ACT Wazalendo yafurahia mchakato wa Katiba mpya

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro akizungumza akifungua kikao kazi cha mafunzo ya namna ya kutumia Tehama kwenye upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wasajili wasaidizi wa watoa huduma za masaada wa kisheria jijini Arusha.

Muktasari:

  • Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimefurahishwa na hatua ya Serikali kuandaa bajeti kwa ajili ya mchakato wa Katiba mpya.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza kufurahishwa na tamko la Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro kuhusu kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mchakato wa Katiba mpya.

Dk Ndumbaro alitoa tamko hilo juzi, Machi 24, 2023 wakati wa kikao cha Baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo jijini Dodoma aliposema Sh9 bilioni zitaongezeka katika bajeti ya wizara hiyo yam waka 2023/24 kugharimia mchakato wa Katiba mpya.

“Tujipange inawezekana Sh9 bilioni isitoshe kwa hiyo lazima tujipange kuomba nyongeza ya bajeti. Hivyo ikifika Septemba hadi Oktoba tuwe tumejipanga,” alisema Dk Ndumbaro.

Leo, Machi 26, 2023 Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Dorothy Semu amewaambia waandishi wa habari kuwa fedha hizo zitawezesha kupata sheria mpya ya vyama vya siasa mwaka huu.

“ACT Wazalendo inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhusu mchakato huu,” amesema Dorothy.

Semu ameitaka Serikali kuharakisha hatua za utekelezaji wa masuala hayo kwa kutoa ratiba kama ilivyopendekezwa kwenye ripoti ya kikosi kazi.

“Tunaamini itakapofika Novemba mwaka huu tuwe na sheria mpya ya vyama vya siasa, uchaguzi na kuwepo na sheria itakayoelezea mchakato wa Katiba mpya utafanyikaje,” amesema.

Dorothy amesema tayari chama hicho kimeona muda huo pia utatosha kuunda kamati ya wataalamu kwa ajili ya kuwianisha katiba pendekezwa ili kupata rasimu mpya itakayopigiwa kura na wananchi.

Hata hivyo, amevitaka vyama vyote vya siasa kuwa na lugha moja kwenye kushinikiza utekelezwaji wa hilo, ili kuepuka ucheleweshwaji.

 “Tunavisihi vyama vyote vya siasa kuvuta upande mmoja ili kufanikisha mageuzi haya na kuepuka kuwa na njia zisizo rasmi zitakazochelewesha mchakato huu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu ametangaza ratiba ya awamu ya pili ya mikutano ya hadhara ya chama hicho itakayofanyika katika Mikoa tisa.

Ameitaja Mikoa hiyo ni Ruvuma, Shinyanga, Katavi, Mwanza, Kahama, Simiyu, Njombe, Geita na Rukwa.