AFP waitaka Serikali kutekeleza Katiba

Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima nchini (AFP), Rashid Rai akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Chaduru, wilaya ya Dodoma Mjini, mkoani Dodoma.

Muktasari:

  • Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, Chama cha Wakulima Nchini (AFP) kimefanya mkutano wake wa kwanza wa hadhara na kushauri kufanyika kwa mambo mbalimbali ili kuleta ustawi wa Taifa.

Dodoma. Chama cha Wakulima (AFP), imeshauri Serikali ya awamu ya sita kujikita katika utekelezaji wa Katiba kwa kuondoa umasikini, ujinga na maradhi ili kuwaepusha Watanzania na changamoto wanazokutana nazo katika maeneo hayo.

Katibu Mkuu wa AFP, Rashid Rai ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa kwanza wa hadhara tangu Rais Samia Suluhu Hassan aondoe zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, lililodumu kwa zaidi ya miaka saba, tangu mwaka 2015.

Katika mkutano huo, uliofanyika Chaduru, wilayani Dodoma, Rai ameitaka Serikali kujikita katika kutekeleza Katiba iliyopo ya mwaka 1977 katika kuondoa umasikini, ujinga na maradhi kama kifungu cha tisa cha Katiba hiyo kinavyoeleza.

“Hii ndio maana ya kaulimbiu yetu ya siasa na maisha ya watu, kwasababu ukiondoa umasikini, ujinga na maradhi utakuwa umefanya maisha ya watu yaboreke,”amesema.

Amesema ilivyo sasa bado kuna mgogoro mkubwa katika umasikini, mfumo wa kuondoa ujinga na afya ambapo watu wanataabika kupata huduma bora za afya.

Rai amesema leo hii ikitokea ukampeleka mgonjwa wako katika hospitali yoyote na ikitokea akafariki na ukawa hujalipa gharama za matibabu huwezi kuchukua mwili wa ndugu yako.

Naye Mwanasheria wa chama hicho, Kigoma Marwa, ameitaka Serikali kutumia miaka utajiri wa nchi ulioelezwa katika Katiba kwa ajili ya kugharamia afya na elimu kwa Watanzania.

“Katiba ilivyosema kuhusu utajiri wa nchi hii, matumizi yake yanatakiwa kwenda kuondosha umasikini, ujinga na maradhi inamaana kumbe walioandika Katiba hii walifahamu kuwa nchii ni tajiri,”amesema.

Naibu Katibu Mkuu Bara, Mark Isidory amewaomba Watanzania kushirikiana na chama hicho katika kutetea na kupigania maslahi yao yaliyoainishwa kwenye Katiba.