Urais wa George Weah Liberia umeshikwa na watu watatu

Muktasari:

  • Mchezaji bora wa soka ulimwenguni mwenye tuzo ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Ballon d’Or mwaka 1995, ameongoza kwenye matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 10, mwaka huu, lakini hakuvuka asilimia 50, hivyo anarudia ngwe pili dhidi ya Makamu wa Rais, Joseph Boakai aliyetoka wa pili.

Kwa mara ya tatu mfululizo, Liberia inaandika historia ya kufanya marudio ya uchaguzi wa Rais, kutokana na matokeo ya mzunguko wa kwanza kukosa mshindi aliyevuka asilimia 50 ya kura kama Katiba ya nchi inavyotaka.

Mchezaji bora wa soka ulimwenguni mwenye tuzo ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Ballon d’Or mwaka 1995, ameongoza kwenye matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 10, mwaka huu, lakini hakuvuka asilimia 50, hivyo anarudia ngwe pili dhidi ya Makamu wa Rais, Joseph Boakai aliyetoka wa pili.

Weah wa CDC amepata kura asilimia 39.2 na Boakai wa Unity asilimia 29.6. Uchaguzi wa pili, unafanya Waliberia ndani ya miaka 12 sasa, liwe Taifa ambalo mshindi wa urais hapatikani kwa urahisi. Mwaka 2005 na 2011, Rais wa Liberia alichaguliwa baada ya kufanyika uchaguzi wa marudio.

Ikumbukwe pia Weah hii si mara yake ya kwanza kuongoza. Mwaka 2005 aliongoza kwa tofauti kubwa ya kura dhidi ya Rais wa sasa, Ellen Johnson Sirleaf. Alipata asilimia 28 na Sirleaf asilimia 19. Uchaguzi uliporudiwa, Sirleaf alivuna kura asilimia 59.4 na Weah 40.6. Sirleaf akatangazwa Rais.

Mwaka 2011, Sirleaf akitetea kiti chake kwa muhula wa pili, kwa tiketi ya chama chake cha Unity, alikabiliana vilivyo na Winston Tubman wa CDC, mgombea mwenza wake akiwa Weah. Mgombea mwenza wa Sirleaf alikuwa Boakai. Kwa mantiki hiyo, washindani wa sasa wa urais walikuwa wagombea wenza uchaguzi uliopita.

Matokeo ya awali mwaka 2011 ni kuwa Sirleaf alipata asilimia 43.9, Tubaman asilimia 32.7. Uchaguzi wa marudio ulipofanyika, Sirleaf alishinda kwa kura asilimia 90.7, wakati Tubman alipata kura asilimia 9.3. Sirleaf akawa amefanikiwa kutetea kiti chake.

Mwaka huu, imekuwa sasa mazoea kwamba Liberia hawapati mshindi wa urais katika matokeo ya awali. Tangu kuvunjwa kwa utawala wa Waliberia waliotokea Marekani, Rais wa zamani wa nchi kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu 1997. Taylor alishinda kwa kura zaidi ya asilimia 75.

Taylor aliweza kuwateka vijana wa Liberia, wakawa hawaambiwi kitu. Hata wazee walipoonya kuwa mtu huyo ni hatari kwa sababu alisababisha mauaji ya watu wengi katika Vita ya Kwanza ya Kiraia nchi humo, vijana waliibuka na kauli mbiu; Killed My Ma, He Killed My Pa, but I Will Vote for Him (Alimuua mama, alimuua baba lakini nitampigia kura).

Taylor alijiuzulu urais mwaka 2003 kwa shinikizo la kimataifa, ikiwa ni baada ya kumalizika kwa Vita ya Pili ya Kiraia Liberia. Hivi sasa Taylor anatumikia kifungo cha maisha jela nchini Uingereza baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ugumu ni nini Liberia?

Uongozi wa kura ambao Weah ameupata katika Uchaguzi wa Oktoba 10 si wa kushangaza hata kidogo. Mwaka 2005, Weah alikuwa mtu pendwa zaidi na iliaminika angeshinda kwa urahisi lakini matokeo ya mwisho yalimshangaza.

Mwaka 2005, Weah hakujitokeza yeye mwenyewe kugombea, la! Ilizugushwa hati ya kusaini maombi (petition) yenye kumtaka Weah akubali kugombea urais. Watu wengi walisaini na kwa ombi hilo la saini za Waliberia wenzake, Weah alikubali.

Hata hivyo, baada ya kujitosa ulingoni alipata kura asilimia 28 na katika marudio akapata asilimia 40.6 na kumwacha Sirleaf akiandika rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza Afrika kutawazwa kuwa Rais wa nchi yake.

Kwa nini watu walimuomba Weah kwa wingi agombee urais mwaka 2005 kisha wakamgeuka? Jawabu la swali hilo lipo kwenye neno moja tu; ukabila. Ndiyo, siasa za Liberia zimetawaliwa na ukabila uliopitiliza.

Katika kutawala siasa za ukabila Liberia, hakuna kabila hata moja linalofikia wingi wa watu japo asilimia 25 ya nchi. Kabila kubwa zaidi ni Kpelle ambalo watu wake wanakadiriwa kuwa asilimia 20.3, mengine yote idadi yake ya watu ni chini ya asilimia 14.

Hali hiyo inasababisha mpaka watu wasio na nguvu kabisa kisiasa, wawe na uamuzi kwenye matokeo ya mwisho ya urais. Kwamba uchaguzi wa awali anayeongoza hapati asilimia 50 na katika marudio mshindi ni yule ambaye anafanikiwa kushawishi wagombea wadogo kumuunga mkono.

Hiyo ni sababu ya Sirleaf aliyepata kura asilimia 19 mwaka 2005 katika matokeo ya awali, kuibuka mshindi katika uchaguzi wa marudio, maana aliungwa mkono na wagombea wengi wadogo. Kwa uchaguzi wa tatu sasa, wagombea wadogo Liberia ndiyo wamekuwa wakiamua mshindi wa kiti cha urais.

Mwaka huu na kile ambacho kitaamuliwa Novemba 7, katika uchaguzi wa marudio, hakina tofauti na yaliyojiri mwaka 2005 Weah alipoangukia pua au mwaka 2011 Sirleaf alipompoteza Tubman kwenye kura za mzunguko wa pili.

Waliberia wamekuwa wakihuburiwa ukabila, hivyo hupiga kura kutokana na matarajio ya nafasi za makabila yao serikalini. Nadharia ya utambulisho wa kisiasa kwenye makundi ya kijamii (identity politics), kwa Liberia imeingia moja kwa moja katika ukabila.

Pamoja na sera, misingi ya ujenzi wa nchi, ubora na kuaminika kwa mgombea, kwa Liberia watu hungoja mgombea ajipambanue kikabila ili watu wa makabila wajue wamchague kwa sababu wana maslahi naye au wampigie kura mwingine.

Imekuwa ikitokea Liberia kwa watu kujitokeza kugombea kwa sababu ya kuamini wataungwa mkono na makabila yao. Na kweli watu hupiga kura kwa kutazama makabila ya wagombea. Wengine ambao makabila yao hukosa wagombea huangalia aliye na afadhali kwao.

Ukabila ulivyoota mizizi

Mapema mwaka huu, Boakai alinukuliwa na gazeti maarufu Liberia, Front-Page Africa, akilalamika kuwa Rais Sirleaf ambaye ni wa chama chake, hamuungi mkono katika mbio zake za urais, badala yake anampigia chapuo Charles Brumskine wa chama cha Liberty.

Madai ya Boakai ni kuwa Rais Sirleaf yupo tayari chama chao (Unity) ambacho ndiyo chama tawala, kipoteze uongozi wa nchi kwa sababu ya kabila. Boakai ni kabila la Kissi, Sirleaf ni Kru, ingawa mama yake ni chotara wa Liberia na Ujerumani. Brumskine ni Mkongo (jamii ya wakuja) lakini mwenyewe anajitambulisha kuwa kabila la Bassa.

Mapema kabisa Brumskine alianzisha kampeni kuwa ni zamu ya Bassa kuongoza Liberia kwa sababu tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 1847 wakati wa utawala wa Waliberia waliotoka Marekani (Americo-Liberians) na wazawa asilia, nchi hiyo haijawahi kutawaliwa na Bassa.

Bassa ni kabila la pili kwa kuwa na watu wengi Liberia, likiwa na watu wansokadiwa kuwa asilimia 13.4 nyuma ya Kpelle lenye asilimia 20.3. Utambulisho huo wa Bassa umemuwezesha Brumskine kupata kura asilimia 9.7, hivyo kushika nafasi ya tatu.

Julai mwaka huu, mgombea mwenza wa Weah, Jewel Taylor ambaye ni mtalaka wa Charles Taylor, alifanya mahojiano na Front-Page Africa na kueleza kuwa anaamini sababu kubwa ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza ni kabila lake la Kpelle ambalo lina watu wengi, hivyo itakuwa rahisi kwa Weah kupata kura nyingi za wana-Kpelle.

Hiyo ndiyo Liberia ambayo siasa zake zinazungumzwa kikabila na watu hawaonyani kuhusu hatari yake. Nchi ina historia ya machafuko ya kikabila lakini watu hawajajifunza, ahadi za kikabila zinatolewa mithili ya ujenzi wa miundombinu au ustawishaji wa hali za kimaisha.

Kwa nini ukabila Liberia?

Wakati mataifa makubwa Ulaya yalipoketi kuligawa Bara la Afrika mwaka 1884-1885, tayari Liberia ilikuwa imeshajitangaza kuwa nchi huru na jamhuri, miaka 38 kabla na kuthibitishwa na Uingereza. Hivyo, Liberia kama ilivyo kwa Ethiopia ni nchi za Afrika ambazo hazikugeuzwa makoloni ya Wazungu.

Mwaka 1816, aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Georgia, Marekani, Robert Finley aliibua wazo la kutengeneza jamii ya koloni la Marekani barani Afrika (American Colonization Society ‘ACS’). Finley alifariki dunia mwaka 1817 kabla ya mpango huo kuanza lakini uliendelezwa.

Mwaka 1821-1822 (Karne ya 19), Wamarekani Weusi waliokuwa watumwa Marekani, waliachiwa huru na kuelekezwa Pwani ya Afrika Magharibi ili kuunda jamii ya koloni la Marekani (ACS). Hata hivyo, kituo chao kikuu kikawa Liberia.

Hata hivyo, Liberia tayari ilikuwa na wakazi wake walioishi katika jamii za makabila ambayo yalihamia kuanzia Karne ya 13-16 kutokea Sudan (Songhai Empire), Mali na maeneo mengine ya Afrika. Jamii ya waliozungumza Kimende pamoja na makabila ya Dei, Kru, Bassa, Gola, Grebi, Gio na Kissi ni watu wa mwanzoni kuishi Liberia.

Waliberia waliotokea Marekani utumwani walipofika Liberia, nao wakajiona wana hadhi kubwa, wakawatawala wenyeji, wakawanyang’anya ardhi, wakawageuza watumwa kwenye mashamba na shughuli nyingine za uzalishaji mali. Wao walizungumza Kiingereza, hivyo hawakutaka kujifananisha na wenyeji waliowasiliana kwa lugha za makabila yao.

Awali, Waliberia waliotokea Marekani (Americo-Liberians), waliwatawala Waliberia wenyeji kwa msaada wa Marekani, lakini baada ya kufanikiwa kuthibitisha utawala wao, Americo-Liberians waliitangaza Liberia kuwa nchi huru mwaka 1847 na Uingereza ikathibitisha lakini Marekani waligoma.

Tangu wakati huo, Waliberia waliolowea kutoka Marekani wakawa wanatambulika kuwa tabaka la juu kwenye nchi na wenyeji wakikandamizwa. Waliberia wenyeji walinyimwa hata haki ya kupiga kura kuchagua viongozi wao mpaka mwaka 1946 chini ya uongozi wa Rais William Tubman, ndipo Waliberia wenyeji walipewa haki ya kupiga kura kikatiba.

Kulikuwa na sheria ya kukataza Waliberia wenyeji kufika mijini, Rais Tubman aliifuta sheria hiyo, hivyo kuwezesha wenyeji kuwa huru kutoka vijijini na kutembelea na kuishi mijini ambako awali, waliishi Americo-Liberians peke yao.

Hata hivyo ni Tubman huyohuyo aliyeasisi siasa za ukabila baada ya uchaguzi wa Urais mwaka 1951 kukabiliwa na mgombea wa kwanza mwenyeji, Didwho Welleh Twe wa kabila la Kru, aliyekuwa msomi aliyekubalika kwa jamii kubwa ya wenyeji wa Liberia ambao walikuwa wamechoshwa na ubaguzi wa Waliberia waliotokea Marekani.

Tubman alipoona ugumu wa kumshinda Twe kwa kura, alimpachika sifa ya ubaguzi, kwamba ni mkabila. Katika kumgawa Twe na jamii ya Kru, alisema Twe ni Settra Kru, yaani kundi la watu wachache mno kwenye kabila la Kru. Matokeo yake Twe alipingwa na Kru wenzake. Mwisho Twe alikimbia nchi alipoona maisha yake yapo hatarini.

Ni wakati huo makundi mawili yakawa na thamani kubwa kijamii na serikalini. Waliberia waliotokea Marekani na Waliberia wenye asili ya Congo. Wapo wenyeji waliacha kufundisha watoto wao lugha zao za asili na kulazimisha kujifanya Wakongo au Americo-Liberians.

Mwaka 1980, Samuel Doe wa kabila la Krahn alipompindua Rais William Tolbert ndiyo ilikuwa mwisho wa utawala wa Waliberia waliotokea Marekani.

Doe alijitahidi kujenga miundombinu kuliko watangulizi wake wote, alikuza uchumi na kujitenga na siasa za ukabila.

Watu wachache mno kutoka kabila la Krahn ndiyo walipata nafasi serikalini, lakini wengi zaidi walitoka makabila mengine, hata baadhi ya Waliberia waliotokea Marekani. Hata hivyo, Doe alishutumiwa kuua watu na kukiuka misingi ya haki za binadamu, vilevile rushwa ilishamiri katika utawala wake.

Waliompinga Doe walimshutumu kwa ukabila, kwamba Serikali yake ilijaza watu wa Krahn. Shutuma hizo zimeendelea kila utawala. Kutoka kwa Amos Sawyer, Taylor mpaka Sirleaf. Hata hivyo, Doe anabaki kukumbukwa kwa kuumaliza utawala wa Waliberia waliotokea Marekani, maana aliua wanachama na mashabiki wengi wa chama cha Whig.

Mpaka sasa Liberia ni ya ukabila, ukitaka ushinde uungwe mkono na makabila mengi wenyeji. Zaidi ya asilimia 85 ya Waliberia ni Wakristo, ukitaka uambulie sifuri kwenye uchaguzi, jitokeze na jina linalokupambanua kuwa ni Muislam, hutachaguliwa, zaidi utaitwa wa kuja kutoka Mali, Gabon, Gambia na kwingineko.

Nani atashinda 2017?

Sasa basi, kati ya Weah na Boakai, atakayeshinda ni yule ambaye ataweza kushawishi kuungwa mkono na wagombea wengine wadogo ili apate kura za watu wa makabila yao.

Weah ni Kru na anajivunia kabila la mgombea mwenza wake, Jewel Taylor ambaye ni Kpelle. Ipo kampeni inaendeshwa pia kuwa haiwezekani Weah ashinde kwa sababu ni Kru, wakati Rais anayeondoka madarakani, Sirleaf naye ni Kru.

Kingine ni kuwa Jewel Taylor kuwa mgombea mwenza wa Weah, kinasababisha uvumi kwamba nwanasoka huyo wa zamani, atasababisha Charles Taylor aiongoze Liberia akiwa gerezani nchini Uingereza.

Kitendo cha Weah kupata kukiri kuwa alizungumza na Taylor kwa simu akiwa gerezani Uingereza, kiliongeza wasiwasi wa Taylor kuitawala Liberia kwa ‘timoti’ endapo Weah atashinda.

Pamoja na kila kinachozungumzwa, mshindi wa Urais Liberia ataamuliwa na wanasiasa watatu kati ya walioshika Tano Bora lakini hawaingii mzunguko wa pili. Wa kwanza ni Brumskine aliyepata kura asilimia 9.7, Alexander Cummings wa ANC asilimia 6.9 na Prince Johnson wa MDR asilimia 6.6.

Japo wapo wengine kama 15 lakini hao watatu ndiyo wamebeba majaliwa ya Rais anayefuata Liberia. Ama Boakai au Weah, yeyote atakayecheza vizuri na kura za wanasiasa hao watatu pamoja na makabila yao, atakuwa Rais.

Liberia ina watu 4.5 milioni lakini wapigakuta hawazidi 1.2 milioni. Hivyo, mgombea atakayevuna kura 650,000 mpaka 700,000, huyo atakuwa Rais bila shaka. Kila la heri Liberia Novemba 7, 2017.

Mwaka 2005 kampeni kubwa dhidi ya Weah ilikuwa uzoefu, kwamba alitoka kustaafu soka moja kwa moja na kugombea Urais. Hivi sasa Weah ni mwanasiasa kwa miaka 13. Mwaka 2014 alichaguliwa kuwa seneta wa jimbo la Montserrado. Hivyo, uzoefu si tatizo tena.