Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama chanzo cha tatizo la haja kubwa kwa mtoto-Mtaalamu

madaktari wakiendelea na kazi wodini

Muktasari:

Tatizo hili linawaathiri zaidi watoto wa kiume na likishagundulika anafanyiwa upasuaji hapo hapo, lakini kwa watoto wa kike huweza kukaa wiki mbili au mwezi

Dar es Salaam.Ugonjwa wa watoto kutoka utumbo nje, umeonekana tishio na unashika namba mbili katika magonjwa yanayosumbua watoto ukiachia ule wa Hernia (Kidole tumbo) ukiwa unashika nafasi ya kwanza.

Ugonjwa huo ambao kitaalamu unaitwa ‘Anorectal Malformations’ ni muunganiko wa matatizo ambayo yanaathiri mifumo ya haja kubwa na ile ndogo kwa watoto wa jinsi zote na kwamba ili kutambulika kunahitaji utaalamu wa hali ya juu.

Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa upasuaji Muhimbili, Zaituni Bhohary anasema tatizo hilo ni kwamba njia ya haja kubwa inasimama na hivyo kusababisha utumbo mkubwa kupanuka, hivyo wanachofanya cha haraka kuokoa maisha ya mtoto ni kumtoboa ubavuni na kumwekea njia ya muda.

“Tatizo hili kuna watoto wanazaliwa na hapo hapo inagundulika wana hilo tatizo. Hivyo tunawafanyia upasuaji huo wa kuwatoboa ubavuni haraka (Emergency Operation) na pia kuna wengine wanagundulika baada ya wiki mbili mpaka mwezi mmoja.

“Tatizo hili kwa watoto wa kiume ndilo linawaathiri zaidi na tukishagundua tu anafanyiwa upasuaji hapo hapo lakini kwa watoto wa kike ana uwezo wa kukaa wiki mbili au mwezi na si zaidi ya hapo, kwani kukaa zaidi kutasababisha apate maambukizo (infection) kwenye mkojo ‘UTI’ ambayo si vizuri kwa kuwa inaleta homa kali kwa mtoto na tatizo hili linasababishwa na haja kubwa kuingia sehemu ya uke wa mtoto.

“Tukishawafanyia upasuaji wa awali wa kuwatoboa ubavuni, wanakaa miezi sita au zaidi, kwa vile akishafikia umri huo ana uwezo wa kumudu dawa ya usingizi tofuati na hapo ataumia.

Tatizo hilo linasababishwa na nini?

“Sababu kubwa ya tatizo hili ni upungufu wa madini ya Folic Acid. Wanawake wengi kipindi cha ujauzito wanapuuzia kwenda kliniki mpaka dakika za mwisho na wengine hawataki kutumia zile dawa wanazopewa kwa ajili ya kupata hayo madini kwa kigezo zina ladha mbaya na wengine hawapendi harufu yake.

“Kitu kingine kinachosababisha ni stress msongo wa mawazo (stress). Ukiangalia kesi nyingi za watoto wenye tatizo hili, ni wale waliozaliwa na wanawake wasioolewa (single mothers,) ambao wanapewa mimba na wanaume wakazikataa na asilimia kubwa ni wanawake ambao hawana uwezo wa kifedha hivyo kusababisha hata lishe yao kuwa duni.

Pia alisema wasichana wanaozaa wakiwa na umri mdogo nao ni tatizo jingine linalochangia ugonjwa huu sugu kwa watoto.

“Kwa jumla wanawake ambao watoto wao wamepata tatizo wengi wamekimbiwa na wanaume, uhudhuriaji mdogo wa kliniki, vyakula duni vya kujenga mwili na pia kama mtoto hajazaliwa na tatizo hili la utumbo nje basi atazaliwa kilema.

“Takwimu zinaonyesha kila mwezi kwa hapa Muhimbili watoto 15 hadi 16, wanazaliwa na tatizo hili idadi ambayo inaongezeka kila kukicha.

Anashauri nini?

“Ningeshauri mwanamke ambaye anapanga kubeba mimba basi aanze kutumia dawa hizi zenye madini ya Folic Acid, kwani itasaidia kupunguza tatizo hili la kuzaa watoto wenye tatizo la njia ya haja kubwa na pia itasaidia kupunguza watoto wenye ulemavu.

“Kwa wale ambao wanapata mimba na kukimbiwa na wanaume basi hawana budi kuwahi kliniki ili waanze kupatiwa huduma hizo. Nadhani wanaume wanatakiwa washirikishwe kwa kiasi kikubwa kwani wao ndiyo chanzo kikuu cha tatizo hili.

“Kama wanaume wataelimishwa umuhimu wa kuhudhuria kliniki na wake/ wenza wao, basi naamini kwa kiasi kikubwa tatizo hili litapungua kwa vile kuna vitu muhimu ambavyo wataelimishwa kuanzia kwenye lishe na jinsi ya kuishi na mama mjamzito ili kuzuia matatizo kama hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yakizingatiwa yanaepukika.

Dk Bokhary pia aliitaka jamii kubadili mfumo wa maisha na kuacha kuiga mifumo ya maisha inayofanywa na watu wa nchi za Magharibi.

“Kuna mfumo mwingine unaigwa lakini hauna tija, kwa mfano watu kwenda kwenye maduka makubwa (Supper market) kununua vyakula vya makopo wanaona kama ni ‘fasheni’ lakini hawajui kama vina madhara makubwa mwilini. Vyakula vya makopo ni hatari zaidi kwa afya, huleta ongezeko la magonjwa ikamo saratani.

“Watoto wanalishwa vyakula vya makopo. Hii ni hatari sana au vile vinavyotunzwa kwenye majokofu. Ni bora wakalishwa vyakula vinavyotoka shambani moja kwa moja, hii itasaidia kupunguza ongezeko la madhara.