Ndani ya boksi: Konde Boy, Wema na Zari wananata na biti ya usafini

Muktasari:

  • Harmonize, kwa wakati huu anabaki kuwa mmoja wa wanamuziki bora. Ni bora kwa utunzi wa mashairi. Ni bora kwa melodi na ni bora zaidi kwenye kugeuza matukio kuwa nyimbo.

Harmonize, kwa wakati huu anabaki kuwa mmoja wa wanamuziki bora. Ni bora kwa utunzi wa mashairi. Ni bora kwa melodi na ni bora zaidi kwenye kugeuza matukio kuwa nyimbo.

Ni vigumu kutemana na Mondi kisha ukaendelea kukimbiza kisanii. Ni kama jasiri muongoza njia. Wengi waliopishana naye kwenye mitikasi ya muziki waliyumba ama kutoweka jumla.

Sasa kuna Mondi kama Mondi na zile mtu tatu nyuma ya Mondi. Said Fela, Babu Tale na Salaam. Hao wote wana utawala wao kwenye hili ‘gemu’ la muziki huu. Wana mizizi mirefu kwa sasa kiasi kwamba ukiwavimbia ujue una kesi kubwa. Wakati zamani ‘gemu’ lilizunguka eneo dogo tu. Kariakoo kwa Wahindi na vipindi vya burudani kwenye redio chache zilizokuwepo. Leo hii muziki umeenda mbali zaidi na kwa sasa ukikosa ‘koneksheni’ umeisha.

Unaweza kufanyiwa umafia kwenye ‘vyuzi’ za ‘yutyubu’. Dili za ‘kolabo’ na wasanii wakubwa na hata kwenye mishe na taasisi kubwa za binafsi na Serikali. Ukizingua watu wanazingua mara tatu.

Harmonize ‘alibato’ na watu wenye pesa na ‘koneksheni’ kubwa ndani na nje ya nchi. Lakini anaendelea kuleta ubishi akikimbiza mtaa namna anavyotaka. Uliza Rich Mavoko alipo kabla ya kumchukulia poa Konde.

Konde yupo daraja la juu ukiondoa Mondi na King Kiba. Na kuna ‘gepu’ kubwa sana kati yake na watu walio chini yake. Hayupo pale kwa bahati mbaya, ni mapambano na kuelewa njia za matobo.

Hata enzi zile waliopotea kisanii kwa kuzinguana na jasiri muongoza njia. Ni wale ambao walishikwa mkono na yeye kutoka hatua ya mwanzo. Lakini wale aliokutana nao wakiwa tayari wametoka waliendelea na mishe zao kiroho safi.

Lakini Konde huyu wa sasa ‘anabato’ na waliomshika mkono toka awali. Wanaomjua kindakindaki na wenye kuelewa nguvu na udhaifu wake. Hii ni vita ambayo kama hujajipanga ile ‘kivyede’ lazima utoweke.

Konde alikuwa mtoto pendwa pale Usafini. Alifanya kila kitu kama bosi. Kuanzia staili ya muziki mpaka pozi kwenye video na maisha ya kawaida. Alipita njia za bosi wake Mondi kwa kila kitu na wala hakujali maneno ya waja.

Hata kujitwisha totozi kama Wolper ilikuwa staili ya njia za Mondi. Yale siyo mapenzi tu, bali ilikuwa sehemu ya kujikamatia kijiji chako kwenye sanaa. Na alifanikiwa sana kwenye hili ndio maana yupo pale.

Wapo waliomponda kwa tabia yake ya kumuiga Mondi. Kwamba kivuli cha Mondi kitamfanya awe chini kila siku. Wakataka ajitafute mwenyewe ili awe yeye na kuondoka kwenye ule ‘u-kama’ Diamond.

Lakini hili halikumbadilisha kabisa na akaendelea kuishi kwa kivuli cha Umondi. Mashabiki wake, mashabiki wa Wolper na WCB. Wote wakawa kijiji chake na kubeba ukubwa baada ya Mondi.

Alipotangaza kutemana na WCB. Wengi hawakuamini kama ni kweli. Walijua ni ‘kiki’ au anatafutwa mtu wa kumshindanisha kina Kiba badala ya bosi wake Mondi. Anatemana na Mondi? Haiwezekani. Ndio akili za wengi zilihisi.

Walipoona ni mtiti wa kweli stori zile zikabadilika. Wale wale walioamini ni ‘kiki’, ndio wale wale walioanza kudai kuwa Konde Boy atapotea kisanii. Hakuna aliyeamini katika Konde Boy nje ya WCB, wengi wakiamini ndio mwisho wa msela.

Mpaka sasa Konde ‘kapruvu’ wengi kuwa ameweza nje ya WCB. Lakini pamoja na hayo sumu ya Usafini bado inamtafuna. Naye ni sehemu ya watu ambao hawawezi kutema sumu ya Madale.

Ana muziki, sauti na melodi tamu. Lakini kila kitu anakisafirisha kupitia ‘kiki’ za madem. Kiki za pisi kali. Kiki za matukio ya mapenzi. Hana kipya nje ya WCB, anaishi Kimadale katika ulimwengu wake.

Ukizama kwenye ukurasa wa Konde pale Instagram. Kinachokosekana ni jina WCB tu. Lakini mengine yote ni yale yale ya Usafini. Kuna sumu ya Madale inaenezwa na Konde bila kujua au kwa kujua.

Ukiachana na Konde, kuna kiumbe upande wa jinsi ya pili. Ambacho nacho kinaeneza sumu ya Madale kwa namna moja au nyingine. Zari licha ya kuisusa Madale, lakini bado ana mizuka ya huko.

Wengi waliamini aliingia chaka la simba kwa Mondi. Siyo tu kwa hulka, hata kwa umri walipishana kinoma. Kilichopo kwenye ubongo wa Mondi, kilipita kwa Zari miaka mingi nyuma.

Kama ni ‘uveta’ wa faragha. Zari bila shaka alimalizia na neno “Asante”. Lakini Mondi aliinuka kama katoka kunawa uso tu. Wapo walioamini hata watoto wale ni uzembe wa Dai na ligi za ‘drai chama kituo’.

Lakini taratibu watu wakapata picha kuwa ukiachana na umri na utaifa, pia makuzi yalikuwa tofauti. Mondi ni mtoto wa kitaa, msela mwenye njaa ya maisha. Zari yeye alidata tu na lile ‘taito’ la mwamba.

Kumiliki kiumbe kama Zari ilikuwa kama zali kwake. Muda ulipoenda akazoea na kuanza kurudi kwenye asili yake tena. Ni baada ya kuona alichotaka alishapata kwa wema na wenzake. Akaanza kupiga matukio.

Na ‘laifu’ la kiki za warembo kwake likaendelea. Hiki kitu ni kama ndoa ya Kikristu kwa Mondi. Hatoweza kuachana na kiki kwa pisi zake. Hebu fuatilia mapito yake kwa sasa. Hii ni Zuchu time!

Toka Sepenga na Mobetto hadi Zari. Raia wakaanza kumuonea huruma Zari. Kwa kuzama chaka la simba toka mbuga ya Tandale. Wakiamini hakustahili kutendewa kwa namna ile na Mondi Bin Laden.

Kosa la Zari halikuwa kumzalia Dai. Bali kutuama eneo lililomfaa Gigy na wenzake. Hizo ndio pisi zilizostahili kumiliki vurugu na heka heka za yule msela kichwa ngumu kama Mondi. Ndio ukweli huo.

Uhusiano wa Zari na Mondi, uliibua kiumbe mwingine ndani ya mwili wa Zari. Hakuwa Zari yule wa wakati ule. Akageuka mtu wa ‘drama’, ‘makiki’ na kuendeleza mititi mitandaoni. Akawa yeyote na kusutana kama dawa.

Kilichotokea ni kama Mondi, alieneza sumu ya ‘laifu staili’ kwa Zari. Mtoto wa Kiganda ukitazama pigo zake za sasa. Humtofautishi na kina Amber Lulu. Anaishi Pretoria na swaga za Madale. Uswazi husema kimeumana.

Wakati zamani akingetetemesha kwa ‘shoo ofu’ za ndinga, mijengo na bata refu. Hivi sasa anapita kule kule kwa Mondi Bin Laden. Kiki za pisi kali, na yeye anajikikisha na ‘viserengeti boi’ vyake.

Umeona ya huko insta? Kifupi Zari kashindwa kuachana na maisha ya kumiliki vitoto. Anazeeka mwili, akili imebaki utotoni. Muda mwingi yupo ‘bize’ kujipigisha picha na kivulana umri wa mtoto wake. Anachetuka kana kwamba anajibu pigo za Mondi na Zuchu. Ni kama gari limewaka ghafla, ana heka heka kama kapandwa na siafu. Umri na kile afanyacho ni maji na mafuta.

Sijui ni Mondi aliyefanya ahusudu kuishi na vitoto au ndio ‘fantas’ yake.

Kama taifa wifi tunaye. Tena wifi wa mwendokasi. Ana heka heka sana na afanyayo siyo mageni kwetu. Yale ni Mondilisim.

Wametutangazia kutemana na sasa wanaishi kirafiki wakilea watoto wao. Lakini zile swaga na tabia alizobeba Madale, hajatemana nazo Zari. Bado anaishi kwenye kivuli cha Usafini kwa asilimia kubwa.

Hii sumu ambayo pia ilimea kwenye akili za Wema. Kabla ya kumilikiana na Mondi, wakati wa ustaa wake hakujua mambo ya kiki. Siku zote aliandikwa kwa matukio na siyo kwa kiki. Wema aliandikwa kwa kila kitu leo anaandikiwa kwa kitu.

Ni sumu ya Madale inaendelea kumtafuna mpaka leo. Wema yuko bize na kiki za Whozu. Yamekuwa maisha yake rasmi kwamba kila msanii anaweza kumtumia Wema kwa kiki za sanaa. Licha ya kufifia ila bado yupo.

Hii leo Konde Boy ana albamu yake. Mashabiki ndio wanamshindanisha na Mbosso. Lakini yeye yupo bize na kiki zake na Kajala. Hii ni sumu ya tangu Usafini, alipomtumia Wolper kwenye mishe zake.

Kuna albamu ya Konde Boy na kuna maisha ya Konde na Kajala. Wakati mashabiki wanamshindanisha na Mbosso. Ukweli ni kwamba albamu ya Konde Boy inashindana na nguvu ya penzi la Kajala.