Viongozi waliopotea kipindi cha Magufuli wanavyong’ara kwa Samia

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (kulia) akimshukuru Rais John Magufuli baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao Ikulu Septemba 10, 2019 alipokwenda kumuomba msamaha kutokana na kuhusika katika mazungumzo yasiyofaa dhidi ya Rais Magufuli. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Katika utawala uliopita walipotea kisiasa, lakini sasa wanaonekana majembe

Lula da Silva ameshinda urais wa Brazil kwa muhula wa tatu. Ni safari ngumu ya kisiasa. Mapambano yaliyomlazimu kuucheza mpira mgumu. Hatimaye Lula ni mshindi tena.

Kama alivyoishinda shere, akachomoza kutoka familia hohehahe, baba na mama wote kapuku, mpaka kukwea ngazi za kisiasa na kuifikia ofisi namba moja Brazil, akaliongoza Taifa hilo mwanachama wa G8, ndivyo ameweza kuvuka vizingiti vya kisiasa.

Kashfa nyingi zikamwandama, tuhuma za rushwa zikafululiza juu yake. Alipotoka madarakani mwaka 2010 baada ya kuongoza vipindi viwili vya urais, akakutana na misukosuko mingi. Akakutwa na hatia ya rushwa. Akafungwa jela.

Ni siasa za kusaka mchawi (political witch-hunt), ndivyo Lula alivyojitetea. Kwamba mahasimu wake wa kisiasa walimtengenezea skendo na kumbambikia kesi za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi. Alihukumiwa kwenda jela miaka 12.

Alikaa jela siku 580. Yaani mwaka mmoja, miezi sita na ushee. Machi 2021, Mahakama ya Upeo Brazil, ilitengua hukumu ya Mahakama ya Curitiba, iliyomtia hatiani Lula na kumsweka jela miaka 12.

Baada ya kutoka jela, alianza kujipanga upya kisiasa. Ameshinda urais kwa mara ya tatu. Ametoa kauli kuwa “walitaka kumzika akiwa hai, lakini ameshinda kifo”. Wakati anakwenda jela, ilitabiriwa kuwa ingekuwa mwisho wake kisiasa. Hakuna aliyewaza ujio wa tatu wa Lula katika kiti cha Rais wa Brazil.


Tuongeze muhtasari

Kenya, si muda mrefu umepita tangu William Ruto alipochaguliwa kuwa Rais na Rigathi Gachagua akiketi kwenye kiti cha Naibu Rais. Katikati ya kampeni, Gachagua alikutwa na hatia ya vitendo vya rushwa.

Mahakama ya Juu Kenya ilitoa ruhusa Serikali kutaifisha Sh202 milioni za Kenya (Sh4 bilioni) kwenye akaunti ya Gachagua. Jaji alisema, Gachagua alipata fedha hizo kwa njia ya rushwa.

Ni political witch-hunt, ndivyo Gachagua alijitetea. Hakuondolewa kwenye mbio za kuuwania urais. Wananchi hawakugeuza shingo dhidi yake, wakampigia kura. Jitihada za kumzuia asiapishwe zikagonga mwamba. Gachagua ni Naibu Rais halali.

Mlete Lula, kisha tumweke pamoja na Gachagua. Kama walisingiziwa, lilikuwa jambo la hatari mno. Ni siasa za roho mbaya na mauaji. Kwa nini umtengenezee mwenzio kesi ili kumuua kisiasa?

Ikiwa kweli walihusika na vitendo vya rushwa, hatari ni kubwa. Wahalifu wanapotembea huru, tena wanaichezea shere hadi mifumo ya kisheria, kisha wanashinda kura za wananchi. Hao wanaweza kufanya chochote kwa sababu hudharau mifumo na wananchi wao.

Ndio sababu, mifumo ya nchi hupaswa mno kulindwa. Maana inapogeuka kuwa vitu vya kuchezea, Taifa huwa mfu. Aghalabu, nchi ikishakufa kimifumo, wananchi huchezewa na kuyumbishwa na makundi mawili; matajiri na wanasiasa. Basi!

Mifano ya Gachagua na Lula, ikulete kwenye tafakuri hii, kwamba Kenya na Brazil, kwa macho ya mkalimani wa kisiasa, ni mataifa yaliyokufa kimifumo, ingawa Katiba zao ni imara. Kama mtu anaweza kufungwa jela na kuachiwa kwa hoja kuwa alihukumiwa kimakosa, halafu akashinda urais. Huoni kuna shida ya kimfumo?

Ikiwa mtu anakutwa na hatia ya vitendo vya rushwa hadi fedha kwenye akaunti yake, Mahakama inaamuru zichukuliwe na Serikali. Halafu mtu huyo anatembea huru na kuchaguliwa kisha kuapishwa kuwa Naibu Rais. Unawezaje kuacha kutafsiri kwamba mifumo ya mataifa imekufa?


Tufanye kikao Tanzania

January Makamba na Nape Nnauye waliondolewa kwenye mfumo wa uongozi kipindi Tanzania ikiongozwa na Dk John Magufuli. Hivi sasa, Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu ni Samia Suluhu Hassan. Mambo yamebadilika.

January ni Waziri wa Nishati, Nape ndiye bosi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tehama. Yupo mtu atasema kila kiongozi huchagua timu yake ya kazi. Magufuli aliona hawamfai, Samia ameona ndio majembe yake ya kumpa matokeo.

Hata hivyo, hoja ipo kwenye jinsi walivyochukuliwa na uongozi wa Magufuli na namna wanavyochomoza chini ya Samia. Kwa Magufuli, ungewaona January na Nape kama watukutu wa kisiasa, walioshindwa kumheshimu Rais wa nchi.

Kipindi cha Samia, unawaona January na Nape ndio vinara wa wizara muhimu. Jinsi wanavyofanya kazi, unapata picha ya namna wanavyofurahia kutimiza wajibu wao chini ya Rais Samia.

Siha ya mjadala ni njema kama utamleta mezani Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana. Alivyoachia kiti cha Ukatibu Mkuu kwa kuandika barua mfululizo za kuomba kupumzika. Kipindi hicho Mwenyekiti CCM akiwa Magufuli.

Vuta picha jinsi Kinana alivyoshindwa kuchanua kisiasa tangu Magufuli alipoingia madarakani. Tena kuna wakati akawa anapotea kabisa licha ya kuwa Katibu Mkuu wa chama tawala. Ona alivyorejea CCM akiwa Makamu Mwenyekiti. Anavyochanua.

Wote watatu, Kinana, January na Nape, wanaonekana wenye furaha mno kufanya kazi chini ya Rais Samia. Kipindi cha Magufuli, wote watatu hawakuwa kwenye furaha yao ya uongozi ambayo jamii ilizoea.

Akumbukwe na mwandishi wa habari aliyejipa cheo cha mwanaharakati huru, mtetezi wa Rais Magufuli, Cyprian Musiba. Aliwashughulikia Kinana, January na Nape vilivyo. Aliwapa majina mabaya ya kila aina. Aliwaita wezi. Kuna kipindi aliwasogeza jirani kabisa na tuhuma za uhaini. Alidai walikula njama za kumwangusha Rais Magufuli.

Wakati akifanya hayo, Musiba alitembea bila hofu. Kinana na veterani mwenzake wa jeshi na kwenye siasa, Yusuf Makamba, wakatoa waraka wakieleza hisia zao kuwa Musiba alikuwa akilindwa na nguvu isiyohojiwa na chochote. Ipi hiyo? Hawakuitaja!

Kinana, Makamba, Nape na January, waliandamwa mpaka kurekodiwa sauti kupitia mazungumzo yao kwa simu. Hawakuwa na kipindi kizuri wakati wa Magufuli. Chama kimoja, lakini walitafutana. Ni siasa za kuwindana (political witch-hunt).

Ni kipindi ambacho ni vizuri kuhoji. Je, akina Kinana, Nape na January, walisingiziwa wakati wa Magufuli au Samia ndiye ameamua kusafiri na watu ambao walibainika si wasafi wakati wa mtangulizi wake?

Kama walisingiziwa, iweje mifumo yote ikae kimya? Je, kipindi cha Magufuli mifumo yote ilikufa ndio maana iliwezekana kutokea yaliyowapata akina Kinana, Nape na January?

Ikiwa Samia ndiye anawabeba kimakosa, kwa nini inawezekana? Mifumo yote ya nchi imekufa mpaka kuwezekana watu waliokataliwa kwa makosa ya uadilifu, kurejeshwa kwenye ofisi nyeti za Serikali na chama kinachotawala?Dhambi ya siasa nyepesi

Wanazuoni wa sayansi ya siasa walileta msamiati unaoitwa kwa Kiingereza “populism”, ukiwa na tafsiri ya karibu na neno “popolarismo”, lilipo kwenye kamusi ya siasa Italia. Maana yake ni siasa za kujijenga kwa watu wa kawaida.

Mwanasiasa mwenye siasa za mtazamo wa ki-populism huitwa populist. Ambacho hufanya ili kukubalika kwa wananchi wa maisha ya chini ni kujenga hoja za ulinganisho wa matabaka. Kuwafanya wananchi wa kawaida kuona wananyonywa.

Vilevile, mwanasiasa populist hutaka ionekane viongozi waliopo na matajiri (elite class), wanafaidi uchumi wa nchi kuliko wengine. Hujenga picha hakuna ulinganifu katika mgawo wa keki ya Taifa. Kwamba elite class wanamega karibu keki yote, halafu kidogo inayosalia ndio hugombewa na kundi kubwa la tabaka la chini.

Aghalabu, mwanasiasa populist hutengeneza uadui na tabaka la juu (elite class), hivyo kujenga uhusiano mzuri na wananchi wa kawaida. Hata Lula, kilio chake Brazil ni wanasiasa populist, ambao walijaribu kumwandama kwa kesi mfululizo, ili kuufanya umma umtambue kuwa si mwenye nia njema na nchi.

Kadhalika, alichokuwa anakifanya Musiba ni kuuonyesha umma kuwa Magufuli ndiye kiongozi aliyekuwa na nia njema na wananchi wanyonge, na kwa sababu hiyo tabaka la juu lilimpiga vita. Majina ya Kinana, January na Nape yakaingia kwenye mlango huo. Kuna wakati wanasiasa populist hujenga hoja za matabaka kwa haki, lakini mara nyingi hutengeneza utengano kwa hila za kisiasa, ili kukubalika kwa wananchi wa kawaida. Je, Kinana, January na Nape walishughulikiwa kwa haki? Kama ndio, basi tuamini kuwa Rais Samia ameunda Serikali ya ulinzi kwa tabaka la juu.

Ikiwa Kinana, January, Nape na wengine, walizushiwa kwa hila za kisiasa, basi mifumo ya nchi inapaswa kuimarishwa mno. Maana siku zijazo, ataibuka populist mwingine. Pengine mambo yakawa mabaya kuliko yaliyoshuhudiwa kabla ya Rais Samia.

Rais William Ruto na Gachagua ni wanasiasa populist. Ndio maana siasa zao wameeleza ni za kujenga uchumi kuanzia chini. Wametengeneza mtazamo kuwa viongozi waliokuwepo kabla yao ndio waliofaidi keki ya taifa kuliko wananchi wa kawaida.

Wakasema wanajenga “Taifa la Wapambanaji” – “Hustler Nation”. Bodaboda na akina mama wachuuzi wa mbogamboga (mama mboga) ndio serikali yao. Ni sababu wananchi wa chini waliamini kashfa za rushwa za Gachagua ni za kutunga kwa chuki. Eti vigogo walitaka kumdidimiza mkombozi wa wanyonge. Ni populism. Siasa za kujiegemeza kwa wananchi wa chini.

Mifumo mizuri, kuanzia kwenye vyama, Bunge madhubuti hadi Mahakama imara, husaidia udhibiti wa hila za viongozi wenye kujiegemeza kwenye siasa za wananchi wanyonge. Mara nyingi uongo ndio huwa mtaji wa wanasiasa populist.