CCM yaeleza vinavyowapa jeuri chaguzi za 2024/ 2025

Mbunge wa Busokelo jijini Mbeya, Atupele Mwakibete.

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya kimesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi ndiyo silaha itakayowapa uhakika wa kushinda Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025.

Mbeya. Wakati joto la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwakani likianza kupanda, Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya kimeanza kuchora ramani ya kushinda Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

 Uchaguzi wa Serikali za mitaa unatarajia kufanyika mwakani 2024, huku ule mkuu ukifuatia mwaka 2025 ukiwa wa kuchagua wabunge na Rais.

Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa anayewakilisha Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela amesema kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi ndiyo silaha itakayowawezesha kuendelea kushika dola.

“Tunafanya kila liwezekanalo kwa kuwajibika kwa wananchi kuhakikisha wanapata huduma zote ndiyo maana tumepunguza na kuondoa kero ili chaguzi zijazo tubaki na viti vyote,”

“Hadi sasa kwa Mkoa wa Mbeya utekelezaji wa miradi ya maendeleo imefikia asilimia 85 na matarajio yetu hadi mwakani na kufikia 2025 tuwe tumekamilisha asilimia 100 katika huduma zote kwa wananchi,” amesema Ndele.

Mbunge wa jimbo la Busokelo, Atupele Mwakibete amesema kwa kipindi alichoongoza, amejitahidi kuwafikishia huduma wananchi ikiwamo miundombinu ya barabara, afya, elimu, maji na nishati.

“Tumejenga vituo vinne vya afya, zahanati nne na kuboresha nyingine nne, hospitali ya Wilaya iliyogharimu zaidi ya Sh2.6 bilioni na huduma za upasuaji zimeanza, lakini jengo la utawala lenye vyumba 200 kwa zaidi ya Sh8 bilioni,”

“Upande wa elimu zipo shule mpya mbili Busokelo Boys na Busokelo Girls, umeme tayari kila kijiji umefika, maji pia tumewafikia wananchi, hivyo rai yangu waendelee kuiamini CCM,” amesema Mwakibete.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Ghana Mashariki, Philimon Mwansasu amesema kutokana na kazi kubwa iliyofanywa hadi sasa anaamini CCM itaendelea kushinda kuanzia mwakani hadi 2025.

“Ukiangalia hata wabunge wapo kwenye majimbo yao kila mmoja akisikiliza na kutatua kero, hii ni silaha kubwa ambayo tunaenda nayo mwakani na kwenye uchaguzi mkuu ili kushinda,” amesema Mwansasu.

Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Isyesye, Novatus Mpoli amesema kutokana na kazi waliyoifanya chama hicho, tayari amepokea kadi 180 kutoka vyama vya upinzani kujiunga CCM.

“Walitukopesha watu imani, tunalipa kwa vitendo, tumetekeleza ilani na matarajio yetu ni kushinda viti vya mitaa na hadi uchaguzi mkuu, tunashukuru hadi sasa tumepokea kadi za vyama vya upinzani 180 waliojiunga CCM,” amesema Mpoli.