Sugu kutoka yo! rap hadi ‘Bongoflava library museum in Dar’

Kama utani hivi ikaanza Summer Jam. Bongofleva ikiwa chini ya wahuni tu. Ilikuwa ngumu sana asiyerap (michano) kupokelewa kwa nguvu na mashabiki. Mashabiki walitaka wachanaji tu.

Dully Sykes na wenzake ujasiri wao na kutoogopa kwao. Wakaingia kwa miguu miwili. Na kufanya muziki kusiwe kwa ajili ya masela tu kama Manduli Mobb, GWM, LWP, BDP na wenzao.

Hata watoto wazuri wa kike wakaanza kuelewa. Muziki ukakamata sasa. Balaa likaendelea kwa uzao wa Mandojo na Domokaya. Hapo tayari Q Chilla na TID walikuwa na makazi yao maalumu kwenye muziki.

Vikajitokeza na kuzaliwa vipaji vingi tu. Licha ya wachanaji kuwa juu. Lakini uwepo wa mabishoo wa asili na roho za kisela kama Mr Blue, Ngwair na wengine. Ikawa kilainishi cha muziki na kuupeleka kibiashara zaidi.

Miaka ya nyuma zaidi. Beach Party na Yo! Rap Bonanza, zilichangia muziki kushika hatamu miaka ya 90. Ila Fiesta ikaamsha wasanii wengi miaka ya 2000. Mapromota kujiongeza na kubusti shoo, maisha yakawa mepesi zaidi.

Daraja la uswahilini na ushuani likavunjwa kama ukuta wa Berlin, kupitia muziki tu. Watoto kutoka Mikoroshini wakaiteka Obey. Watoto wenye taswira ya uswahilini wakawa juu kama minara ya kuongozea ndege.

Wazee wa fursa waliona muziki una maisha. Una pesa. Una utajiri. Ni zaidi ya biashara ya unga. Mwamko wa watu na mizuka ya Bongofleva ilikuwa hatari yenye hatari. Mungu akupe nini, gunia la chawa? Mapromota watangatanga kama wafugaji wa Kimasai.

Bongofleva ikatanuka kama kiatu cha plastiki juani. Ikianzia Dar na harufu yake kusambaa mikoani. Kila kona ya nchi zilianzishwa studio na wasanii kibao kurekodi. Licha ya kuleta wasanii kadhaa wa Marekani na kwingineko, bado wazawa walikimbiza.

Uzalendo wa kupenda vitu vya homu haujaanza leo. Walishakuja wengi sana. Lakini bado thamani ya almasi ya homu ikawa juu kuliko makinikia ya Marekani, Jamaica kama siyo Afrika Kusini. Nigeria walijaribu kutikisa uzalendo wetu kwa wasanii wazawa lakini wapi.

Kuna wakati Unigeria ikawa kama ndio kila kitu. Undava, ubabe na fujo za kizazi cha kina Diamond kilipambana. Nao pia hii leo ni mashabiki wa muziki wetu. Tuzo zilichukuliwa na Nandy na kina Vanessa kwenye vibaraza vya mama zao na Davido.
Miaka ya karibuni wasanii wa Marekani na kwingineko, wamewekwa kando. Kitakachotokea leo kilitokea miaka mingi nyuma. Sioni sababu ya wasanii kutoka Ulaya na Marekani kuja kuchota pesa kibwegebwege hapa.

Baada ya fujo za mwanzoni mwa miaka ya 90. Kim & The Boys ya Abdulrahman Magomelo (RIP), wakaleta kitu cha Yo Rap Bonanza. Hii ilikuwa chachandu ya kujaza upendo kwenye nyoyo za watu na muziki wa kizazi kipya. Na mtiti wa muziki huu ulipoendelea kuteka hisia za watu, Joseph Kusaga, Ruge na Prime Time Promotion, wakaja na Fiesta baada ya Summer Jam. Ikawa noma zaidi na funga kazi ya kuutangaza muziki huu ndani na nje ya nchi.

Fiesta pamoja na kuwapa vijana kipato kizuri, pia lilikuwa jukwaa kuu la 'kulink' kati ya Bongo na dunia. 'Kolabo' na nyota wa kimataifa zikaanza kuibuka kwa kasi. Na hapa Ambwene Yessaya 'AY', aliitumia fursa vyema.

Muziki huu kila baada ya muda unazalisha kitu. Baada ya msako wa maokoto ya vijana wapya wakiongozwa na Mondi. Leo hii umeibua kitu cha kuitwa Bongo Flava Honors. Lengo ni kuwapa heshima wachonga barabara.

Ni wazo la Joseph Mbilinyi 'Sugu', lakini wazo limetokana na mazingira ya sasa. Vijana wanapata pesa nyingi lakini wale ambao ndio chanzo cha dili hili ni kama wanapuuzwa hivi. Bongo Flava Honors ipo kwa ajili yao.

Lakini pamoja na hayo bado tunaambiwa kuwa kuna haja ya kwenda mbele zaidi. Sugu kaleta wazo jipya tena la kujenga maktaba ya muziki huu. Ni Bongo Flava Library Museum In Dar. Lengo ni kuweka kumbukumbu sawa kwa kizazi vijavyo.
Yes! Akili ya kuwaza uwepo wa hiki inatokana na kinachoendelea. Mafanikio ya wasanii wa sasa ndio msukumo ulipo. Lazima watu wajue kile kilichompa utajiri na umaarufu mkubwa Diamond kilitoka wapi? Safari ilikuwaje?

Kuna Mbongofeva ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma 'FA', kilichompa umaarufu ni kitu gani? Kimetoka wapi? Huu muziki unahitaji kuwekwa kwenye mazingira ya kumbukumbu sahihi.

Sugu kutoka Hiphop Summit, Daladala Swahili Arts, Vinega wa Anti Virus, Bongo Flava Honors na sasa anatuletea Bongo Flava Museum. Hii ni kubwa kuliko, kwa sababu dunia ya sasa haijui kilichotokea mwanzo.

Dunia inaenda mbio sana. Usipoweka sawa kumbukumbu utasahaulika kama ugonjwa wa kisonono na ndui. Bongofleva haijaota kama ukoka. Iliandaliwa. Ikakua ikajengwa na kuimarishwa kila baada ya muda fulani. Bongo Flava Museum In Dar inakaribia.