CCM yawaonya wanaojipitisha kutaka ubunge, udiwani

Muktasari:
- Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema wanachokifanya ni kuyumbisha chama.
Mkinga. Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewaonya makada wa chama hicho mkoani Tanga ambao wameanza kujipitisha kutangaza nia ya kutaka Ubunge na udiwani waache mara moja vinginevyo wakiendelea wanajimaliza wenyewe.
Makamu huyo wa Rais ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga ametoa onyo hilo Oktoba 9, 2023 wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho ngazi ya matawi na mashina waliopo wilayani Mkinga mkoani hapa.
Abdullah amesema wanazo taarifa kuwa wapo watu wenye matumaini wameanza kupitapita wakitaka kujenga msingi wa kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa CCM mwakani na Uchaguzi Mkuu wa 2025 kabla ya chama hakijafungua pazia lake.
Amesema chama hicho kina kanuni na taratibu zake na zinapaswa kuzingatiwa na CCM haitaruhusu mtindo wa kila mtu kuamua anavyotaka.
“Wabunge na Madiwani bado wapo madarakani kwenye majimbo na kata hizo. Waacheni wafanye kazi kwa amani, wasubiri muda mwafaka badala ya uvunjifu wa amani. Chama hakiruhusu hili,” alisisitiza
Amewaonya viongozi wanaojificha nyuma ya watu hao na kuacha kukigawa chama kwa kuwa wanajua wanaojitokeza sasa nyuma yao kuna watu wanawabeba.
Mlezi huyo pia amesema haridhishwi na kasi ya kazi za kisiasa zinazofanywa na viongozi wa Wilaya ya Mkinga na amewaagiza waongeze kasi na wawe karibu na wananchi.
"Unapoona nasema hivi lazima uelewe kwamba najua kuna tatizo, kazi ya kisiasa ina maana kwamba viongozi lazima washirikiane kwa karibu na watu wanaosikiliza matatizo yao na kutafuta ufumbuzi wao," amesema Abdullah
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abrahaman amesema ziara ya Mlezi huyo itawaimarisha kisiasa huku akipigilia msumari kwa kuwataka hao wanajipitisha wasubiri muda ufike lakini kwasasa waache waliopo madarakani wafanye kazi.
Mwenyekiti huyo amesema kwa sasa wanaendelea kukiimarisha chama chao kwanzia ngazi zote za mashina na matawi ndani ya mkoa huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amewataka wanaojipitisha wasubiri muda ufike lakini pia waache wabunge na madiwani waliopo madarakani wafanye kazi zao.
Kindamba amesema kuna maeneo wanasema anawapigia debe wabunge waliopo madarakani jambo ambalo amesema hao ndiyo wabunge anaofanya nao kazi kwasasa.