Mgombea Chadema akumbuka alivyobwagwa uchaguzi 2020

Upendo Peneza akizungumza na Wananchi katika mkutano wa hadhara unaofanyika katika eneo la Msufini Mtaa wa Msalala Kata ya Kalangalala mjini Geita.

Muktasari:

  • Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Ubunge Geita Mjini kupitia Chadema mwaka 2020 Upendo Peneza amesema kwa madhila waliyoyapata katika uchaguzi na kuwa hai hadi leo huo ni ushindi mkubwa kwake na chama.

Geita. Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Ubunge Geita Mjini kupitia Chadema mwaka 2020 Upendo Peneza amesema kwa madhila waliyoyapata katika uchaguzi na kuwa hai hadi leo huo ni ushindi mkubwa kwake na chama.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho unaendelea kwenye eneo la Msufini Mtaa wa Msalala Mjini, Geita Peneza amesema ulikuwa uchaguzi mchungu  na kwamba kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ni fursa kwake kuwatumikia wananchi nje ya Bunge.

Peneza amewataka wananchi kuonyesha mabadiliko kwa kuikataa CCM katika uchaguzi mkuu ujao wa serikali za mitaa ambao utaonyesha njia ya ushindi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumzia mgawo wa umeme unaendelea mkoani Geita, Peneza ameitaka serikali kujipanga upya kwakuwa mgawo huo unawaathiri wananchi hasa wafanyabiashara wadogo wanaotegemea nishati hiyo kuendesha biashara.

"Serikali inayokusanya kodi za walala hoi ambao pamoja na mgawo wanalipa kodi hii siyo sawa ni kuwaibia. Walisema mgawo ni miezi mitatu imeisha bado mgao upo hatuzuii walipe kodi lakini wapeni umeme wa uhakika ili wafanye kazi wapate fedha walipo kihalali huku mifuko yao ikiwa imetuna," amesema Peneza.

Akizungumzia Bima ya Afya kwa Wote, Peneza amesema Serikali haiwezi kuwa na bima hiyo wakati vijijini vituo vya afya viko umbali wa zaidi ya kilomita 20 huku vikiwa havina wataalamu wa kutosha wala dawa.

"Tunataka Serikali itekeleze vipaumbele muhimu kama dawa, watoa huduma pamoja na miundombinu rafiki na siyo kusema unaleta bima wakati unaongeza gharama kwa wananchi kuzifikia hospitali ambazo ziko mbali na maeneo hayo,"amesema.

Peneza amesema atatumia mikutano ya hadhara kupinga tozo zisizo rasmi kwenye sekta ya madini ambazo zinawaumiza wananchi wengi wa Geita ambao kazi zao kubwa ni uchimbaji wa dhahabu.