Wakongwe waingia, watupwa CCM

Wanachama wa CCM wakimpongeza Mwinshehe Mlao (kulia) baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Pwani wakati wa uchaguzi uliofanyika wilayani Kibaha, mkoani humo juzi. Picha na Sanjito Msafiri

Dodoma/mikoani. Uchaguzi wa CCM ulioanza kuandia juzi ngazi ya mkoa umerejesha wakongwe wa siasa nchini huku wenyeviti kwenye mikoa minne yenye majiji -- Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Mbeya na Dodoma waking’olewa.

Aidha, uchaguzi huo umeshuhudia zaidi ya wenyeviti 15 kati ya 26 wakiwemo hao wa majiji wakitupwa nje, ama kwa majina yao kukatwa na vikao wakati wa mchujo na wengine kushindwa katika sanduku la kura.

Si kwa wenyeviti tu, uchaguzi huo ambao umekuwa ukilalamikiwa na baadhi ya wajumbe wa maeneo mbalimbali kukithiri kwa vitendo vya rushwa, umewatupa nje baadhi ya makada waliokuwa wakitetea nafasi zao za ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) na mkutano mkuu.

Kutemwa kwa vigogo hao, kumeshuhudia sura zingine zilizowahi kushika nafasi hizo miaka ya nyuma zikirejea kwenye ulingo, hali inayotazamwa na wachambuzi kuwa inaweza “kutokana na msukumo awamu za uongozi katika chama.”

Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa alisema, “hii ndio maana ya uchaguzi, kama ingekuwa nafasi fulani inashikiliwa na mtu moja kwa moja, kusingekuwa na haja ya uchaguzi, lakini hii inatufundisha uongozi ni dhamana, kuna kuingia na kutoka.”

Dk Kahangwa alisema, “lakini unaweza kukuta CCM kuna hali fulani, hawa walioingia kuna wa miaka ya nyuma na uongozi wake ulikuwa mwingine, sasa wakati fulani unaweza usiwe mtoto pendwa kwa viongozi wa juu waliopo kwa hiyo kambi ndani ya CCM inaweza kuwa sababu moja ya haya kutokea.”

Alisema kuna fukuto ndani ya CCM, “hasa kuelekea uchaguzi mkuu 2025, wajumbe wa NEC na mikutano mkikuu ndio wanaoamua, sasa wale wanaotiliwa shaka kukwamisha baadhi ya mambo, wanawekwa kando. Lakini pia fukuto kwa wale wanaoona wanastahili kuendelea au la, wakaamua vinginevyo chini kwa chini.”

Dk Kahangwa anaungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya siasa na maendeleo, Bubelwa Kaiza aliyesema kinachoonekana katika uchaguzi wa CCM ni uwepo wa makundi.

“Kuna kundi la akina Dk Bashiru Ally ambao wanapambana kubaki kwenye chama chao baada ya vitu walivyovifanya kuanzia mwaka 2017 kubadilishwa vyote, mfano mtu kubaki na cheo kimoja, kwa hiyo yapo mashindano ya makundi mawili.

Natarajia mashindano yajionyeshe, haya mbadiliko yanayojionyesha baadhi ya watu majina yao kukatwa, sijui wametoa rushwa, ni namna ya kundi moja kutafuta njia ya kudhibiti kundi lingine, kwa hiyo haya ni mashindano katika awamu mbili, ukiangalia viongozi walioondolewa kwenye utawala uliopita sasa wanarejeshwa,” alisema.

Katika uchaguzi huo uliomalizika jana, Mkoa wa Dar es Salaam wenye historia ya siasa za ushindani, umepata mwenyekiti mpya, mwanasiasa mkongwe nchini, Abbas Mtemvu.

Ni jiji ambalo limekwiongozwa na wanasiasa wakongwe kama, Ramadhani Nyamka, Hemed Mkali, John Guninita, Ramadhani Madabida na mwanamke pekee Kate Kamba.

Kate Kamba aliyekuwa akitetea kiti hicho hakuweza kufua dafu mbele ya Mtemvu, mtoto wa mpigania uhuru wa Taifa hili, Zuberi Mtemvu.

Alhaji Zuberi Mtemvu alikuwa mwanaharakati na mzalendo aliyeshiriki katika kupigania uhuru wa Tanganyika katika miaka 1950.

Abbas aliyewahi kuwa mbunge wa Temeke mwaka 2005, juzi alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

Pia, mkoani Mbeya ambako kumekuwa na siasa za upinzani kwa muda mrefu umepata mwenyekiti mpya wa CCM, Dk Stephen Mwakajumilo.

Chama katika mkoa pamoja na wengine, kwa miaka ya karibuni kimewahi kuongozwa na Nawab Mullah, Godfrey Zambi na Jacob Mwakasole aliyeshindwa kwenye uchaguzi wa juzi, pia umekuwa ni ngome ya upinzani kwa muda mrefu.

Jiji lingine ambalo mwenyekiti wake ameshidwa uchaguzi ni Dodoma, makao makuu ya nchi na Serikali ambapo aliyekuwa akitetea kiti hicho ni Godwin Mkanwa amekaa kwa muhula mmoja kabla ya kupigwa na Adam Kimbisa ambaye amerejea mara ya pili.

Kimbisa alichukua uenyekiti kutoka kwa William Kusila miaka 10 iliyopita na katika uchaguzi uliofuata 2017 hakugombea na nafasi hiyo ikachukuliwa na Godwin Mkanwa, na sasa Kimbisa amerejea. Jiji la Mwanza lenye idadi kubwa ya watu nalo limekuwa na siasa za upinzani wa nje na ndani ya CCM, limepata mwenyekiti mpya baada ya kuondoka Dk Anthony Diallo, aliyekaa kwa miaka 10 baada ya kurithi mikoba ya Clement Mabina. Nafasi hiyo sasa imechukuliwa na Sixbert Jichagu.

Yaliyojitokeza kwa majiji hayo ni sawa na kilichotokea Mkoa wa Tanga ambapo aliyekuwa mwenyekiti wake, Henry Shekifu jina lake lilikatwa na vikao vya juu huku jijini Arusha, Zelothe Steven akiendelea kupigania nafasi yake kwa kuwa hadi tunakwenda mitamboni matokeo yalikuwa hayajatangazwa.


Vigogo waliotupwa

Mbali na wenyeviti hao, chaguzi huo umewatupa vigogo wakiwamo mawaziri wawili wastaafu na mkuu wa mkoa mmoja na wakuu wawili wastaafu wa wilaya kwa kuenguliwa na NEC kwenye nafasi walizokuwa wakigombea za ujumbe wa NEC na uenyekiti kwenye mikoa ya Arusha na Manyara.

Mawaziri waliong’olewa ni Philip Marmo ambaye alikuwa anagombea nafasi ya uenyekiti Mkoa Manyara na Dk Mary Nagu ambaye alikuwa anagombea nafadi ya ujumbe wa NEC.

Dk Nagu pia aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uwaziri ikiwamo waziri wa uwezeshaji katika ofisi ya waziri mkuu.

Wengine waliofyekwa ni mkuu wa mkoa mstaafu wa Morogoro, Loata Sanare aliyekuwa akigombea wenyekiti Mkoa wa Arusha sawa na Lembrice Kivuyo aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Rombo.

Imeandikwa na Samira Yusuph (Simiyu) Daniel Makaka na Saada Amir (Mwanza), Rehema Matowo (Geita), Baraka Loshilaa, Bakari Kiango, Tuzo Mapunda (Dar es Salaam), Habel Chidawali (Dodma),Gasper Andrew (Singida), Yohana Challe (Mbeya), Hamida Shariff (Morogoro), Janeth Joseph (Kilimanjaro)