufunga ndoa na Raffaele Pansardi aliyekuwa mhasibu wa Serikali.

 Akiwa ndani ya ndoa alibahatika kupata mimba 17 lakini tatu ziliharibika na watoto 10 wakafariki dunia wakiwa na umri mdogo.

Jambo hilo lilikuwa likimpa mawazo sana Leonarda kwa kuwa, aliwahi kutabiriwa na mtu wa masuala ya nyota kwamba, atapata mimba na kuzaa lakini watoto wake wengi watafariki dunia.

Hivyo, hadi kufikia hapo alikuwa na watoto wanne tu,  na ilipofika mwaka 1939 mtoto wake wa kiume aliyekuwa kipenzi chake, alijiunga na jeshi kwa ajili ya maandalizi ya kupambana kwenye Vita vya Pili vya Dunia.

Leonarda aliingiwa na wasiwasi sana na akapanga kumlinda mtoto wake kwa gharama zote, baada ya kuhangaika sana kwa makuhani na watu wa masuala ya nguvu za giza, aliambiwa atoe kafara kwa kuua watu ili mtoto wake awe salama huko vitani alipokuwa anaenda.

Mtu wa kwanza kumfanyia mauaji alikuwa ni mwanamama Faustina Setti ambaye hakuwahi kuolewa kwenye maisha yake, hivyo Leonarda aliamuahidi angempeleka kwenye Jiji la Pola kumtafutia mume, lakini alimsihi kutotangaza kwa mtu yeyote juu ya taarifa hizo.

Pia, akamtaka aandike barua za kusema kwamba amefika salama Pola ili akiondoka iwe rahisi kwa ndugu zake kujua ameenda wapi.

Faustina akafanya hivyo na siku kadhaa kabla ya safari alimtembelea Leonarda na siku hiyo hiyo akauliwa kwa shoka.

Katika mahojiano Leonarda alisema alipomuua, alimkata vipande vipande kisha akaviweka kwenye beseni na kuchanganya na kilo saba za Caustic soda, kisha akakoroga mchanganyiko huo mpaka vipande hivyo vikayeyuka.

Baada ya hapo alimimina kwenye ndoo kadhaa na kumwaga kwenye tanki la maji taka lililokuwa karibu.

Damu iliyosalia aliisubiri hadi igande, akaweka kwenye oveni, akaiponda na kuchanganya na unga, sukari, chokoleti, maziwa na mayai kisha akakanda viungo vyote kwa pamoja, baada ya hapo alitengeneza keki nyingi za chai na kuwapa wanawake waliokuja kumtembelea, ingawa yeye na mumewe walizila pia.

Mauaji ya pili aliyafanya kwa mwanamke mwingine Francesca Soavi aliyemuahidi kwamba angemsaidia kumpeleka Jiji la Piacenza kwa ajili ya kupata kazi kwenye shule ya watoto wa kike.

Kama alivyofanya mauaji ya kwanza, huyu pia alimuambia aandike barua kisha siku kadhaa kabla ya kuondoka alimtaka aende nyumbani kwake akampa kinywaji kilichokuwa na dawa.

Baada ya hapo akamuua kwa kutumia shoka na mwili wake akautengenezea tena sabuni na keki.

Mauaji ya tatu na ya mwisho kufanywa na mwanamke huyo ni ya Virginia Cacioppo ambaye utaratibu ulikuwa ni ule ule wa awali ingawa huyu aliamuahidi kumpatia kazi ya kuwa katibu muhtasi kwenye moja ya ofisi huko Florence.

Siku chache kabla ya safari husika, aliwasili nyumbani kwake akamuua na kuutumia mwili wake kwenye kutengeneza sabuni na keki kama kawaida.

Baada ya hapo, shemeji wa Cacioppo, Albertina Fanti, alitilia shaka kutoweka kwake ghafla na alikuwa amemwona mara ya mwisho akiingia kwenye nyumba ya Cianciulli.

Aliripoti suala hilo kwa polisi akafungua jalada la uchunguzi na akamkamata Cianciulli ambaye hakukiri mauaji hayo hadi tuhuma yao ilipomwangukia mwanaye, Giuseppe Pansard, kisha akatoa maelezo ya kina juu ya kile alichokifanya kumwondolea mwanaye lawama.

Baada ya kukiri makosa yake Mahakama ilimhukumu kwenda gerezani miaka 30, alifariki dunia Oktoba 15, 1970 kwa matatizo ya ubongo.