CCM yaionya ACT-Wazalendo kuacha kejeli

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM (Zanzibar), Khamis Mbeto akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za chama hicho Kisiwandui. Picha na Jesse Mikofu

Unguja. Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo waache kutumia lugha za kejeli na matusi wanapowakosoa viongozi wa Serikali na chama tawala wakiwa kwenye mikutano ya hadhara.

Kauli hiyo ya CCM inatokana na mikutano miwili ya hadhara iliyofanywa na ACT-Wazalendo Februari 26, Nungwi Unguja na Machi 4 Tibirinzi Pemba mwaka huu, ambapo viongozi wake waliibua masuala mbalimbali waliyodai ndiyo chanzo cha umasikini wa Zanzibar na viongozi wameshindwa kuyatatua.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto alisema hawatakubali kuona wanasiasa wanatumia majukwaa kueleza uongo na kupotosha umma kwa makusudi ili Serikali ichukiwe.

Alisema CCM ipo tayari kukosolewa na kuelezwa kasoro zilizopo, lakini kwa njia ya kistaarabu bila kutumia kauli za kejeli na matusi kama wanavyofanya baadhi ya viongozi wa ACT-Wazalendo.

Hata hivyo Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasilino na Umma wa ACT Wazalendo, Salim Bimani alisema chama kimekosoa kwenye mikutano ya hadhara na wamejenga hoja kwa wahusika, hivyo watoke hadharani wajibu hoja.

“Sisi tunathamini utawala bora na utawala wa sheria, tunaamini Zanzibar moja, yenye mamlaka kamili, tunataka vyombo husika vionyeshe kasoro tulizotaja.”

Alisema kuhusu lugha za kisiasa kila mtu ana tafsiri yake “lakini hatujakashifu, pengine kuna jambo limemuuma mtu sisi tumezungumza ishu na ishu ndio siasa, tunaheshimu taratibu zote za kisiasa,” alisema Bimani.

Katika mkutano wake wa jana, Mbeto alisema umiliki wa kampuni ya usafirishaji Uwanja wa ndege wa Zanzibar (Dnata) kuchukua asilimia zote na kuwaacha wazawa na sakata hilo wanaliachia vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake.

Alisema kupitia kampuni hiyo tayari kuna ajira zaidi ya 375, sawa na asilimia 70 zimetolewa.

Kuhusu mamlaka kamili inayodaiwa viongozi wa ACT-Wazalendo, Mbeto alisema Zanzibar inatakiwa ijisimamie. Alisema nchi kuwa na mamlaka kamili sio njia ya kukuza uchumi, kwani yapo baadhi ya mataifa, ikiwemo Hongkong, Dubai na Scotland hazina mamlaka kamili, lakini uchumi wao upo juu duniani.

Akizungumzia ukosefu wa chakula, Mbeto alisema Zanzibar kilo moja ya mchele wa pembe inauzwa Sh2,000, huku kiroba cha kilo 25 kikiuzwa kwa Sh45,000, akidai hakuna ukosefu wa chakula maana kwa mwezi inatumia tani 11, lakini mpaka sasa kuna hifadhi ya tani 50 za mchele.

Alisema ndani ya miaka miwili Serikali imetangaza ajira zaidi ya 2,900 katika sekta za elimu na afya, huku kukiwa na ajira zisizo za moja kwa moja na nyingine katika sekta binafsi, hivyo kufikia mwaka 2025 ajira zilizotolewa katika ilani ya CCM (Zanzibar) zaidi ya 300,000 zitakuwa zimefikiwa.

Mbeto alisema Serikali kupitia mfuko wa hazina imetoa Sh16.8 bilioni kwa ajili ya kuwakopesha wajasiriamali wadogo na tayari vikundi 2,200 vimeshapewa mkopo huo na walionufaika si makada wa CCM pekee kama ilivyoelezwa.