Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taji Liundi, jina muhimu lisilotajwa Bongo Fleva (2)

Taj Liundi

Muktasari:

Wiki hii tunaendelea kuungazia muziki huu na harakati za taji Liundi kuupa nguvu.

Dar es Salaam. Wiki iliyopita tuliona jinsi Taji Liundi alivyoweza kuuingiza muziki wa Bongo Fleva sokoni kwa kuupa nafasi kwa mara ya kwanza hewani akitumia kituo cha Radio One Stereo ambako alikuwa mtangazaji.

Wiki hii tunaendelea kuungazia muziki huu na harakati za taji Liundi kuupa nguvu.

Anaeleza kuwa wakati harakati za kukuza muziki zikiendelea, kukaibuka makundi mengi ikiwamo la Four Cruise Flavour, ambalo ndiko alikotokea mwimbaji wa miondoko ya R&B, Mr Paul ambaye alipata sifa kutokana na kurudia kibao cha “Zuwena” kilichotungwa na Marijani Shaaban.

Nani mwanzilishi wa neno “Bongo Fleva”

Taji anasema akiwa ameshaondoka Radio One Stereo na mrithi wa kipindi chake kuwa Mike Mhagama ndipo siku moja alisikia “Bongo Fleva” likitamkwa kumaanisha muziki wenye vionjo vya Tanzania.

“Niliwahi kufanya naye mazungumzo akanileleza kuwa yeye siku moja akiwa studio anaendesha kipindi alitumia neno hilo la Bongo Fleva kuutambulisha muziki ambao wakati huo vijana walishagawanyika wengine wakipenda kuimba na wengine kurap, hivyo ninaamini ndiye alianzisha neno hilo,” anasema Liundi.

Hapo ndipo alipoona alichokuwa anafikiria kuhusu kukuza vipaji vya vijana wa Tanzana, kilitimia.

Hakuna dhana sahihi iliyowahi kuwekwa bayana ya muziki wa Bongo Fleva, lakini kilicho bayana ni teknolojia ya kurekodi muziki iliyorahisisha kazi kiasi kwamba vijana wengi wakaweza kuingia studio bila ya kuambatana na lundo la wapiga ala.

Bongofleva pia ilichagizwa na midundo iliyokwisharediwa na uwezo wa kompyuta kufanya mambo mengi, ndiyo iliyorahisisha vijana wengi kumudu kuingia studio na kurekodi. Walichotakjiwa kufanya ni kutunga mashairi na kurap au kuimba sambamba na midundo. Mambo mengine hufanywa na producer.

Taji anaona huo umekuwa ukombozi kwa vijana. Wakati ule hakukuwa na kitu ambacho wangeweza kufanya, kusikiliza, kushawishika kama ilivyokuwa kwa muziki huo. Kila mtu sasa anataka kuufanya.

Anasema leo asilimia 60 ya Watanzania ni vijana, hivyo miaka 20 iliyopita ule ndiyo walikuwa wanakua, na kwamba katika suala la burudani wasingeweza kwenda na kasi ya bendi kongwe za Msondo na Sikinde.

“Ilikuwa kuna msukumo kutokana na masuala ya utandawazi na soko huria, pia kuiga mambo ya Magharibi. Lakini nilihakikisha wanakuwa wastaarabu wanavaa vizuri, ili angalau muziki huo usionekane wa kihuni. Majukwaani nilikuwa nazima muziki kama mwimbaji hakuwa amevaa vizuri na namshusha jukwaani,” anasema.

“Kizuri zaidi umekuwa ukirithiwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine huku kukiwa na mabadiliko makubwa; kwanza ulivyokubalika, pili vijana wenyewe walivyo wabunifu.”

Anafafanua ingawa aliona Zimbabwe wamefanikiwa, anaamini mafanikio yamekuwa makubwa zaidi Tanzania na muziki wa vijana unakwenda na wakati, ukiungana na mfumo wowote wa mabadiliko bila kutetereka na kutaka ubaki kama ulivyoanza.

“Makundi kama siyo waimbaji walioanza kipindi kile wakati wa harakati, walikuwa wanapenda kurap, lakini sasa unaweza kuona aina zote za muziki zinapigwa ndani ya Bongo Fleva, hakuna anayelalamika kuwa aina fulani ya muziki inabaniwa na nyingine kuachiwa,” anasema.

Anaeleza kuwa katika mafanikio hayo kuna changamoto hasa kwa wasanii wenyewe, kama kujiamini kupita kiasi na kufanya vitu ambavyo labda vinaweza visiwajengee heshima katika muziki wao. Anatoa mfano wa tungo ambazo haziwezi kudumu.

Anazitaja sababu za kuchuja mapema nyimbo kuwa ni maudhui au mada zinazozungumziwa kwenye nyimbo nyingi kuwa hazina mashiko na zinatungwa haraka.

Alitola mfano wa wimbo wa Diamond na Ney wa Mitego uitwao “Mapenzi na Pesa”, kuwa hauwezi kudumu. Utachezwa kwenye vituo vya redio na TV, lakini hauwezi kuwa na mashiko ya kuendelea kwa sababu ni kama wamekurupuka.

“Kuna mifano ya utunzi, angalia mwimbaji kama Lady Jay Dee, hajawahi kukosea. Sisemi kama hao siyo waimbaji wazuri, ni wazuri lakini wanatakiwa kujipanga na kujipa muda wa kutunga ili kuhakikisha muziki unaishi, ”alisema Liundi.

Anasema anamuheshimu Jide kwani hakuwahi kukosea, siku zote alijipanga, anatunga nyimbo za maisha ya kawaida bila kujifanya anajua sana au hajui kabisa.

Anafafanua kuwa Jay Dee hakuanza muziki ukiwa unalipa bali ukiwa chini kabisa na alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakipiga simu na kuimba redioni laivu kutaka kipaji chake kitambulike.

“Amekomaa, na sasa unalipa na bado anafanya vema,” alisifu Taji.

“Siwapondi wasanii wa sasa, lakini inabidi wakaze msuli ili kutunga nyimbo zitakazoishi kama za kina Juma Nature, Profesa Jay, Mr 2, ambao walitunga nyimbo ambazo ukizisikia hadi leo unaamini hiyo ndiyo Bongo Fleva, kwani miaka 10 bado ipo katika ubora ule ule,” anasema Liundi.

Ni kifanyike ili kukuza muziki wa kizazi kipya

Liundi anasema kila kitu bila kusomea ni ngumu kukifanya kwa ufasaha, ingawa wapo watu wenye vipaji ambao wanaweza kufanya bila kupata elimu, lakini wengi wao wanahitaji kusoma ili waweze kutambua na kuthamini kazi zao.

Anasema iwapo waimbaji wataelimishwa muziki na kuelewa, wakafundishwa kupiga ala, kutunga mashairi ya kufikirika, yatakayomgusa kila anayesikia, hakutakuwa na haya malalamiko ya muziki jojo.

Bifu wasanii na watangazaji kisa nini?

Liundi anasema tatizo ni watangazaji kuwa mameneja wa wasanii, kitu kinachosababisha watangazaji kuwapa nafasi wasanii walio chini yao tu.

Anasema iwapo wasanii wangekuwa na mameneja wengine, kusingekuwa na uhasama kama huu. Anasema pia watangazaji hutaka fedha ili wazicheze nyimbo za wasanii redioni.

“Hili suala huwa nalisema mara nyingi. Ni vigumu kulithibitisha kutokana na hawa watu kuwa makini wanapofanya mambo yao, lakini ukweli unabaki pale pale wasanii wanahonga fedha ili nyimbo zao zichezwe redioni,”anasema Liundi.

Maisha baada

ya utangazaji

Liundi anasema kuwa alipoacha kutangaza alikuwa mshereheshaji wa shughuli mbalimbali akilenga zaidi za mashirika.

Anasema alipokuwa akiendelea na kazi hiyo hakusahau kuwa anaweza kutangaza tena vizuri licha ya kuwa hakusoma kabisa masuala ya habari, hivyo akafikiri jinsi ya kurudi kwenye fani.

. “Ninachotaka kufanya sasa ni kurudi kwenye habari kwa staili ya aina yake, kwa kuwa ninafanya kazi nyingi za kusherehesha mashirika mbalimbali ikiwamo ya umma, karibu kwa wiki kazi nne hadi tano, nitakuwa nawahoji baadhi ya watu hasa wahusika wakuu katika kazi husika na kufanya kipindi, ”anasema.

“Hiyo itakuwa fursa nyingine kwa wenye kampuni kupata wasaa mzuri wa kuelezea wanachofanya na kikasikika na kueleweka na watumiaji wa huduma zao badala ya kuzungumzia ndani katika ukumbi wakiwa wenyewe na bila kuficha kazi hiyo nitaifanya katika kituo cha matangazo cha Azam,” anasema.