Ado Shaibu athibitishwa tena katibu mkuu ACT Wazalendo, ataja kipaumbele

Muktasari:

  • Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama cha ACT- Wazalendo, wamemthibitisha Ado Shaibu kuhudumu katika nafasi ya Katibu Mkuu wa chama kwa miaka mitano ijayo.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amesema kipaumbele chake cha kwanza ni kujenga taasisi imara katika mifumo madhubuti, akisema atatekekeleza hilo kwa staili ya uongozi wa pamoja.

Amesema hayo leo Alhamisi, Machi 7, 2024 muda mfupi baada ya wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho kumthibitisha kutumikia nafasi hiyo kwa miaka mitano ijayo.

Ado amewaambia wajumbe hao kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake ndani ya miaka minne, kazi ya ujenzi wa taasisi hiyo hakuifanikisha ipasavyo.

"Nasema mbele yenu kazi ya ujenzi wa taasisi hatujaifanikisha vizuri, lakini nafurahi moja ya vipaumbele vya mwenyekiti (Othman Masoud Othman) ni kwamba tuna nia ya ujenzi wa mifumo madhubuti ya taasisi.

"Baada ya kujenga mifumo tutaendelea kujiimarisha na kazi inayofuata ni kujenga msingi madhubuti wa taasisi ya ACT - Wazalendo kuwa taasisi madhubuti ya kisiasa Afrika," amesema Ado.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, nafasi ya katibu mkuu ilipigiwa kura, lakini kutokana na mabadiliko ya katiba ya chama hicho, hivi sasa nafasi hiyo ni ya uteuzi na kuthibitishwa na wajumbe halmashauri kuu.

Kikao cha halmshauri kuu kimeongozwa kwa mara ya kwanza Othman aliyechaguliwa jana katika mkutano mkuu wa nne uliofanyika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, wajumbe hao walimchagua Dorothy Semu kuwa Kiongozi wa Chama (KC), akirithi mikoba ya Zitto Kabwe aliyetumikia nafasi hiyo kwa mihula miwili iliyohitimishwa Machi 5,2024.

Kilichobaki ni sekretarieti mpya ambayo wakati wowote itatangazwa na kuridhiwa na wajumbe wa halmashauri kuu ya ACT- Wazalendo. Sekretarieti hiyo itajumuisha manaibu makatibu wakuu Tanzania Bara na Zanzibar, makatibu wa ngome za vijana, wazee na wanawake na wakuu wa idara.

Awali, wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho walisema ni wakati muafaka kwa Ado kuendelea kuhudumu nafasi hiyo kutokana utendaji kazi wake wa miaka minne.


Katibu wa ACT- Wazalendo, mkoa wa chama hicho wa  Chake chake, Pemba Saleh Juma amesema Ado amefanya kazi kubwa anayopaswa kuindeleza, hivyo hakuna sababu kuwekwa nje ya mfumo wa uongozi.