MAKALA YA UCHUNGUZI: Waganga wanavyowafilisi wanaosaka utajiri, bahati (4)
Muktasari:
Habari yetu ya uchunguzi wa ujanja wa waganga kufilisi watu wenye hamu ya kupata utajiri na ajira jana iliishia siku ya miadi ambapo mchunguzi wetu aliwasiliana kwa simu na mganga kupata majibu ya wafalme, badala yake alianza kulalamika lazima atekeleze alichoambiwa, yaani afanye mapenzi na Malijari. Mazungumzo kati ya mchunguzi na mganga yaliendelea hivi…
Aliendelea kunieleza kwa sauti ya ukali kuhusu kosa langu la kutompigia simu mtu wa kufanya naye mapenzi niliyetafutiwa na wafalme, akisisitiza kuwa hiyo ni nguvu ya majini.
“Hiyo ni nguvu ya majini. Walikuambia watakutafutia mtu na ni kweli wamekutafutia,” alisema Mganga.
Aliendelea kusisitiza kuwa nilitakiwa kumshikilia huyo mtu labda na yeye angenisaidia kwa sababu anaongozwa na majini, na kwamba angekuja kushtukia baadaye wakati nikiwa tayari nimefanikiwa.
“Jana wafalme walinisumbua, ‘vipi mjukuu wetu’, ‘vipi mjukuu wetu’ sasa naomba unihakikishie zoezi hili utalimaliza leo. Nilimjibu ndiyo, akasema kwa hiyo niwaambie wafalme utalimaliza leo?” Nilimjibu ndiyo. Alikubaliana na mimi na kusisitiza nijitahidi.
Lakini, Mganga aliendelea kunihoji kuhusu nilichoambiwa na wafalme kama kuna kitu kingine cha kufanya zaidi ya mapenzi. Nilimueleza nilichoambiwa na wafalme ni hicho tu.
“Mtafanya tendo hilo mara ngapi, ukikutana na mpenzi wako huwa mnafanya tendo la ngono mara ngapi?” aliuliza lakini nikajifanya sikusikia vizuri na kumuuliza kwa namna ya kutaka arudie swali lake.
“Ukikutana na mpenzi wako huwa unafanya naye mara ngapi mpaka akaridhika?” Nilimjibu mara moja. Hata hivyo, alionyesha kushangazwa na jibu hilo na kunihoji tena. “Mara moja tu basi! Na yeye anajihisi ameridhika na wewe unalidhika?” Nilimjibu ndiyo.
Kuonyesha kwamba Mganga huyu ni hatari kwa masuala ya ngono, aliniuliza tena, “Samahani najaribu kwenda huko mbali, lengo ni kutaka kujua ili niweze kukusaidia, samahani ukifanya naye huyo baba (Malijari) akun… au wewe utam…? Nikamuuliza (hicho alichokitaja ndiyo nini), kwa namna alivyoonekana anapenda mambo ya ngono alisema: “Nyinyi si vijana bwana au hujawahi (anataja hicho kitendo kichafu kama niliwahi kumfanyia mpenzi wangu au yeye kunifanyia). Nilimjibu sijawahi kufanya kitendo hicho wala kufanyiwa.
Lakini, Mganga badala ya kuzungumzia matatizo yaliyonipeleka kwake, yeye alijikita zaidi kwenye masuala ya ngono kwa kuendelea kunihoji kuwa huyo mwanaume (jini) nitafanya naye mara ngapi?
Nilipomjibu kwamba wafalme waliagiza nifanye naye mara moja alikubaliana na hilo na aliendelea kunihoji kama nilitekeleza agizo lake la kuandaa nywele za sehemu za siri.
Hata hivyo, nilimjibu sikuwa nimeziandaa huku nikimtupia swali la kutaka uhakika kama kweli aliniambia niziandae. “Ndiyo nilikwambia baada ya kuniambia umekosa mchanga wa makaburini,” alijibu.
Nilishangazwa na kauli hiyo, nikakumbuka hakuniambia nifanye hivyo, badala yake aliniambia nipate majimaji ya ukeni na mchanga wa makaburini, nikahisi huenda anawaeleza watu wengi tofauti.
Mganga akijikita kwenye ngono
Aliniambia, “Jana wewe uliniambia mchanga umekosa au siyo, nikakwambia utafute nywele za sehemu za siri.” Nilimjibu hukuniambia hivyo. Lakini, aliendelea kunihoji “sasa unaweza kuupata mchanga wa makaburini?” Nilipomjibu ndiyo aliongeza swali akitaka kujua nina kitu gani kwa wakati huo?
Nilimhoji tena Mganga kutaka kujua alimaanisha nini kwenye swali lake, kumbe alitaka kujua kama nina dawa au zindiko lolote mwilini. Nilipomjibu sina aliendelea kuniuliza akitaka kujua huyo mwanaume (jini) aliniambia wakati nawasiliana naye alikuwa wapi. Nilimjibu yuko Kariakoo na alikuwa akijiandaa kwenda Kawe.
Mganga alinitaka nimalizane na huyo mwanaume (jini) siku hiyo, huku akiendelea kunihoji kama kuna sehemu nilifikiria kuomba kazi. Nilimweleza nilitaka kuomba kazi katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Fezza.
Aliniuliza ilipo shule hiyo na nilipomueleza ipo Kawe, alileta hoja nyingine akitaka nikubali kupewa pesa za majini ili niweze kuendesha maisha yangu huku nikiendelea na kazi ya kufundisha.
Nilipomjibu kwamba ushauri wake siyo mbaya, alileta swali lingine akitaka kujua kama niliishawahi kutumia pesa za majini. Nilimjibu sijawahi kutumia ndipo akasema:
“Siyo masharti magumu, masharti si ya kuua, utaambiwa tu utoe misaada kwa watu wasiojiweza na fedha hizo utazipata. Majini yatakuwa yanakuletea yenyewe ukiyaomba”.
Aliniambia majini niliyoongea nayo ndiyo nitakuwa ninayaomba (fedha) kupitia kwake (Mganga huyo) na yenyewe yatanielekeza mahali pa kuzichukua au yataniletea ndani au sehemu yoyote ile.
Nilimwambia Mganga kuwa haina shinda ninachotaka ni utajiri na nipate kazi tu. Alisema cha kufanya ni kukamilisha zoezi la kufanya mapenzi na jini lililokuja kwa kupitia kijana aliyekosea namba, yaani Malijari.
Baada ya kuelewana, Mganga huyo alinitaka nimtafute Malijari kwa kumpigia simu ili kujua sehemu alipo nami niende tukafanye tendo la ngono.
Mawasiliano na jini
Nilifanya hivyo, nikampigia Malijari lengo likiwa ni kutaka kuonana naye na kumshawishi kimahaba ili akubali kufanya ngono na mimi.
Ilikuwa ni asubuhi baada ya kuongea na Mganga huyo nilimpigia Malijari ambaye alipokea huku akisema; “niko na mke wangu, naomba nitumie meseji,” baada ya kusema hivyo alikata simu.
Nilimtumia ujumbe mfupi wa maneno uliyosomeka ,”samahani kaka kwa usumbufu, mimi nimekupenda toka jana, usiku sijalala naomba tuonane leo mpezi wangu najua nakusumbua ila moyo wangu umekupenda.”
Malijari huyo (jini) alinijibu kwa kuniuliza “wewe uko wapi”nilimjibu “niko Buguruni kaka” aliuliza tena , “kwahiyo ulikuwa unasemaje?”
Nilimjibu, “naomba tuonane basi” akauliza “kwani kuna nini au unataka tufanye nini? Nilimjibu “Nataka tufanye mapenzi ‘dear’nina hamu kweli toka ulivyonipigia jana mwili wangu ulipata msisimko. “
Alinijibu; “naogopa mimi” nikamuuliza unaogpa nini? Alijibu, “sikujui halafu mimi niko Kawe” Nilimwabia si tukionana ndiyo mwanzo wa kujuana jamani? Nakuomba tafadhali.
Alijibu, akitaka nimfuate Kawe lakini mapenzi tukafanyie Mbezi Beach. Nilisita kwa kumueleza kuwa ni mbali alinijibu kama sitaki basi na pia nikichelewa sitomkuta atakuwa amekwenda hospitali.
Nililazimika kumsihi kwa kumueleza namfuata naye alikubali huku akisisitiza niwahi kwakuwa jioni alikuwa na safari ya kwenda hospitali kumuona mgonjwa. Nilipomwambia najiandaa alitaka kujua nitavaa chupi ya rangi gani.
Uso kwa uso na jini
Safari ya kuona na jini, kumbuka lengo ni kwenda kufanya tendo la ngono ili zipatikane mbegu zangu za kike kwa ajili ya kufanyia dawa ya kufufua nyota yangu na kupata pesa za majini na utajiri.
Katika safari hii niliongozana na mpigapicha na dereva, lengo likiwa ni kutaka kumuona huyo jini ambaye muda wote tulizungumza naye kwenye simu, lakini kimsingi ilikuwa ikisikika sauti ya Mganga ambaye alikuwa akiibadilisha.
Nikiwa njiani muda wote Malijari ambaye awali aliniambia anaitwa Omary, alikuwa akiniuliza nimefika wapi huku akisema kama nina fedha za kulipia chumba au alipie yeye.
Nilimjibu alipie chumba kwani mimi sikuwa na fedha, Omary (Jini) alikubali na kunitaka nikifika Mbezi nimwambie ili anielekeze mahali pa kwenda.
Nilifika Mbezi nikampigia simu na alinitaka nishuke kituo kinachoitwa Africana, nikiwa na wenzangu tulifika kituo cha Africana tukasogea mbele kidoga na kituo hicho kisha nilimpigia simu kuwa nimefika.
Malijari huyo alinitaka nimsubiri kidogo, wakati nikimsubiri, nikampigia Mganga kumwabia tayari nimeshafika eneo ambalo nimeambiwa na jini tukutane.
Mganga huyo alisema sawa ila nihakikishe namridhisha ili wafalme wafurahi, nilimhakikishia nitafanya hivyo.
Baada ya muda wa nusu saa nikampigia Malijari ambaye aliniuliza namna nilivyovaa, lakini aliniuliza kama nina fedha kidogo kiasi cha Sh1,000.
Aliniambia nichukue bodaboda lakini kabla ya kuondoka nimpe simu dereva ampe maelekezo ya sehemu ya kumkuta ambayo aliitaja ni eneo liitwalo The Father gate Santaliam Clinic.
Nilipanda kwenye pikipiki hiyo na kuondoka nikiongozana na mpigapicha hadi eneo hilo. Nilimlipa bodaboda kisi cha Sh1,000 na kumuomba aondoke.
itaendelea