Mfanyakazi anapaswa kuepuka mazingira hatarishi kazini

Muktasari:
Pamoja na hayo wafanyakazi wengi wanaposikia mtu fulani, aliyekuwa akifanya kazi katika kiwanda au kampuni hiyo amekufa hakuna hata mmoja wa wafanyakazi anayechukua hatua za kudadisi juu ya chanzo cha kifo hicho.
Tumeona mara nyingi baadhi ya wafanyakazi wakitekeleza majukumu yao, kwenye mazingira magumu yaliyo hatarishi. Hivyo, mfanyakazi hutekeleza majukumu yake katika mazingira yanayomuua taratibu huku wengine wakiwa hawajui kwamba mazingira yao yanaathiri afya zao.
Pamoja na hayo wafanyakazi wengi wanaposikia mtu fulani, aliyekuwa akifanya kazi katika kiwanda au kampuni hiyo amekufa hakuna hata mmoja wa wafanyakazi anayechukua hatua za kudadisi juu ya chanzo cha kifo hicho.
Mfanyakazi awe mwajiriwa au kibarua ni haki yake kujua juu ya baadhi hata ya kemikali zilizopo kiwandani, ambazo huuwa kwa kusababisha madhara mbalimbali mfano saratani.
Wafanyakazi wengi wanazeeka na kufa kabla ya umri wao, kwa kudhani kuwa kudai haki ni dhambi na kwa kudhani ya kuwa thamani ya utu wao ni wa chini kwa sababu ya umaskini au kwa sababu ya kukosa elimu.
Baadhi ya waajiri wengine wanajiamini wana haki ya kushusha thamani ya wafanyakazi wake, ili wapate ustawi wa kifedha.
Wafanyakazi kadhaa nchini wamepoteza viungo au maisha yao, matahalani kwa sababu ya kuvuta vumbi la madini migodini wakiwa sehemu za kazi.
Athari hizi siyo kwa wafanyakazi tu, bali hata wakazi wanaozunguka migodi hiyo.
Kuna idadi kubwa ya wafanyakazi ambao leo wanafanya kazi kwenye mazingira magumu yanayotisha. Watu wengi wanatumikishwa na waajiri wao kwenye mazingira ambayo yamezungukwa na sumu bila kujali, kwa sababu tu wanataka kupata faida kubwa.
Leo ukipita katika baadhi ya viwanda na hata baadhi ya mabohari hapa nchini, utagundua watu wanavyolishwa sumu au kujilisha sumu kwa kuamini kwamba wao wana thamani ndogo au kubwa sana kuliko binadamu wengine. Hii inajulikana sana kwamba watu wanafanyakazi katika mazingira ya aina hiyo, kwa sababu tu ya kutaka fedha na kuamini kuwa wataishi maisha magumu na familia zao wakiacha kazi.
Baadhi ya viwanda mara nyingi huwaweka wafanyakazi katika mazingira ya kujikinga na hatari, kama vile vifaa vya kuzuia hewa chafu, viatu maalumu, mavazi ya kazi au kofia pale inapokuwa kuna kiongozi anatembelea kiwanda. Akiondoka wafanyakazi wanaambiwa wavue na waendelee na kazi kama ilivyo desturi yao. Mfanyakazi anayekubali mazingira haya ni kwamba, bado hajajitambua na wala hafahamu haki zake.
Wafanyakazi kumbukeni kuwa mazingira hayo yanawaua polepole na mara nyingi huwa mnajidanganya kwa sababu hamuoni wenzenu wakianguka na kufa ghafla hapo kazini.
Lakini, wanaposikia fulani ambaye alikuwa akifanya kazi hapo kazini amekufa, na wala hawahangaiki kuuliza juu ya kifo cha mfanyakazi mwenzao kimesababishwa na nini.
Wafanyakazi mnatakiwa kujua ya kwamba kemikali, vumbi na mengineyo mengi viwandani huua kwa kumpa mtu maradhi yanayoenda polepole.
Ni muhimu sana kwa wafanyakazi kujua jambo hili kwamba katika dunia hii ambapo watu wanazidi kumezwa na tamaa na wasiwasi zaidi, kufahamu haki zao. Cha ajabu wengi wao wanakuwa wanalipwa mishahara midogo ambayo hata haikidhi mahitaji yao. Kwa hiyo haitatokea hata mara moja, baadhi ya waajiri wakasimamia usalama wa wafanyakazi wao kwa kiwango cha juu kabisa, kwa sababu kwa kufanya hivyo kutafanya watumie gharama za ziada hivyo kupunguza faida.
Ni juu ya mfanyakazi mwenyewe kujiuliza juu ya usalama wake katika kazi. Kama kuna dalili za usalama mdogo, ni vema mfanyakazi akajaribu kuangalia njia za kujitoa na kutafuta shughuli nyingine.
Kuna ugumu katika kupata ajira au kubadili shughuli, lakini kama tahadhali wafanyakazi wengi wanadhani watoto wao na wengine wanaowategemea wataathirika kimaisha.
Wananchi wanasubiri Mfuko wa Fidia (WCF) ulioanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Na. 20 ya mwaka 2008, kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika Sekta ya Umma na Binafsi Tanzania Bara ambao wataumia, kuugua ama kufariki dunia kutokana na kazi.
WCF ilianza kazi rasmi Julai 1, 2015. Lengo kuu la uanzishwaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika Sekta ya Umma na Binafsi Tanzania Bara ambao wataumia, kuugua ama kufa kazini. Kwa mujibu wa Kifungu cha pili cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Namba 20 ya mwaka 2008, wahusika wa mfuko ni waajiri wa sekta ya umma na binafsi nchini.
Christian Gaya ni mwanzilishi wa kituo cha HakiPensheni Tanzania na mshauri wa masuala ya pensheni. ([email protected] au 0655131341)