Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu za kudorora ubunifu wa sayansi na teknolojia nchini

Muktasari:

Kwa mfano, wakati nchi ikiendelea kutegemea teknolojia kutoka nchi za nje, wabunifu nao wameshindwa kujikomboa kimaisha.

Licha ya kuwapo kwa  ubunifu wa kuridhisha katika  sayansi na teknolojia nchini, ubunifu huo haujafikia hatua ya kuifaidisha nchi.

Kwa mfano, wakati nchi ikiendelea kutegemea teknolojia kutoka nchi za nje, wabunifu nao wameshindwa kujikomboa kimaisha.

Wakitoa mhadhara wa wazi hivi karibuni jijini Dar es Salaam, maprofesa John Bessant na Joe Tidd kutoka  vyuo Vikuu vya Exerter na  Sussex, vyote vya  Uingereza, wanasema ubunifu huongeza biashara kwa watu,  hivyo huwa chachu ya kujikwamua kimaendeleo.

Akieleza maana ya ubunifu, Profesa  Bessant anasema kuwa  ni namna tunavyofikiria kitu fulani na kukifanya vile tunavyotaka kiwe.

“Ubunifu ni suala linalohusisha vitu vingi, ni mchazo wa vitu vingi unaohusisha elimu na ufahamu wa ndani na nje,” anasema na kuongeza:

“Ubunifu ni kile tunachofikiria na kukifanya tunavyotaka, ni kipawa cha  mtu na unatakiwa uzalishwe kwa wingi kwa ajili ya kuuza sokoni.”

Kwa upande wake Profesa Tidd anasema ili ubunifu uzae matunda kwenye jamii husika, lazima kuwe na mikakati na uungwaji mkono kutoka  serikalini na watu binafsi.

“Lazima kuwapo na mikakati endelevu ya ubunifu. Jinsi gani na wapi ubunifu huo ufanye kazi, lazima jamii pia iunge mkono. Kwa mfano, Serikali inatakiwa itunge sera endelevu, sekta binafsi inatakiwa kutoa mchango kwa miradi ya ubunifu,” anaeleza.

Akifafanua zaidi anasema kuwa inawezekana kwa mbunifu kutengeneza mamilioni ya fedha kila mwezi bila kuwa na elimu kubwa, mtaji wa kuwekeza na bila hata kuajiriwa.

Anatoa mfano wa kampuni ya kutengeneza nguo ya Zara Inditex ya Uingereza iliyoanza kwa mtaji wa Sh40,000 mwaka 1963,  na sasa ina maduka 950 katika nchi 70 duniani yenye thamani ya Sh13 trilioni.
Maendeleo duni ya ubunifu chini
Akizungumza kuhusu ubunifu wa teknolojia nchini, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,  Profesa Makame Mbarawa anasema kuwa  ubunifu  unahitaji jitihada za wadau ambao ni vyuo vikuu na sekta binafsi.

“Ubunifu wa teknolojia unafanyika kwa ushirikiano wa nguzo tatu ambazo ni Serikali, sekta binafsi na vyuo vikuu. Ndiyo maana tunawataka wadau hawa kushirikiana na Serikali ili kuuhamasisha,” anasema Profesa Mbarawa na kuongeza:

“Sisi kama Serikali tunafanya marekebisho ya sera ya sayansi na teknolojia ili iendane na hali ya sasa. Kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech),  tumechukua baadhi ya vijana na tunawafundisha ili wawe chachu ya ubunifu.”

Akitaja zaidi mikakati zaidi ya Serikali, Profesa Mbarawa anasema kuwa mwaka 2010, Serikali ilitenga Sh19 bilioni kwa ajili ya utafiti wa sayansi na teknolojia, na kuanzisha chuo cha sayansi na teknolojia cha ngazi ya shahada ya uzamivu na kuboresha vyuo vingine.

“Serikali inafanya jitihada kubwa kukuza ubunifu,  lakini bado sekta binafsi haijajitokeza kuunga mkono na hata vyuo vikuu,” anasema.

Akitoa mifano ya nchi zilizoendelea kwa teknolojia kama vile Korea Kusini, anasema kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia yalichochewa na sekta binafsi.

“Korea imeendelea kwa teknolojia kutokana na msukumo wa sekta binafsi. Angalia bidhaa kama Samsung au Hyundai, siyo za Serikali, ni za watu binafsi. Kwa hiyo kama sekta binafsi zitajitokeza tutafika mbali,” anaeleza.

Aidha, anabainisha kuwa Tanzania inaweza kuiga teknolojia za nje na kuzibadilisha kuwa za ndani.

“Korea kwa mfano, imechukua teknolojia za kutengeneza silaha kutoka Urusi, Marekani na Ulaya na kuzibadilisha na sasa wanatengeneza silaha zao. Siyo silaha tu, bali hata teknolojia za mawasiliano na usafiri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitivo cha Sayansi cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam, Dk Costancia Rugumamu , anasema kazi ya vyuo vikuu ni kuzalisha wataalamu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Dk Rugumamu ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika la Sayansi Teknolojia na Ubunifu kwa wanawake, anasema kumekuwa na mwamko mkubwa kwa wananchi kujifunza masuala ya teknolojia nchini.

“Kazi ya vyuo vikuu ni kuzalisha wataalamu wa sayansi na teknolojia. Kwa njia hiyo tunahamasisha maendeleo ya teknolojia nchini,” anasema na kuongeza:
“Ni kweli tunawafundisha wanafunzi kuwa wataalamu, lakini inategemea na mazingira ya ufundishaji yaliyopo.

Tunachokifanya ni kuwahamasisha kuwa wanasayansi. Ili upate mtaalamu lazima umpe motisha,” anasema.

Akizungumzia maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini, Dk Rugumamu anapinga dhana kwamba Tanzania haijafanya lolote katika uvumbuzi wa kisayansi.

“Hayo ni maneno ya mitaani tu, wanaosema hivyo waje kwenye vyuo vyetu waone jinsi tafiti zinavyofanywa na matokeo yake. Kwa mfano nenda pale Taasisi ya teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), utaona uvumbuzi mwingi umeshafanyika na bado tafiti zinaendelea kufanyika,” anasema.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Sekta binafsi nchini (TPSF) Godfrey Simbeye anasema kuwa mfuko huo umekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wabunifu wa sayansi na teknolojia.

“Sisi watu wa sekta binafsi tunachofanya ni kuhakikisha kuwa sera bora zinakuwepo kwa ajili wabunifu na kuwatia moyo ili waendelee kubuni,” anasema Simbeye.

Hata hivyo anasema kuwa hana uhakika kama Serikali inatoa ruzuku kwa wabunifu wa sayansi na teknolojia.