Mjumbe Chadema ahutubia mkutano wa ACT-Wazalendo

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akijadili jambo na Mwanasiasa wa Chadema, Dk Azaveli Lwaitama (kushoto) walipokutana katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru mjini Bukoba leo Jumamosi Juni 3, 2023. Katikati ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji. Picha na Erick Boniphace.

Muktasari:

  • Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Dk Azaveli Lwaitama apanda katika jukwaa la ACT- Wazalendo na kutoa ujumbe unaoshiria vyama vya vyenye malengo yanayofanana sio vema kurushiana vijembe.

Kagera. Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Dk Azaveli Lwaitama, amepanda katika jukwaa la ACT- Wazalendo na kuhutubia akisema anawapenda Zitto Kabwe na Juma Duni Haji kwa sababu wana madini.

 Dk Lwaitama ambaye ni mwanazuoni amepanda katika jukwaa hilo leo Jumamosi Juni 3, 2023 wakati viongozi hao hao wakihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Uhuru Plattform wilayani Bukoba mkoani hapa.

Msomi huyo aliyevalia kofia rangi ya nyekundu sambamba na fulani yenye rangi hiyo iliyoandikwa ' Katiba Mpya' amesema Zitto ambaye ni Kiongozi wa ACT- Wazalendo na Duni Mwenyekiti wa chama hicho; ni jamaa zake.

"Nikiambiwa Zitto na Duni wanakwenda kuhutubia nakwenda kuwasikiliza hawa jamaa ni wenzangu hawa jamaa ni madini matupu nyie vijana wa mjini madini matupu," amesema Dk Lwaitama ambaye aliwahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwanazuoni huyo, ambaye pia amewahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine amesema Duni ni miongoni mwa watu waliomfundisha kuhusu mamlaka kamili ya Zanzibar.

Katika ujumbe wake, Dk Lwaitama amesema sio sahihi kwa vyama vya siasa vyenye lengo moja kurushiana vijembe wenyewe kwa wenyewe badala yake waunganishe nguvu na kupambana na adui yao.

"Watu wanabishana halafu wana lengo moja lakini tofauti ni sera, msiruhusu kuchochewa na kutumia nguvu nyingi dhidi ya mabishano yenu, balala yake elekezeni nguvu zenu kwa yule anayewachochea," amesema Dk Lwaitama.

Kwa upande wake, Zitto amemshukuru Dk Lwaitama kuhudhuria mkutano wake, akisema msomi huyo ni mzee wake tangu wakiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

"Dk Lwaitama yeye ni mtaalamu wa lugha lakini mimi nilikuwa nasoma uchumi, lakini nilikuwa nashinda ofisini kwake hadi watu wananishangaza,” amesema Zitto na kuongeza;

"Nakushukuru sana kwa kuungana nasi leo naunga mkono hoja yako kwamba hakuna sababu ya msingi pale ambapo vyama mnapiginia jambo moja mnaanza kurushiana mawe, badala ya kumrushia yule mnayepigana naye.”

Zitto ameongeza kuwa, hakuna sababu ya kutukana na kupigana badala yake wanasiasa wanapashwa kubadilisha taarifa za kufikia malengo yao, na kwamba ni kwa bahati mbaya wanasiasa wa Tanzania hawajafikia hatua hiyo.

“Inawezekana watu mkawa na lengo moja mkapita njia tofauti na sio vizuri kudhani njia ya mtu mmoja ndio sahihi," amesema.

Zitto amesema hivi sasa mjadala mkubwa ni Katiba Mpya na bahati nzuri katika jambo hilo hawatofautiani, isipokuwa namna ya kuuendea mchakato huo ili kuhakikisha mchakato unafanikiwa.