Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi za mashetani ya kale Zanzibar zimefunikwa na siasa

Muktasari:

  • Leo napenda kuzungumzia mambo yaliyotawala mazungumzo ya watu wa Zanzibar hapo kitambo, lakini siyasikii sana kutajwa na vijana wengi wa sasa. Hawana habari nayo na yamebaki sehemu ya historia ya Zanzibar.
  • Haya ni masuala ya wanga, majini, mashetani na mazimwi ambayo hapo zamani yalitawala simulizi katika baraza na vijiwe vya visiwani. Siku hizo vijiwe vimetawaliwa na habari za siasa na michezo.

Simulizi binafsi

Kwanza nianze na niliyokutana nayo usiku mmoja majira ya kama saa nne usiku hivi katika mwaka 1955 au 1956.

Siku hiyo nilikawia kuondoka klabu yangu ya Wolervhampton Wanderers (siku hizi Ujamaa Sports Club) hapo Rahaleo mbele ya mlango wa kituo cha radio cha Shirika la Utangazaji Zanzibar, siku zile ikiitwa Sauti ya Unguja.

Niliondoka klabu na baiskeli yangu ya Rudge kueleka Gongoni alipokuwa anaishi bibi yangu mzaa mama. Siku ile niliwaambia wazazi nisingerudi nyumbani Kisimamajongoo na ningelala kwa bibi.

Muda mfupi tu baada ya kuondoka klabu, nilipita chini ya Mkunazi katikati ya makaburi yaliyokuwapo eneo hilo ambalo siku hizi imejengwa barabara ya kuelekea Kariakoo kutoka Michenzani.

Niliyoyaona chini ya Mkunazi sitayasahau mpaka siku na mimi nitakapomaliza mkataba wangu wa kuishi duniani na kupumzishwa kaburini kama viumbe vilivyokuwa chini ya ardhi sehemu hio.

Amini usiamini niliyoyaona si madogo na kwa waliokuwa wanayajua sio makubwa. Nilikuta kundi la viumbe (watu) wasiopungua 10 wakiwa katika hali kama ile waliokuja nayo duniani walipozaliwa (bila ya nguo).

Watu hao walikuwa wanacheza ngoma niliyokuwa siifahamu. Nilishtuka, lakini nilijikaza na kupata ujabari ambao sikujua ulitokea wapi wa kuwapigia kengele ya baiskeli yangu wanipishe.

Walikaa pembeni na mara baada ya kupita nikajikuta ninafukuzwa na mbwa na kulazimika kuongeza kasi ya baiskeli niliyokuwa nimepanda. Kilichonishangaza baadaye ni kwamba katika safari yangu ya kukimbilia nyumbani, watu wachache niliokutana nao njiani ilionekana kama hawakuona kilichonikuta, yaani kufukuzwa na mbwa.

Nilipofika nyumbani nilimkuta bibi yangu, Mwanaidi Mohamed Musa ambaye kwa kiasi chake alikuwa mwanazuoni, amekaa barazani na tasbihi yake.

Nilipofika tu na kuhema nilimuona akipiga kelele za ‘Nyoo.….walaaanifu… mahasidi wakubwa’.

Wale mbwa waligeuza njia na usiku ule nilipata homa kali na kufukizwa ubani huku nikisomewa hadi nilipopata usingizi.

Hili lilikuwa tukio lililonifanya kuamini tokea wakati ule kuwepo katika dunia yetu hii viumbe tafauti na sisi wanaoitwa wanga, mashetani, majini na kadhalika.

Siku zile ilikuwa kawaida kusikia wanga walijigeuza mapakacha au mbwa, hasa katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini Unguja na kisiwani Pemba kufukuza watu na kufanya kila aina ya uasherati.

Nilipowaeleza wenzangu yaliyonikuta usiku ule baadhi ya wazee wa klabu waliniambia watu hawapiti chini ya ule Mkunazi ambao upo mpaka hii leo baada ya saa tatu usiku. Miti mingi iliyokuwepo pale imekatwa isipokuwa huo mkunazi.

Wale wazee walisema watu walikuwa hawakaribii sehemu ile yenye Mkunazi nyakati za usiku kwa sababu waliomiliki wa eneo lile walikuwa na mambo yao.

Kwa kweli zama zile yalikuwepo maeneo mengi ambayo watu wa mjini Unguja walihofia kupita baada ya saa tatu usiku, tafauti na hali ilivyo siku hizi.

Kwa mfano katika eneo la Welesi ambao zipo ofisi za magazeti ya Daily News na Nipashe watu wengi waliogopa kupita usiku.

Hii ilitokana na habari za kuwepo mwanamke (watu waliamini kuwa ni shetani) aliyekuwa na umbo la kuvutia na mguu wa wachuma.

Hakuna kijana shabab ambaye alikutana naye alishindwa kuvutiwa na hicho ‘kimwana’.

Kwa mujibu wa simulizi, huyo mwana mama ukishakutana naye hukuganda kama ruba na hakubali uwe na mwanamke mwingine au ufunge ndoa.

Siku hizi hupati simulizi kama hizi isipokuwa yale yaliyosemekana kuwepo zamani hugusiwa mara mojamoja na watu wenye umri mkubwa vijana husema wanasitawisha baraza,

Katika kisiwa cha Pemba mambo kama haya ambayo ukielezewa habari zake utabaki kujiuliza masuala mengi na hupati jawabu. Ndio maana labda wahenga wakaja na msemo wa Pemba peremba…. ukienda na joho utarudi na kilemba.

Huko zilikuwepo sehemu zilizoitwa giningi ambazo inasemekana wanga walizitumia usiku wa kiza kufanya mambo ambayo ukihadithiwa utapigwa na butaa.

Hio ndio Zenj ya zamani, tafauti na siku hizi ambapo mada kubwa za mazungumzo ni siasa, kandanda, muziki, biashara na mambo mengine.

Kwa mujibu wa kumbukumbu, mambo haya yalikuwepo katika eneo moja maarufu la kijiji cha Dunga, Kusini Unguja, ambapo mpaka leo hutokea ajali nyingi za ajabuajabu.

Hapo inasemekana alikuwepo mwanamke mzuri wa Kiarabu ambaye watu walikutana naye usiku akiwa amejifunika uso na kumtaka anayekutana naye kufanya naye mapenzi.

Ukimkatalia ghafla hutoweka na kukuacha katika hali ya kutojitambua na mara nyingine ukapatwa na usingizi na ukiamka asubuhi hujui kilichotokea, lakini unagundua ulifanya tendo la kimapenzi.

Miongoni mwa watu maarufu walioielezea hali hii kwa urefu na taarifa zao kuwepo Jumba la Kumbukumbu la Zanzibar ni daktari wa Kiingereza aliyeitwa Spurrier ambaye aliishi katika kasri ya mfalme ya Dunga mwishoni mwa karne ya 19.

Spurrrier ameeleza kuwa mwezi Desemba 1895, alimuona binti huyo wa Kiarabu akitembea kwa madaha usiku wa manane katika kasri hiyo ya mfalme.

Mwana mama huyu alikuwa amejiremba na kunukia manukato yaliyovutia na alitembea kwa madaha na mbwa mdogo mweusi.

Kasri ya Dunga ilijengwa na mwinyi mmoja maarufu katika historia ya Zanzibar, Mohammed bin Ahmed el Alawi.

Huyu ni kitukuu cha mwinyi maarufu mwenye asili ya Persia, Iran, Hasan bin Abubakar.

Huyu bwana anazungumzwa sana katika simulizi za historia ya Kilwa, Tanzania Bara. Mrithi wake alikuwa Malkia Fatma, mwana mama wa miraba minne mwenye uzuri wa aina yake ambaye alikuja kuolewa na Mwarabu aliyetoka Hadhramout, Yemen, aitwaye Alawi.

Malkia Fatma pia alikuwa na nyumba mjini Unguja, karibu na jengo la Beit el Ajaib, karibu na Ngome Kongwe.

Mwanawe, Hasan alikuwa mtawala wa Zanzibar mpaka 1828 . Hapo ndipo Hassan alipokwenda kuhamia katika kijiji cha Bweni, karibu na Dunga na kuruhusiwa kuwa mtawala kwa masharti ya kumpa nusu ya kodi aliyotoza mfalme Seyyid Said.

Mohammed alimrithi kaka yake Hassan mwaka 1845 na kuamua kujenga hilo kasri ya Dunga kwa miaka 10 na kuishi hapo mpaka alipoiaga dunia mwaka 1865.

Mwanawe wa kiume, Ahmed, ambaye alipokuwa na miaka 15 alirithishwa utawala. Aliamua kuhamia Mji Mkongwe, Unguja mjini, ambapo aliishi kwa muda mfupi na kuiaga dunia.

Kasri ya Dunga ambayo siku hizi ni kivutio cha watalii ikawa haikaliwi na mtu na kuanza kuporomoka hadi miaka ya karibuni ilipofanyiwa matengenezo. Hivi karibuni Serikali ilitangaza mpango wa kulifanyia matengenezo makubwa eneo hili la kihistoria.

Katika sehemu hio, zipo simulizi nyingi za kwamba watumwa wengi walifukiwa hapo wakiwa hai kutokana na kutotii amri za mtawala wa Dunga wa wakati huo, Mwinyi Mkuu.

Katika mwaka kisima kimoja kilichokuwepo hapo kiliposafishwa yalipatikana mabaki ya mifupa na vichwa vya binaadamu.

Huyu mtawala wa jadi Mwinyimkuu na Washirazi, watu wa eneo la Shiraz lililopo Persia, Iran, walihamia Zanzibar na sehemu nyengine za mwambao wa Afrika ya Mashariki mwishoni mwa karne ya 15.

Safari ya kwanza ya inasemekana iliongozwa na bwana mmoja aitwaye Hassan Bin Ali, “nguo nyingi” aliyeondoka Shiraz na majahazi saba yaliyochukuliwa na upepo na kufika sehemu mbalimbali za pwani ya Afrika ya Mashariki. Jahazi moja liliwasili Zanzibar.

Mwingereza mmoja, Yoland Brown, amewahi kuhadithia kuwa baba yake aliyefanya kazi katika Bandari ya Unguja amedai alipokuwa kijana mdogo na kuishi Mambo Msige, karibu na Hoteli ya Serena (zamani pakiitwa Kelele Square), alimwambia mama yake mara mbili alikutana na shetani ndani ya nyumba yao.

Eneo jingine liliosifika kuwa na mashetani la majengo ya kale ya Mbweni, nje kidogo ya mji wa Unguja, ambapo siku hizi pamefunguliwa hoteli ya kitalii.

Mwanamke mmoja wa Kiingereza, Caroline Thackeray, ambaye alikuwa mjane na kuishi Zanzibar kwa miaka 49 ameeleza kwamba alizoea kukutana na mashetani sehemu hiyo. Huyu mama alifariki mwaka 1926 akiwa na miaka 83.

Mpaka leo baadhi ya watu wanaotembelea hoteli hilo hutishana na habari za mashetani kuwepo hapo.

Hii ndio Zenj ya zamani iliyokuwa inasemekana kujaa wanga na mashetani. Nadhani wakati umefika kwa simulizi zote juu ya wanga, mashetani, majini na vibwengo zikakusanywa na kuwekwa pamoja ili watu

waelewe Zanzibar ya zanani ilikuwa vipi.

Hata hivyo, hapana sababu ya mtu kuogopa kutembelea Zanzibar kwani vituko kama hivyo nilivyovielezea vimetoweka na hao wanga na mashetani kuwa sehemu ya historia ya Zanzibar.