SHEKHAN RASHID: Tunawatengenezea mchongo wa Ulaya wachezaji wa Tanzania
Muktasari:
Gazeti hili liliofanya mahojiano na mmoja wa waanzilishi na mchezaji wa timu hiyo, Shekhan Rashid juu ya mambo mbalimbali yanayohusu timu hiyo na mikakati yake katika kufanikisha ndoto za wacheza soka wengi hapa nchini kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa Ulaya.
Mshindwe wenyewe. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wachezaji soka wa Tanzania wanaoishi Sweden kuunda timu iitwayo Kilimanjaro ambayo msimu huu imepanda daraja na mwakani itashiriki ligi daraja la sita.
Gazeti hili liliofanya mahojiano na mmoja wa waanzilishi na mchezaji wa timu hiyo, Shekhan Rashid juu ya mambo mbalimbali yanayohusu timu hiyo na mikakati yake katika kufanikisha ndoto za wacheza soka wengi hapa nchini kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa Ulaya.
Ilipotoka
Shekhan mchezaji wa zamani wa Moro United na Simba anasema timu hiyo ilianza kama sehemu tu ya wachezaji kukutana na kufanya mazoezi lakini kadri siku zilivyokwenda wakaamua kuisajili katika mamlaka za soka nchini Sweden.
“Tumetoka mbali kaka, timu yetu ilianza kama sehemu ya kujifurahisha tu lakini tukaona tuisajili rasmi ili itambulike. Huo ukawa mwanzo wa Kilimanjaro,” anasema mchezaji huyo wa zamani wa Taifa Stars.
Wachezaji
Kiungo huyo anasema kwa sasa timu ya Kilimanjaro inaundwa na wachezaji kutoka mataifa Gambia, Kenya na Tanzania ambayo imetoa zaidi ya nusu ya wachezaji wanaounda kikosi hicho.
“Watanzania ndiyo tupo wengi, lakini pia kuna wachezaji kutoka Kenya na golikipa anayetoka Gambia,” anasema Shekhan na kuwataja nyota wa Watanzania wanaokipiga katika timu hiyo kuwa ni Athuman Machuppa, Credo Mwaipopo, Willium John, Ahmed Dadi na Khamis Abui.
Kwanini Kilimanjaro FC?
Mchezaji huyo anasema lengo la kuipa timu yao jina la Kilimanjaro FC ni kutaka kusaidai juhudi za Serikali ya Tanzania kutangaza vivutio vya kitalii vilivyo hapa nchini.
“Mbali na kucheza soka lengo leu ni kutangaza vivutio vya kitalii vilivyopo Tanzania, hivyo tukaona ni vyema tutumie jina la Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu Afrika uliopo Tanzania.”
Mafanikio
Mchezaji huyo anasema mafanikio yameanza kupatikana Oktoba 7, 2016timu hiyo ilitoka sare ya bao 1-1 na Solna FC na hivyo kufanikiwa kufuzu kucheza ligi daraja la sita msimu ujao na kuwataka wadau mbalimbali ikiwamo Bodi ya Utalii Tanzania kusaidia, mbali na kucheza ligi, itakuwa ikiutangaza utalii wa Tanzania.
“Tumefanikiwa kuipandisha timu kutoka daraja la saba hadi la sita.Tunaomba wadau huko nyumbani na nje ya Tanzania kuunga mkono juhudi hizi zinazolenga kuwanufaisha wachezaji wa Tanzania baadaye, kwamba timu ikifika mbali, watakuwa wakija na kuonekana na timu nyingine,” alisema.
Mikakati
Kuhusu mikakati waliyojiwekea ili kufanikisha timu hiyo kufika daraja la tatu, Shekhan anasema watakaa kufanya tathimini kabla ya kutoka na mikakati kabambe ya kutimiza malengo waliyojiwekea.
Malengo
Nyota alisema lengo kubwa ni kuhakikisha timu hiyo inakuwa njia ya wanasoka wa Tanzania kwenda kucheza Ulaya soka ya kulipwa lakini endapo tu itafanikiwa kupanda daraja la tatu.
“Malengo ni kuwawekea njia nzuri maana timu ikifika daraja la tatu inaruhusiwa kusajili wachezaji kutoka nje. Mungu akijalia tukifika huko tutachukua wachezaji kutoka Tanzania na kuwaleta Sweden lakini kwa kiwango na bidii ya mchezaji.
“Tumedhamiria kutumia fursa hii vizuri hivyo tunaomba wadau wajitokeze kusaidia katika mambo mbalimbali. Pia, Bodi ya Utalii Tanzania tunawaomba waungane nasi maana tuna lengo la kukuza utalii wa nchi yetu achilia mbali kucheza soka, tumeamua kufanya kazi zote, kusaka maisha katika soka lakini papo hapo tunaitangaza Tanzania huku,” anasema.
Neno Kwa TTB
Shekhana anatoa wito kwa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kushirikiana na Watanzania waliopo ughaibuni kuvitangaza vivutio vya kitalii vilivyopo hapa nchini.
“Sisi tumeamua kutumia soka kutangaza vivutio vya utalii lakini ombi letu kwa TTB kuwatumia Watanzania wanaoishi nje kuvitangaza vivutio vilivyopo nchini,” alisema.
Wabongo kazeni
Katika mahojiano hayo Shekhan anawataka wachezaji nchini kuongeza juhudi sambamba na kujitambua hatua itakayowafungulia njia ya kucheza Ulaya.
“Tunahitaji kuona wachezaji wengi wakija Ulaya kucheza soka hasa kwa kuanzia madaraja ya chini. Rai yangu kwa wachezaji waliopo huko ni kujitambua nini wanataka kufanya na kuwa na malengo yanayotekelezeka.
“Nasi tunahitaji kuona wachezaji wengi wa Tanzania wakicheza soka Ulaya, kama nilivyosema hii inakuwa ni njia tu, lakini bidii na juhudi za mchezaji zinahitajika...mataifa yaliyoendelea kwa soka wachezaji wengi wanacheza nje ya mataifa yao, sasa sisi tunmataka kuona wengine wanacheza nje,” anasema.