Muziki na siasa vyaacha historia Bongoflevani 2022
Muktasari:
- Kwa mwaka 2022 Bongofleva imefanikiwa kuwaleta pamoja viongozi na kufurahia muziki huo, huku baadhi ya viongozi pia wakiwa sehemu ya kutoa burudani, hii ni alama nyingine iliyoachwa kwa mwaka huu.
Kwa mwaka 2022 Bongofleva imefanikiwa kuwaleta pamoja viongozi na kufurahia muziki huo, huku baadhi ya viongozi pia wakiwa sehemu ya kutoa burudani, hii ni alama nyingine iliyoachwa kwa mwaka huu.
Baadhi ya matukio yaliyounganisha muziki na siasa ni;
1. Rais Samia & Sugu (The Dream Concert)
Katika kusherehekea miaka yake 30 katika muziki Mei mwaka huu, msanii wa hiphop Bongo, Joseph Mbilinyi, maarufu Mr. II ‘Sugu’ alifanya tamasha lililokwenda kwa jina la ‘The Dream Concert’ ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi. Liliacha historia kwa sababu ndiyo mara ya kwanza Rais Samia kuhudhuria tukio lililoandaliwa na msanii wa Bongofleva, huku Lady Jaydee, Nikki wa Pili, Mwana FA, Joh Makini, Lord Eyes, AY na G Nako wakitoa burudani.
Kitabu cha Sugu ‘Muziki na Maisha’ kilizinduliwa na Rais Samia na kuelekea mwishoni mwa The Dream Concert, Rais Samia alimpa tuzo Sugu ya kuthamini mchango wake katika sanaa na kuzalisha ajira, huku akiwa ni msanii wa kwanza Bongo kupata heshima hiyo.
2. Kikwete & Ommy Dimpoz (Dedication albamu)
Rais mtaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ndiye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albamu ya mwimbaji Ommy Dimpoz ‘Dedication’ uliofanyika Novemba mwaka huu.
Hili nalo litabaki kuwa tukio la kihistoria kwa mwaka huu ndani ya Bongofleva, hii ni albamu ya kwanza ya staa huyo tangu alipojikita kwenye muziki miaka 10 iliyopita. Utakumbuka Machi 2020 Kikwete pia ndiye alizindua albamu ya kwanza ya Harmonize ‘Afro East’, hivyo ni miongoni mwa matukio makubwa ya Bongofleva yaliyoacha alama miaka ya hivi karibuni.
3. Nyimbo tena kwa Rais Samia
Ni mwaka mwingine ambao wasanii wametoa nyimbo kuelezea mafanikio ya Rais Samia, mastaa kama Alikiba, Diamond Platnumz, Harmonize, Zuchu, Mrisho Mpoto na wengineo wamefanya hivyo kipindi cha nyuma. Kwa mwaka 2022, Lady Jaydee na Nandy ni miongoni mwa wengi waliofanya hivyo. Wimbo wa Lady Jaydee aliomshirikisha Rama Dee ‘Suluhu’, ambapo kwenye The Dream Concert, Jide aliimba kionjo cha wimbo huu na kuutoa rasmi kufika Septemba mwaka huu. Pia wimbo wa Nandy ‘Kazi Iendelee’, uliotoka Juni mwaka huu akipongeza utendani wa Rais Samia Suluhu. Kupitia wimbo huo alitanabahisha maeneo ambayo Rais Samia amefanya vizuri, ikiwamo nchi kufunguka kimataifa, maboresho ya elimu, ajira kwa vijana na kuwainua wanawake na wazee.
Ikumbukwe Juni 2021, Rais Samia alipiga simu kwenye Nandy Festival Dodoma ambapo alisema anashukuru kwa tamasha hilo kufanyika siku ambayo anatimiza siku 100 madarakani. Huyu ni msanii wa kwanza wa Bongofleva kupigiwa simu na Rais wakati anatumbuiza, kisha akafuata Zuchu akiwa kwenye shoo yake ‘Home Coming’ iliyofanyika Zanzibar.
4. Mwana FA (mbunge) - Sio Kwa Ubaya
Wimbo wake mpya ‘Sio Kwa Ubaya’ uliotoka hivi karibuni akimshirikisha Harmonize una historia kubwa kwake, kwani ndio wa kwanza kuutoa akiwa mbunge tangu alipochaguliwa Oktoba 2020.
Wimbo wa mwisho kwa Mwana FA ulikuwa ‘Gwiji’ uliotoka Juni 2022 akiwashirikisha Maua Sama na Nyoshi El Saadat, baada ya hapo akaenda bungeni akiwa ni msanii wa tatu wa hiphop Bongo kufanya hivyo baada ya Sugu na Profesa Jay.
5. Nikki wa Pili (DC) - Ronaldo
Tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Pwani hapo Juni 2021, Nikki wa Pili alikaa kimya kwa muda mrefu upande wa muziki kutokana na majukumu yake, hadi Juni mwaka huu aliposikika kwenye wimbo wa Weusi ‘Ronaldo’. Ameandika historia ya kuwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza kusikika kwenye wimbo wa Bongofleva mwaka huu.
Ronaldo anayeimbwa katika wimbo huo, ni mchezaji soka wa Ureno anayetajwa kurejea Real Madrid akiwa wa kwanza kushinda mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na binadamu mwenye wafuasi wengi kwenye mtandao wa Instagram, wakiwa zaidi ya milioni 520.