Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maandamano kama msafara wa mamba

Nikupongeze kwa hatua yako ya maridhiano na vyama vya upinzani. Tumeona jambo kubwa lililokuwa likiwatisha Watanzania kwa muda mrefu likifanyika bila kuzua taharuki.

Jambo hili ni maandamano yaliyoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia maandamano yaliyofanyika kwa utulivu mkubwa pamoja na kuwapo kwa hofu ya ndani kwa kila Mtanzania kama ilivyozoeleka.

Maandamano ni haki ya msingi kwa wananchi kama njia ya kupeleka ujumbe uliokusudiwa kwenye mahala palipokusudiwa.

Lakini tofauti na ukweli huo, maandamano yanayofanyika duniani kote yanatawaliwa na vurugu kutokana na kutokubaliana kwa makundi ya waandamanaji na Serikali zao pamoja na vyombo vyao vya ulinzi na usalama.

Sehemu kubwa ya dunia imekumbwa na hofu kutokana na hali ilivyo kwa sasa.

Katika kipindi cha miezi kadhaa katika kila pembe ya dunia, maandamano yamekuwa changamoto kila uchao. Tumeshuhudia mataifa mbalimbali yakitikiswa na mzimu huo kuanzia jirani zetu Wakenya, Afrika Kusini, Tunisia, Nigeria, hadi kule Ufaransa, Ujerumani, Georgia, Israel, Peru mpaka Brazil.

Kwa jumla sehemu kubwa ya dunia imemezwa na maandamano kwa sababu mbalimbali, zikiwemo uchumi, ubaguzi, vita na kadhalika.

Hofu inakuja pale maandamano yanapoendana na ghasia na vurugu zinazosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali, uchumi na mazingira. Wakati mwingine hasira za waandamanaji hupitiliza na kusababisha vyombo vya usalama kutumia silaha kuyazuia.

Kwa mfano Kenya kumekosekana utulivu kwa kile wanachokiita “hali ngumu ya maisha” ambapo kwa wiki kadhaa maandamano yanayoongozwa na kinara wa upinzani, Raila Odinga yamekuwa mwiba kwa Serikali.

Kule Afrika Kusini raia wanamtaka Rais Ramaphosa ajiuzulu kwa kuwa ameshindwa kushughulikia tatizo la ajira na rushwa. Tunisia wanadai kuchoshwa na “utawala wa mtu mmoja” ambapo wanamtuhumu Rais wao kutokuwajali wananchi wake, na kwamba anataka kutawala peke yake.

Wanigeria wanalalamikia uhaba wa noti na hali ngumu ya maisha.

Kiujumla kila waandamanaji wana madai yao, mengine ni ya ndani ya nchi kama yale ya Ufaransa ambapo wafanyakazi wanagomea kuongezwa kwa umri wa kustaafu, lakini yapo pia yanayotikisa dunia kama ubabe wa Israel dhidi ya Mamlaka za Palestina pamoja na kudhoofishwa kwa nguvu za Mahakama.

Lakini kwa Tanzania madai makubwa ni yale ya muda mrefu yanayotaka uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi.
Kila mmoja anakumbuka mwaka 2007 nchini Kenya ambapo zaidi ya watu 1000 walipoteza maisha katika ghasia za uchaguzi.

Maelfu ya watu waliandamana kupinga matokeo ya uchaguzi uliomuweka madarakani Mwai Kibaki na kusababisha vurugu zilizowapelekea Wakenya kunusa vita ya ndani. Siku chache zilizopita Rais Ruto alimwambia Odinga:

“Inatosha sasa huwezi kuendelea kuihujumu nchi kwa kisingizio cha maandamano”.

Lakini kabla alisikika akiwaambia viongozi wa dini nchini humo waombe Mungu wakati yeye na mamlaka zake wakijiandaa kupambana na waandamanaji. Wakati huohuo, Odinga mwenyewe amesikika mara kadhaa akisema hatishwi na kauli za Rais na makamu wake kwa vile hawamjui vema na hata baba yao alikuwa hawezi kumtisha.

Pengine kutokuelewana huku ndiko kunakoweza kupandisha hasira za waandamanaji. Na matokeo yake ni nguvu kubwa zaidi kutumiwa na waandamanaji, lakini pia na vyombo vya usalama katika kuyazima.

Kauli za ukinzani za wanasiasa zinaamsha ari ya maandamano, lakini pia vurugu na uvunjifu wa amani usio na ulazima wowote. Pengine hata maadui wa amani wanaweza kuutumia mwanya kama huo kufanya yao.

Kwa muda mrefu Watanzania walizoea kuona vurugu kwenye maandamano ya kisiasa. Kuna ukweli kuwa kwenye msafara wa mamba kenge huwa hawakosekani, hivyo watu wabaya hutumia maandamano ya amani kama sehemu ya kufanya uhalifu.

Na si maandamano ya siasa pekee, hata kukiwa na sherehe au shughuli inayohusisha mikusanyiko watu waovu huweza kuichukulia hiyo kuwa fursa kwao.

Huku uswahilini tulikuwa na ngoma yetu iliyokuwa bora sana ya mchiriku. Ngoma hii ilikuwa na chembechembe za ngoma ya mtaa kwa mtaa iliyoitwa Mdundiko.

Ingeweza kuanzia Mwananyamala ambako ndiko makao makuu ya kikundi, ikakata mitaa hadi Mbagala kwenye shughuli. Kila ilipokatiza iliondoka na kitongoji, maana ilimgusa kila aliyeisikia hata akatamani kuisindikiza.
Kama mashairi ya nyimbo zake yalivyokuwa yakiimbwa: “Kamuacha mume wake, kafuata mdundiko...” Ilipopita mitaani akinamama walitelekeza vyungu mekoni na kuserebuka nayo. Watoto nao waliifuata na kupotezwa umbali mrefu kutoka nyumbani.

Ilikuwa ngoma adhimu yenye mashabiki wengi, lakini ilishuka thamani yake kutokana na ukweli kwamba kwa kuwa ilijaza umati mkubwa kila iliporindima, vibaka wakaanza kuitumia kama kivuli cha kufanyia uhalifu.

Raia wema waliporwa pochi zao na simu, wanawake wakanyang’anywa kanga, vitenge na vitambaa vya kichwani, watoto wakadhalilishwa na matukio mengi ya maudhi yalitendeka.

Kwa kawaida maandamano hayatofautiani na ngoma hii. Wanakusanyika wenye nia ya dhati ya kufikisha ujumbe uliokusudiwa, lakini pia wahalifu wanaweza kuichukulia nafasi hiyo kama fursa kwao. Ukweli nimefurahishwa na ukomavu wetu kwa kuwapa ulinzi waandamanaji na kuwasikiliza maoni yao. Kwa mwenendo huu tuna kila sababu ya kufikia suluhu ya matatizo yetu bila bughudha. Hongera sana.