Walicheza Simba, Yanga, pia walizifundisha

Jamhuri Kihwelo
Muktasari:
Wapo baadhi ya wachezaji waliozichezea klabu hizo na baadaye wakapata mafunzo ya ukocha na kurudi kuzifundisha klabu hizo, ambapo wapo wengine waliopata mafanikio makubwa walipozinoa klabu hizo.
UWEPO wa klabu mbili kongwe za soka, Simba na Yanga umesaidia kuleta mafanikio kwa wachezaji wengi tangu zamani kwani wachezaji wa klabu nyingine hujituma kwa juhudi na maarifa ili siku moja waweze kucheza kwenye klabu hizi.
Wapo baadhi ya wachezaji waliozichezea klabu hizo na baadaye wakapata mafunzo ya ukocha na kurudi kuzifundisha klabu hizo, ambapo wapo wengine waliopata mafanikio makubwa walipozinoa klabu hizo.
Baadhi ya wachezaji hao waliozichezea Simba na Yanga wengine walikuja kuwa makocha wakuu, lakini wengine walikuwa makocha wasaidizi katika klabu hizo.
Ifuatayo ni orodha fupi ya wachezaji ambao waliwahi kuzichezea klabu hizi mbili na kupata nafasi ya kuzifundisha.
WALIOWAHI KUWA WACHEZAJI WA TIMU YA YANGA NA KUIFUNDISHA
Fred Felix 'Minziro'
Huyu aliichezea Yanga miaka ya 1987 akiwa beki wa pembeni wa kushoto, kabla ya kuja kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo.
Hivi sasa Minziro ni kocha msaidizi wa klabu ya Yanga akishirikiana na Mholanzi Ernest Brandts.
Charles Boniface Mkwasa
Aliwahi kucheza kwenye klabu ya Yanga akiwa mchezaji wa kiungo na alionyesha ujuzi wa kusakata kabumbu wa hali ya juu akiwa na klabu hiyo, ambapo baadaye alikuja kuwa kocha.
Kipaji cha Mkwasa kiliibuliwa na kocha Mohamed Msomali akiwa ni kocha wa timu ya Mseto ya Mjini Morogoro na baadaye alisajiliwa kuichezea Yanga.
Kenneth Pius Mkapa
Aliichezea timu ya Yanga kwa mafanikio makubwa miaka ya 1990 akiwa beki mahiri wa pembeni wa kutumainiwa na kikosi cha timu hiyo kipindi hicho.
Baada ya kustaafu alikuwa kocha msaidizi akiwa chini ya kocha mkuu wa timu hiyo, Dusan Kondic na kama kawaida aliipatia mafanikio makubwa timu hiyo hasa katika mechi za Ligi Kuu.
Baada ya kuichezea kwa mapenzi makubwa Yanga, Mkapa amekuwa mmoja ya wataalumu wa ufundi katika timu hiyo, akichukua zaidi nafasi ya umeneja, lakini hivi sasa anafundisha soka mkoani Iringa.
Mkapa alitamba akiwa kwenye kikosi cha Yanga na wachezaji kama Willy Mtendawema, Said Swed 'Scud', Godwin Aswile, Selemani Mkati, Sanifu Lazaro na Athumani China.
Salvatory Edward
Huyu ni mchezaji aliyecheza kwa umahiri mkubwa kwenye timu ya Yanga miaka ya 1990 akiwa mchezaji wa kiungo.
Salvatory akiwa kocha msaidizi wakati Yanga ilipokuwa ikinolewa na kocha Mserbia Kostadin Papic, timu ya Yanga ilipata mafanikio. Hivi sasa Salvatory ni kocha mkuu wa Yanga B.
Sekilojo Chambua
Alicheza kwenye timu hii akiwa anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, ambapo kabla ya kusajiliwa Yanga alikuwa ni mchezaji mahiri wa timu ya Tukuyu Stars ya Mbeya.
Licha ya kuichezea Yanga kwa mafanikio, pia aliwahi kuteuliwa kuifundisha Yanga akiwa kocha msaidizi chini ya Mmalawi Jack Lloyd Chamangwana, ambapo kwa pamoja walifanikiwa kuipa Yanga ubingwa wa Tanzania Bara.
WALIOWAHI KUWA WACHEZAJI WA TIMU YA SIMBA NA KUIFUNDISHA.
Amri Saidi
Aliichezea Simba miaka 1990 na alicheza kwa umahiri mkubwa kiasi cha kuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo.
Miongoni mwa vitu alivyoweka historia baada ya kuwa kocha msaidizi wa Simba ni pale alipoiongoza Simban na kuifunga Yanga kwa mabao 4-3, baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri kwenda kwao Zambia kwa shughuli za kifamilia.
Jamhuri Kihwelo 'Julio'
Aliichezea Simba kabla ya kuwa kocha msaidizi na baadaye kocha mkuu na sasa akishika nafasi ya Meneja na kocha msaidizi wa timu hiyo.
Pamoja na mafanikio aliyoyapata katika timu ya Simba, mwaka 2008 alikuwa ni kocha wa timu hiyo, lakini kilimtokea kitu kibaya kwani alitimuliw na viongozi wa Simba wakati huo baada ya kupata matokeo mabovu mfululizo.
Selemani Matola
Ameichezea Simba katika nafasi ya kiungo miaka ya 2000 na baadaye alienda Afrika Kusini kuichezea kwenye timu ya Super Sports ya huko.
Wakati Yanga ikandamizwa mabao 4-3, Matola alikuwa kwenye benchi la ufundi akisaidiana na marehemu kocha Syllersaid Mziray na Amri Said.
Aliwahi kupewa nafasi ya kuifundisha timu ya Simba ya vijana 'Simba B',kabla ya kujiengua.
Abdallah Kibadeni
Alikuwa akicheza nafasi ya ushambuliaji katika timu ya Simba katika miaka ya 1970.
Wachezaji aliowahi kucheza nao Simba wakati huo ni Mohamed Bakari, Haidari Abied, Aloo Mwitu, Mohamed Kajole, Idd Juma, Omar Gumbo na Mwenyekiti wa sasa wa Simba, Ismail Aden Rage.
Mwaka 1990, aliifundisha timu hiyo akiwa chini ya marehemu SyllersaidMziray na kuiongoza vema kuifunga Yanga bao 1-0 likifungwa na mlinzi wa kushoto, Mavumbi Omari.
Simba iliandika historia ya kufika fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, chini ya kocha Abdallah Kibadeni aliyeichezea kwa mafanikio makubwa Simba katika miaka ya 1974 na kuiongoza timu yake kufikia hatua ya robo fainali ya Kombe la Mabingwa barani Afrika (CAF).
Hassan Hafif
Alikuwa ni mchezaji na mwalimu kwa wakati mmoja kitu kilichompa sifa na kuwa na mashabiki wengi hasa wanaoipenda na kuitakia mema timu hiyo.
Mashabiki wa soka watakuwa wakimkumbuka Hafif kupitia fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, wakati Simba ilipoumana na Sport Club Villa ya Uganda mwaka 1990.
Katika mchezo huo, Hafif ambaye aliingia kipindi cha pili aliipatia timu yake bao la tatu, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, pia Hafif aliwahi kuwa msaidizi wa kocha Kibadeni alipokuwa akiinoa timu Simba.