Safari ya Zitto iliyojaa majanga ACT, anavyokiacha chama kwenye ubora

Naikumbuka siku, Novemba 2013, jioni. Nilipokea ujumbe wa simu kuwa Naibu Katibu Mkuu Chadema, Tanzania Bara, Zitto Kabwe alivuliwa nafasi zote za uongozi kwenye chama hicho. Kosa ni kubainika kuandaa waraka wa kimapinduzi.

Pamoja na Zitto, wengine ni Profesa Kitila Mkumbo, ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, vilevile aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba. Wakati Zitto alivuliwa nafasi za uongozi, Kitila na Mwigamba, walivuliwa uanachama.

Zitto, hakuwa tu Naibu Katibu Mkuu Chadema, bali pia Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni. Nafasi hiyo pia aliipoteza. Alikaribia kupoteza na ubunge wake, jimbo la Kigoma Kaskazini (Chadema), akawahi mahakamani kukizuia chama hicho kujadili uanachama wake.

Yalikuwa mapito magumu kwa Zitto, mwanasiasa kijana maarufu aliyependwa na kila rika. Alikuwa kivutio cha vijana wengi kujiunga na siasa, na kutamani kuwa viongozi, jinsi alivyoliteka Bunge kwa hoja makini. Aliposimamia hoja aliyodai kuwa mgodi wa Buzwagi uliuzwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Zitto akawa juu kabisa ya kilele cha umaarufu wa kisiasa Tanzania.

Wanafunzi waliokwenda bungeni kusoma kwa vitendo, walichanganyikiwa walipomwona Zitto. Aliaminiwa kuongoza kamati za kudumu za Bunge za Mashirika ya Umma (Poac) na Hesabu za Serikali (Pac). Hoja yake ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ikakusanya saini za wabunge wa upinzani hadi CCM. Ikabidi mawaziri nane walazimishwe kujiuzulu Mei 2012, kumwokoa Waziri Mkuu.

Kashfa ya uchotwaji fedha Benki Kuu kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, iliyohusisha mgogoro wa kibiashara baina ya Tanesco na kampuni ya IPTL, ilidhihirisha umahiri wa Zitto. Mawaziri wawili, Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini) na Profesa Anna Tibaijuka (Ardhi), pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, waliondolewa Baraza la Mawaziri. Aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, aliondolewa ofisini.

Nyota haikupaa kwa sababu ya kashfa ya uhusiano wa kimapenzi na mbunge mwenzake, aliyekuwa mke wa mtu, marehemu Amina Chifupa, bali kwa kazi. Alikuwa mbunge wa upinzani aliyependwa hadi na CCM. Wengi wakasema alikuwa kipenzi cha Rais Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM.

“Nasubiri kuona Zitto atakavyojibu mapigo, nakiamini sana kile kichwa,” aliandika Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma “MwanaFA”, wakati huo akiwa hata siyo mbunge. Ni baada ya Zitto kuvuliwa vyeo vyote Chadema. Zitto aliaminika, alijenga ahadi kubwa ya kesho yake ya kisiasa.

Sarakasi za mahakamani ziligota ukingoni Machi 10, 2015. Baada ya shauri lake kutupiliwa mbali na Mahakama, haikuchukua muda, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, alitangaza rasmi kuwa Zitto alipoteza uanachama wake. Wakati huo, Lissu alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema.

Mchoro maarufu wa katuni, ukimwonesha Zitto anamwagilia mche unaoanza kuota, kwa matumaini ya kukua ili uwe mti mkubwa. Ni uwasilishaji wa mchoraji gwiji, Ally Masoud “Kipanya”, akitafsiri kazi ngumu ambayo Zitto alikuwa nayo, kuhakikisha anakijenga chama kipya, ACT Wazalendo, kiweze kukua na kitoe ushindani.

Katuni hiyo haikuwa mbali na kitovu cha ukweli. Matumaini yote ya ACT-Wazalendo, yaliegemea kwa mtu mmoja; Zitto. Mbio za urais hadi mchuano wa wabunge majimboni, chama hicho kilitegemea nguvu ya Zitto.

Bahati mbaya kwa Zitto na ACT, Uchaguzi Mkuu 2015, ulikuwa mgumu zaidi katika historia ya siasa Tanzania. Waziri Mkuu aliyejiuzulu Februari 2008, Edward Lowassa, alicheza karata ngumu kushinda urais. Rais Kikwete, alicheza mpira mgumu, kuhakikisha Lowassa hafanikiwi.

Kikwete akiibeba CCM begani na mgombea wake, Dk John Magufuli, Lowassa kwa tiketi ya Chadema, akibeba baraka ya vyama vingine vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ikasababisha taifa ligawanyike vipande viwili; wa Magufuli (Kikwete na CCM), wa Lowassa (Ukawa). ACT, chama kichanga, kilikutana na dhoruba kali.

Oktoba 15, 2015, aliyekuwa mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, alifariki dunia kwa ajali ya helikopta, iliyotokea kwenye pori la Selous, kijiji cha Mtende, Morogoro. Baada ya kifo hicho, Zitto alieleza jinsi ambavyo alishirikiana na Deo kuasisi ACT.

Kisha, Zitto akaingia kwenye mgogoro mkubwa na aliyekuwa mshirika wake wa karibu, David Kafulila, ambaye ni mbunge wa Kigoma Kusini 2010 – 2015. Kafulila hakuhamia ACT. Hiyo ikawa asili ya mgogoro wa washirika hao wa kisiasa, waliojenga uhusiano mithili ya mtu na mdogo wake, tangu walipokuwa Chadema.

Hiyo ndiyo tafsiri ya Zitto kuingia ACT na mguu mbaya; alitakiwa kuisaidia ACT katika uchaguzi mgumu mno, uliokuwa umetekwa na pande mbili. Mshirika wake muhimu, Deo, alipoteza maisha kabla ya uchaguzi. Halafu “mdogo wake” Kafulila, aligoma kuambatana naye ACT. Kafulila alibaki NCCR-Mageuzi.

Uchaguzi Mkuu 2015, ACT walionesha hamu kubwa kwenye majimbo. Walisimamisha wagombea ubunge wengi, wakishika nafasi ya pili nyuma ya CCM. Hata hivyo, matokeo hayakuwa mema kwao. Mbunge mmoja tu, Zitto, ambaye alifanikiwa kushinda ubunge jimbo la Kigoma Mjini na akawezesha ACT kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mgombea urais wa ACT, Anna Mghwira, alipata kura 98,763 katika kura 15.2 milioni, zilizopigwa kuchagua rais. Magufuli na Lowassa, peke yao walikusanya kura 14.95 milioni, katika jumla ya kura 15.2 milioni. Huo ni uthibitisho kuwa mchuano wa uchaguzi ulikuwa wa pande mbili. Hakukuwa na fursa ya mgombea wa tatu kuleta changamoto ya matokeo (kingmaker scenario).

Machi 28, 2015, Zitto alichaguliwa kuwa Kiongozi wa ACT, Machi 29, 2015, Tanzania ilifanya Uchaguzi Mkuu. Hivyo, Zitto alikiongoza chama hicho kwa miezi saba kasoro siku tatu, uchaguzi ukawadia. Baada ya uchaguzi, kilikuwa kipindi cha kuuguza majeraha ya kushindwa. ACT haikufikisha japo asilimia tano ya kura za wabunge, iweze kupata fursa ya kuteua wabunge wa viti maalum pamoja na ruzuku.

Ulipowadia mwaka 2016, Dk Magufuli akiwa Rais wa Tanzania, alipiga marufuku shughuli za kisiasa. Zikageuka nyakati za vuta nikuvute baina ya viongozi wa upinzani na dola. Zitto alikuwa mmoja wa viongozi waliolala mahabusu mara nyingi. Halafu, wabunge na madiwani wa upinzani walihamia CCM kwa hoja kumuunga mkono Magufuli. Zitto alipoteza madiwani ndani ya halmashauri yake.

Aliyekuwa Mshauri Mkuu wa ACT, Profesa Kitila, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, kisha aliyekuwa mgombea urais, Anna Mghwira, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Zitto na ACT yake, walibaki wapweke. Watu muhimu kwenye chama, Dk Magufuli aliwasajili na kuwatumia kwenye serikali yake.

Machi 18, 2019, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad, aliongoza kundi kubwa kuhama kutoka Cuf na kuhamia ACT. Ni kutoka hapo, angalau ACT ikapata nguvu Zanzibar. Ikajenga matarajio ya wabunge wengi au hata kushinda urais visiwani. Uchaguzi Mkuu 2020, dunia ilishuhudia uharibifu mkubwa. Vyama vyote vya upinzani vililia. ACT haikuwa na nafuu.

Kulekea Uchaguzi Mkuu 2020, ACT walimpokea mwanasiasa na mwanadiplomasia nguli, Bernard Membe. Matumaini yaliongezeka. Membe akateuliwa kuwa mgombea urais wa ACT. Hata hivyo, kadiri siku zilivyosogea, mazingira yalimtafsiri Membe kuwa mmoja wa wagombea dhaifu.

Uchaguzi Mkuu 2020 ulipomalizika, Membe alitangaza kujivua uanachama wa ACT. Miezi mitatu baada ya kumalizika uchaguzi, Seif “Maalim” alifariki dunia. Mpaka sasa pengo la Seif halijaweza kuzibwa ndani ya ACT. Awali, ilionekana Seif angeibeba ACT Zanzibar na Zitto, Tanzania Bara. Alipoongezeka Membe, matumaini yakawa makubwa.

Kwa mantiki hiyo, kuondoka kwa Membe na kifo cha Seif, mambo hayo mawili yaliiumiza mno ACT. Halafu mpaka wakati huo, hakukuwa na fursa ya kufanya shughuli za kisiasa. Vyama vya upinzani vilijitutumua kwa vipimo vidogo. Vivyo hivyo kwa ACT.

Januari 3, 2023, ruhusa ya kufanya siasa ilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan. Vyama vya siasa vikaanza kufanya mikutano ya hadhara na shughuli nyingine za kisiasa bila bughudha. Machi 2024, Zitto amekabidhi uongozi wa chama kwa Kiongozi mpya, Dorothy Semu.

Kikokotoo kitakuonesha kuwa Zitto alifanya siasa kwa nafasi, miezi saba Rais akiwa Kikwete. Kipindi chote cha Magufuli, fursa ilikosekana. Halafu akafanya siasa tena kwa mwaka mmoja baada ya Rais Samia kutoa ruhusa. Hivyo, kutoka Machi 2015 mpaka Machi 2024, ni miaka tisa ya uongozi wa Zitto, ila amefanya siasa kwa mwaka mmoja na miezi saba.

Kuondoka kwa Seif ni pengo lisilozibika, lakini angalau uwepo wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud na viongozi wengine kama Ismail Jusa, Juma Duni, Nassor Mazrui na wengine, kunaifanya ACT ibaki na matumaini makubwa Zanzibar. Anaacha upweke.