Steve Nyerere: Mie sio kuwadi, ni mzee wa koneksheni

Steve Nyerere: Mie sio kuwadi, ni mzee wa koneksheni

Muktasari:

  • Koneksheni! Ni neno ambalo limekuwa kubwa na kutambulika na watu wengi kwa maana tofauti, japokuwa wengi wanalitumia ndivyo sivyo.


Koneksheni! Ni neno ambalo limekuwa kubwa na kutambulika na watu wengi kwa maana tofauti, japokuwa wengi wanalitumia ndivyo sivyo.

Wajanja wa mjini wanakwambia unapokuwa na mtu anayeweza kukupatia koneksheni, inaleta urahisi au wepesi wa kupata taarifa nyeti kwa wakati na kufanikisha jambo lako kwa urahisi zaidi.

Miongoni mwa watu mashuhuri wanaotajwa kama daraja kwa walio wengi ni pamoja na msanii wa maigizo na mchekeshaji machachari, Steven Mengere, maarufu Steve Nyerere.

Msanii huyo anayesifika zaidi kwa kuigiza sauti za watu mashuhuri nchini, mara kadhaa amekuwa akisaidia kupatanisha, kuwakusanya wasanii pamoja kwa muda mfupi na kusaidia mambo mengi, ikiwemo kuratibu shughuli, hasa michango katika misiba na sherehe za watu maarufu.

Wakati shughuli zake nyingi amekuwa akizifanya bega kwa bega na waigizaji wa kike ambao ni maarufu, Steve Nyerere amekuwa akizungumzwa sana kuhusu madai ya ukuwadi.

Steve Nyerere amefanya mahojiano maalumu na Mwananchi na hapa amefafanua kwa kina tuhuma hizo.


MZEE WA KONEKSHENI

Anapoulizwa juu ya tuhuma kwamba amekuwa akitumika kuwakuwadia baadhi ya watu, anasema kwa sauti ya kujiamini;

“Siwezi kumzungumzia binadamu anavyokuhisi…kuna mtu anakuhisi wewe unatembea na mtu fulani. Lakini lazima niseme siwezi kuacha kujuana na Amos Makala kwa kuwa ni Mkuu wa Mkoa, mtu atakuja atasema anaongea na huyu kwa kuwa anamkuwadia huyu. Mimi nina watu tunaheshimiana nao, nina watu wananisaidia nikiwaambia tunaona tuwasaidie Bongo Muvi wana mwitikio.

“Ukiwa binadamu mkamilifu huwezi ukawa unajipa wewe tu, huwezi kufa ukakumbukwa kwa roho mbaya, bali unakumbukwa ulivyotumia ‘connection’ yako ulivyosaidia watu.

“Mimi kuna watu ambao wamepata kazi mabenki, kwenye vyama kupitia mimi, siwezi kusimama Posta au Mnazi Mmoja nikaanza kuorodhesha idadi ya watu niliowasaidia, ila ukweli mimi sio kuwadi, ila ni mzee wa koneksheni,” anasema.

Steve anasema wanaomhukumu hawamjui yeye ni nani na kwamba bahati mbaya wanaomjua hawasemi.

“Hivyo nawapuuza yale wanayoyaongea machafu kuhusu mimi, Steve ni mkubwa sana, ninavyokuwa napanda kila siku haimaanishi nitaongelewa mabaya tu.

“Kesho wanaweza kuja na kusema Steve mwizi, inategemea na mapokeo ya mtu, mwingine atakuja kusema ni hivi, kubali kupokea si kwa sababu unayafanya yale matendo, ni kutokana na ukubwa wako na hatua unazopiga kwenye maisha,” anasema.

Kwa mujibu wa Steve, anaamini kwamba mtu hawezi kuunganisha mahusiano bali ni Mungu mwenyewe. “Kuna vitu watu wanahisi huko na siwezi kukataza mtu kuhisi ujinga, mimi ni bora nikuunganishe kwenye ajira kuliko mahusiano, haya hayaunganishwi na mtu yanaletwa na Mungu.”


PENZI LA WELLU
Steve Nyerere anadaiwa kuzaa na mwigizaji wa filamu na tamthilia Bongo, Wellu Sengo na Steve amekuwa akikwepa kulizungumzia hilo.

Hata hivyo Aprili mwaka huu, Wellu alisikika kwenye vyombo vya habari akimlalamikia Steve Nyerere kutomhudumia mtoto waliyezaa pamoja.

“Sitaki kuzungumzia masuala ya mahusiano yangu, hayo mambo ni mengi, nina muda wa kuongea mambo ya msingi pekee,” anasema Steve akijibu tuhuma hizo. Pamoja na mambo mengine, hapa Steve anajielezea yeye ni nani, “Kajitu fulani hivi, kwanza kabishi, pili ni mtu ambaye sikubali nikidondoka, nasimama najipukuta naendelea na safari, juzi JK alisema ana kiherehere huyu ni kwa sababu ananijua nathubutu, kingine napenda kukaa na vijana wenzangu na wazee pia.

“Nasoma vitabu sana na nalala saa nane au tisa usiku, nikiingia Youtube nina uwezo wa kuangalia vitu vingi, inanipata ushujaa mkubwa wa kuelezea mambo mengi. Nyerere amenifanya nipende kufanya mambo mengi aliyopenda kuyafanya, nataka kujua nchi za Afrika dira ya Tanzania ni nini na changamoto wapi zipo…

“Mimi ni binadamu si mkamilifu, hivyo kuna muda nawakosea wenzangu, lakini ni mwepesi kuomba radhi,” anajielezea Steve.


URAFIKI NA JK

Kuhusu urafiki wake na JK, Steve anasema anamuona ni baba kwake. “Jakaya kwangu ni baba, bila yeye nisingefika hapa, nisingepiga hatua, amenikaribisha ndani ya moyo wake na nimemkaribisha kwenye wangu pia. Mimi ni Ridhiwan, Miraj au Khalfan, unapotokea msiba au chochote lazima nitakwenda, amenisaidia mengi siyo kunipa hela, wakati nachapwa nilikuwa namwambia nachapwa, anasema ndiyo uanaume komaa na usinune.“Amenifundisha uvumilivu na hata akinikaripia hapa ni sawasawa na Mzee Mengele baba yangu amenikaripia, si Jakaya peke yake, ni wengi wamenivusha na kuna wengi wana hofu na mimi, ooh amezunguka na mama nchi nzima, kuwa karibu na tajiri haimaanishi na wewe tajiri,” anasema Steve.


SANAA

Licha ya kujihusisha na siasa, Steve Nyerere bado anaendelea na kazi yake ya sanaa ingawa ni nadra kuonekana runingani au katika filamu, anaeleza sababu ya ukimya huo; “Juzi juzi nilionekana kwenye filamu ya ‘Juakali’ kuonyesha bado nina uwezo mkubwa, siyo kwamba sitaki kuigiza hapana, ukitaja dau dogo ndiyo kina Baba Levo wanatuita nyumbu, ukitaja dau kubwa ndiyo tunashindwa kupiga hatua, staa mkubwa Afrika Mashariki, Lupita Nyogo analipwa bei gani?

“Siwezi nikalipwa Sh500,000 nikuridhishe wewe, watoto wananifuata nyuma supastaa halafu sina hela, sina uhakika wa kula, huwezi kunichukua bila milioni 10 au 20. Na kwa sasa ukiangalia waigizaji wa tamthilia, Tanzania ndiyo bora, sasa tulipwe kutokana na uwezo wetu,” anasema na kuongeza:

“Kuna wasanii nawafahamu wanaonekana kila siku kwenye runinga hata wakipita hapo watu hawashtuki. Unachukuliwa kwa bei rahisi utachokwa haraka pia, mimi unanichezesha sini nyingi nilipe milioni 100 nijenge, nifanye mambo mengine hata nisipoigiza kipindi kirefu nitakuwa vizuri.

“Wengi wanakubali kununuliwa kwa bei rahisi kwa sababu hawana kazi ya kuwaingizia kipato, unaweza kuwa msanii ukawa na taaluma yako na kufanya kazi mahali pengine ukaingiza kipato, mimi nina miaka tisa sijaigiza filamu niligombana kisa kuuza hakimiliki. Kanumba aliuza hakimiliki leo filamu zinaonyeshwa na nani anapewa ile hela, nilikataa, nilicheza pata potea, kuna wakati lazima ufanye hivyo kujenga heshima yako,” anasimulia.


SIASA

Kuhusu siasa, Steve anasema wanasiasa wakubwa wametumia kipaji chake kufanikiwa kiasiasa na baadaye kumtupa jalalani.

“Siasa ni maisha yangu naipenda. Naielewa. Najua adhabu ya siasa, mafanikio yake, kilio na shida zake. Kikubwa najua nini nikifanya kwenye siasa wale walionipa dhamana watanisikiliza na niishije, siyo mabavu, ni utashi, kama utatumia mabavu ukiporomoka utaumizwa na wale uliowaongoza.

“Unayemsaidia anakuja kukuacha, atapata marafiki wengine atakuona wewe mbumbumbu, inabidi upokee siyo uanze kusema nilimsaidia yule hapana hamkuandikishiana. “Kwenye maisha yangu kuna watu nilipambana nao bega kwa bega, ingawa walikuwa wanapita kwenye hali mbaya, wasanii wengine waliwakimbia, mimi nilikomaa nao, lakini hawajawahi kunisaidia kitu, muda mwingine nikipiga simu hawapokei, nikiwaomba ushauri wananiambia hili haliwezekani,” anasema.


UONGOZI

Steve Nyerere anasema amewahi kujitosa kuwania nafasi kadhaa za uongozi ndani Chama cha Mapinduzi (CCM). “Nimeshakuwa kamanda wa vijana Kinondoni Bwawani kwa miaka 10, nimejenga pale ofisi moja, mashina mawili, pia nimekuwa kiongozi wa wasanii kama mwenyekiti wao kwa miaka kadhaa.

“Nimewahi kugombea ubunge na Iddi Azzan na kufanikiwa kuwa mshindi wa nne, kwa Kinondoni hili siyo jambo dogo, nilijiona nina nguvu ya kiasi gani, kuna muda kugombea si ushindi ni kujitathmini una nguvu kiasi gani, nikatoka hapo nikaenda kugombea Iringa wajumbe wakaniadhibu,” anasimulia huku akicheka na kuendelea:

“Nilienda kumpima Msigwa pale Iringa, lakini pamoja na wajumbe waliniadhibu nikapata kura sita sikufanya kampeni, niliingia siku mbili kabla ya uchaguzi, ningekaa pale miezi mitatu ningepata nyingi zaidi,” anasema. Kuhusu wanasiasa kuwashambulia viongozi waliopo madarakani anasema: “Mwanasiasa aliyekomaa anapaswa kujibu kwa hoja, wanaofanya hivyo hawana hoja”.

Mwigizaji huyo anaunga mkono dhana ya kuwasifia viongozi akisema kuwa wanafanya hivyo kwa mambo ya msingi na siyo dhambi. “Mfano Rais Samia ana haki ya kusifiwa kwa yale anayoyafanya.”


MAMA ONGEA NA MWANAO

Steve Nyerere, mwanzilishi na mratibu wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao anasema taasisi hiyo iliyozinduliwa miaka minane iliyopita na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete iliunganisha wasanii mbalimbali, ikiwa na lengo la kuungana na Rais Samia mara tu alipotambulishwa kuwa mgombea mwenza wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Tukaungana na Mama Samia kuzunguka nchi nzima, tulihakikisha kabla hajapita sehemu sisi tumeshaingia, tunazunguka mtaani mimi nilikuwa mratibu wa hiyo kitu, nadhani katika taasisi bora ambayo ilifanya kampeni katika kipindi kile ni hii,” anasema.

Steve Nyerere anasema lengo lao ilikuwa kuhakikisha Mama Samia na mgombea wa kiti cha urais wakati huo, Hayati John Magufuli wanapata kura za kutosha.

“Baada ya uchaguzi kupita, tulisema kama taasisi tunabaki kwenye siasa kwa asilimia 60 na asilimia 40 tutazielekeza kwa jamii, wakati ule tayari kulikuwa na mambo mengi, lakini sisi tulisimama kama taasisi.

“Ilipokuja kampeni ya awamu nyingine 2020 bado tulisimama na mama, tulirudi kwa yuleyule chaguo letu tukaanza safari mkoa wa Dar es Salaam, lakini kutokana na vitu vingine ambavyo unamwachia Mungu hatukuweza kuzunguka kote,” anafafanua.

Steve anasema taasisi ilianza kupata misukosuko mingi na changamoto kubwa ilikuwa ni watu wa nje kuanza kuwachomoa waliopo ndani. “Taasisi ilivutwa shati, kulikuwa na watu hawaitaki kwa kifupi. Ukienda kuwaambia wakubwa jamani tunataka tuendeleze ule mwendelezo wetu na mama unaambiwa huko hakufai, na wanaokwambia hivyo ni wakubwa wana nguvu, naona siwezi kubishana nao. “Kuna muda nilipita wakati mgumu, unateswa, unazongwa unaomba fedha sehemu wanapiga simu isitolewe. Walitaka taasisi ife na waliniambia itakufa, ila niliamini hakuna dhahabu bila moto…

“Taasisi ilipitia hekaheka nyingi, lakini nilikuwa ninapigwa mimi. Baada ya hapo Mungu akaamua ugomvi, tunaendelea na tulichokifanya, sasa tumefungua milango siyo taasisi ya Bongo Muvi pekee, tunatoa huduma kwa wenye uhitaji, wakiwemo wanafunzi wasio na viatu,” anasema Steve.

Anaitaja kampeni hiyo ‘Mama Nivishe Viatu’ kuwa, “Imemgusa kila Mtanzania, kwenye mahitaji ni vijijini, ukienda unaona watoto mpaka miguu imeachana, imekatika ‘magaga’, Tabora na vijiji vyake na tumeenda Kibiti, keshokutwa tunakwenda Lindi, Mtwara, Ruvuma na tutaweka kambi Mwanza kwa kuwa kuna vijiji vingi,” anasema.

Akieleza namna wanavyofanya kampeni hiyo, Steve anasema wanatembelea shule zenye uhitaji na kugawa viatu kwa watoto. “Inagongwa kengele tunaangalia watoto wasio na viatu tunawavisha. Kuna mabinti mpaka blauzi zimechanika matiti yapo nje, Asas alitupatia hijabu 200, hawa tunawavisha ili kuwasitiri, Rais Samia pia ametoa msaada kwa watoto hawa wenye uhitaji.

Anasema anapokea simu nyingi za wakuu wa shule za msingi wakitaka awatembelee ili kutoa msaada wa viatu na ameshapokea msaada wa viatu 200 kutoka Suma JKT na 200 vingine kutoka timu ya Yanga.