Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fuata hatua hizi kuchagua fani

Wazazi hawana budi kuwasaidia watoto wao kuchagua fani za kusomea maishani. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Kidato cha tano ndipo mahala mwanafunzi anapoanza kujenga msingi wa taaluma au fani aitakayo maishani kwake. Ni msingi unaoanza kwa uchaguzi wa masomo matatu muhimu kwa elimu ya kidato cha tano na sita.

Kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, kunaashiria kuanza kwa safari ya masomo ya kidato cha tano kwa wanafunzi waliofaulu mtihani huo.

Kidato cha tano ndipo mahala mwanafunzi anapoanza kujenga msingi wa taaluma au fani aitakayo maishani kwake. Ni msingi unaoanza kwa uchaguzi wa masomo matatu muhimu kwa elimu ya kidato cha tano na sita.

Uzoefu unaonyesha kuchagua fani limekuwa jambo gumu kwa watu wengi hususan wanafunzi waliopo shuleni na vyuoni. Makala haya yakidurusu rejea mbalimbali yanajaribu kuwasaidia wanafunzi kujua njia bora wanazoweza kutumia kujua ndoto ya maisha yako kitaaluma.

Kwa wale wanaotarajia kuingia kidato cha tano hivi karibuni, makala haya pia ni muhimu kwa kuwa yatawawezesha kujua namna ya kufanya uchaguzi mzuri wa masomo yao, maarufu kwa jina la michepuo (combinations).

Aidha, umuhimu wa makala haya hauishii tu kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na kidato cha tano, maudhui yake ni muhimu pia kwa wale waliokosa alama za kujiunga na kidato cha tano, lakini wana nia ya kujiendeleza kwa kutumia fursa nyingine za kielimu.

Wasomi na wataalamu katika eneo hili wameandika mambo mengi na tofauti kuhusu jinsi ya kung’amua fani katika maisha ya mtu. Kifupi, kuna hatua kadhaa unazoweza kuzitumia kufanikisha zoezi hili.

Hatua ya kwanza: Kila mwanadamu ana mapenzi na utashi binafsi, ili kufanikiwa katika hili hatuna budi kuwa na malengo kama wanadamu. Katika hatua hii, zungumza na moyo wako, fikiri kile unachokipenda rohoni.

Hatua ya pili: Chagua unachokitaka kwa kuwa ndivyo utashi na mapenzi yako yanavyokuelekeza. Si vibaya kama utakuwa na orodha ya vile unavyovitamani kama fani zako za baadaye. Kumbuka kuipanga orodha hii kwa vipaumbele, kiweke mwanzoni kile unachokitamani zaidi.

Hii ndiyo hatua ya kuusikiliza moyo wako. Fani zipo nyingi kama tutakavyoziona baadaye. Moyo unasemaje, je, unataka kuwa mhasibu, mwanasheria au mwalimu? Orodhesha fani zote unazozitamani katika nafsi yako.

Hatua ya tatu: Jifunze undani wa kila chaguo kwa kusoma, kufuatilia taarifa zake au kwa kuzungumza na watu. Kuna faida nyingi za kuujua undani wa fani uipendayo ikiwamo kujua kama fani hiyo inalipa kimaisha ama la. Pia kupata maarifa ya msingi kuhusu fani fulani kutakuwezesha kujua ni kwa namna gani unaweza kujiajiri au kuajiriwa.

Hatua ya nne: Linganisha nguvu na udhaifu wako kwa kila chaguo. Kumbuka unaweza ukakipenda kitu lakini kikakushinda kwa sababu ya hulka, tabia au hali yako kama mwanadamu. Kwa mfano huwezi kutamani kuwa mtangazaji wa redio au televisheni ilhali una tatizo la kigugumizi.

Hatua ya tano: Ukifika hapa unaweza sasa kufanya uamuzi wa mwisho kwa kuchagua fani uipendayo, inaweza ikawa moja au fani kadhaa ulizozipanga kwa kufuata vipaumbele.

Hatua ya sita: Sasa weka mikakati ya kulifikia chaguo lako. Kwa wewe mwanafunzi, hii ndio hatua ya kuchagua masomo yanayorandana na kile unachokitamani.

Zingatia

Kufanikiwa katika mchakato huu wa kujua fani yako unalazimika kuwashirikisha watu kadhaa muhimu wakiwemo walimu, wazazi, wana fani wenzako, marafiki wanaokujua vizuri na hata watu wengine wenye uelewa wa mambo.

Tafuta fani unayoitaka kwa kuzingatia uwezo wako wa akili kumudu mikikimikiki ya usomaji wake. Acha papara na usifuate mkumbo katika kuchagua fani ili usije kujuta baadaye. Waone waliomo katika fani uitakayo wakueleze uzuri, ubaya wake na hata jinsi ya kupata mafanikio uyatakayo.

Utapata wapi msaada?

Tanzania bado tupo nyuma kwa mambo mengi, nina uhakika hata wataalamu waliobobea katika kutoa ushauri nasaha kuhusu uchaguzi wa fani ama hawapo au wapo wachache mno.

Mtafutaji hachoki, jaribu kutafuta asasi, kampuni ama watu binafsi wanaotoa huduma hizi huku ukikumbuka kuwa huduma hiyo nayo ni bidhaa iliyo sokoni kwa sasa. Jiandae kuingiza mkono mfukoni.

Fuatilia taarifa za watu waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali na soma machapisho kukuza uelewa wa mambo. Ndani ya vitabu kuna utajiri ambao Watanzania wengi tunaukosa kwa kuwa hatuna utamaduni wa kusoma vitabu na majarida. Kuza fikra kuhusu maisha kwa kusoma majarida. Jaribu leo njia hii utayaona matunda yake.

Kuna vitabu maalum kuhusu uchaguzi wa fani, sina ufahamu wa kutosha na vitabu vya Kiswahili lakini kwa wanaoijua lugha ya Kingereza wanaweza kukitafuta kitabu kiitwacho A Structured Guide to Career Selection kilichoandikwa na James O ‘Sullivan

Kwa wajuzi wa mitandao ya kompyuta wana fursa nzuri ya kupitia tovuti zinazozungumzia kwa kina kuhusu chaguzi za fani mbalimbali. Tovuti kama www.collegegrad.com ni maarufu katika uwanja huu.

Umefikiria fani zifuatazo?

Kuna fani ambazo ni muhimu kwa mazingira ya Tanzania na hata yale ya kimataifa. Baadhi ya fani hizi ni kama Sheria, Udaktari, Uandishi wa habari, , Ualimu, Uhandisi, , Biashara, Ufundi, Ukutubi, , Utalii, Muziki, Ukalimani, Fasihi, Utunzi wa vitabu, Ushauri nasaha

Ieleweke kuwa hizi ni fani kwa ujumla wake, bado kila fani ina maeneo maalum zaidi unayoweza kuamua kujikita. Kwa mfano, ndani ya masomo ya biashara unaweza kukumbana na fani ndogo kama Uhasibu, Masoko, Uboharia Utawala wa Biashara na fani nyinginezo.

Kwa wanaoutamani Uandishi wa Habari, unajua kama mgawanyiko wake ni mkubwa? Jiulize unataka kuwa nani kwa kuwa upo uandishi wa habari za magazeti, uandishi wa habari za redio, televisheni, kuna utangazaji, kuna uandishi wa tovuti, blogu na maeneo mengine.

Hujachelewa huu ndio wakati mwafaka, chagua fani ya maisha uipendayo.