Netumbo Nandi - Ndaitwah; Mwanamama anayeandika historia mpya Namibia

Kama ambavyo imekuwa vigumu kwa mwanamke kupata nafasi kwenye jamii yenye mfumo dume, ndivyo ilivyokuwa vigumu kwa Netumbo Nandi-Ndaitwah, mpigania ukombozi nchini Namibia ambaye kupitia chama cha Swapo amekuwa kiongozi wa kitaifa.

Kwa miaka zaidi ya 50 sasa ambayo amekuwa mwanasiasa na kiongozi, amedhihirisha kwamba wanawake wana uwezo wa kuwa sehemu ya mabadiliko ya jamii na chemchemi ya maendeleo ya Taifa lake na watu wake.

Nandi-Ndaitwah, mwenye umri wa miaka 71, ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Namibia baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Taifa hilo, Hage Geingob ambaye alifariki dunia Februari 4, mwaka huu na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa makamu wake, Nangolo Mbumba.

Kabla ya uteuzi huo, Nandi-Ndaitwah alikuwa akifanya kazi kama Naibu Waziri Mkuu wa Namibia na pia Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, akiwa mwanamke pekee anayeshika nafasi ya juu katika serikali ya nchi hiyo.

Ameanza kwa kuweka rekodi ya kuwa makamu wa Rais wa kwanza mwanamke katika taifa hilo lililopata uhuru wake mwaka 1990 kutoka kwa makaburu wa Afrika Kusini. Anatazamia kuandika rekodi nyingine ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika Taifa hilo.

Nasema hivyo kwa sababu tayari amepitishwa na chama chake cha Swapo kuwa mgombea urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, atakabiliana na wagombea wa vyama vingine vya upinzani.

Rais Mbumba, aliyeshika kijiti cha urais baada ya kifo cha Geingob, analivusha taifa hilo katika kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu na yeye hatagombea nafasi hiyo, bali chama kilimpitisha Netumbo kuwa mgombea wake wakati Rais Geingob anapotarajiwa kumaliza muhula wake wa pili.


Maisha ya kisiasa

Nandi-Ndaitwah alianza safari ya maisha ya kisiasa katika chama cha Swapo ambako amekuwa akifanya kazi kuanzia miaka ya 1970, hasa akiwa kiongozi wa juu wa taifa hilo la kusini mwa Afrika anayebeba matumaini ya wananchi wake.

Kati ya mwaka 1976 – 1978, Nandi-Ndaitwah alikuwa akifanya kazi kama naibu mwakilishi wa Swapo katika nchi ya Zambia na baadaye mwaka 1978 – 1980, alipanda cheo na kuwa mwakilishi mkuu wa chama hicho nchini humo.

Baadaye mwaka 1980 – 1986, aliteuliwa kuwa mwakilishi mkuu wa Swapo wa Afrika Mashariki na makao makuu yake yalikuwa Dar es Salaam, Tanzania. Hivyo, ameishi Tanzania na anazungumza kidogo lugha ya Kiswahili.

Nandi-Ndaitwah ameshiriki kikamilifu katika mapambano ya kupigania ukombozi wa taifa hilo, akiwa ndani na nje ya nchi yake hadi hapo walipopata uhuru mwaka 1990 na Swapo kuunda Serikali.

Aliendelea kuwa kiongozi wa chama na alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya Swapo kati ya 1976 – 1986 na pia alikuwa Rais wa Umoja wa Wanawake wa Namibia (Nanawo) baada ya kupata uhuru kati ya mwaka 1991 – 1994.

Mwanamke huyo amekuwa mbunge tangu mwaka 1990, huku akifanya kazi katika wizara tofauti, ikiwemo ya Mambo ya Nje kabla ya kuteuliwa hivi karibuni kuwa Makamu wa Rais katika Taifa hilo.


Kugombea urais

Katika mchakato wa ndani ya chama wa kumpata mgombea urais baada ya Rais Geingob, Nandi-Ndaitwah amejipanga kuweka rekodi ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia kwenye uchaguzi wa Novemba, baada ya kuthibitishwa na chama chake.

Akiwa Makamu wa Rais wa Swapo, Nandi-Ndaitwah alifanikiwa kushinda uchaguzi wa ndani kwenye mkutano mkuu wa Swapo uliofanyika Novemba 24 – 28, 2023 akipata kura 491, sawa na asilimia 58 ya kura zote zilizopigwa.

Mpinzani wake wa karibu, Waziri Mkuu wa Namibia, Saara Kuugongelwa-Amadhila ambaye alikuwa chaguo la Rais Geingob, alipata kura 270.
Kura hizo zinamwezesha Nandi-Ndaitwah kupeperusha bendera ya Swapo kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mifumo thabiti ya chama hicho tawala itaivusha salama Namibia katika kipindi hiki ambacho wamempoteza kiongozi wao, Geingob ambaye pia alikuwa mpigania ukombozi katika taifa hilo akiwa nje ya nchi na hata aliporejea, aliendelea kuwa tumaini kubwa kwa wananchi.

Kuongezeka kwa rushwa serikalini na ukosefu wa ajira kwa vijana kunaongeza hasira ya wananchi, jambo ambalo linaelezwa kwamba litawapa nafasi wapinzani kuidhoofisha Swapo hasa kwenye majimbo.

Wanamikakati wa upinzani wanaeleza kwamba uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Novemba mwaka huu utakuwa na ushindani mkali na wamedhamiria kukinyang’anya chama cha Swapo umiliki wa theluthi mbili ndani ya Bunge.

Mpinzani wake wa karibu anatarajiwa kuwa Pandueli Itula, ambaye alipata asilimia 30 ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2019, kikiwa ni kiwango cha juu kwa upinzani kwenye uchaguzi wa Rais. Anaongoza chama cha Independent Patriots for Change (IPC).

Swapo imekuwa ikishuhudia kushuka kwa kura zake.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2019, Geingob alipata asilimia 56 ya kura zilizopigwa. Kura hizo zimepungua ukilinganisha na asilimia 76 alizopata mwaka 2015 alipogombea kwa mara ya kwanza.

Uchaguzi wa Namibia pia unasifika kwa uwazi wake na uadilifu. Mazingira ya uchaguzi yanaruhusu uhuru wa kukusanyika na uhuru wa kuzungumza kwa pande zote.

Mchakato huu unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Namibia (ECN) ambayo, ingawa si kamilifu, inaonekana kutopendelea upande wowote na inalenga kuwa na utekelezaji mzuri wa uchaguzi.

Siku za nyuma, ECN ilizipeleka Mahakamani kasoro za uchaguzi zilizoibuliwa na vyama vya upinzani.

Mahakama ya Namibia pia haiingiliwi na nguvu za ushawishi wa kisiasa, iko huru. Hili linadhihirika kwenye matukio ambayo Mahakama ya Juu imechukua kesi zilizopelekwa na upinzani na kutoa uamuzi tofauti na msimamo wa ECN.


Atunukiwa tuzo UDSM

Mchango wa Nandi-Ndaitwah siyo tu unatambulika ndani ya Namibia, bali pia na mataifa mengine. Anatambulika kama kinara wa ustawi wa maisha ya binadamu ndani ya Namibia, Afrika na duniani kwa ujumla.

Desemba 6, 2020, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilimtunukia mwanamke huyo udaktari wa heshima (PhD) kama ishara ya kutambua mchango wake katika ustawi wa wananchi wa Namibia, Afrika na dunia, hasa katika ushiriki wake kama mpigania uhuru, kiongozi na mlinzi wa haki za binadamu.

Nandi-Ndaitwah ambaye siku hiyo alitunukiwa shahada hiyo na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, alianza harakati zake za kupigania uhuru akiwa msichana wa miaka 17 tu, mwaka 1969 alipojiunga na Swapo.

Wasifu wake uliosomwa siku aliyotunukiwa heshima hiyo, unaeleza kwamba katika miaka sita aliyokuwa akiishi Dar es Salaam, Nandi-Ndaitwah alitumia ujuzi wake kutoa mihadhara kama mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Miaka ya 1970 – 1980, chuo hicho kilikuwa kitovu cha mihadhara iliyohamasisha ukombozi wa bara la Afrika. Nandi-Ndaitwah alipokea mialiko mingi wakati huo na kwenda kushiriki chuoni hapo akizungumzia mapambano ya ukombozi wa Afrika.


Familia yake

Nandi-Ndaitwah, ambaye ni mama wa watoto watatu, katika maisha yake hapa Dar es Salaam, aliishi Magomeni na alifunga ndoa na Luteni Jenerali Epaphras Denga Ndaitwah katika kanisa la Magomeni, wilaya ya Kinondoni.

Wakati akiishi Dar es Salaam, Mwalimu Nyerere alikuwa akimwita Nandi-Ndaitwah “Mama Swapo” na alishirikiana naye katika harakati za kudai uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika, ikiwemo Namibia.

Alikuwa ni mmoja katika familia ya watoto 13 na baba yake alikuwa mchungaji. Alijikuta analazimika kuwalea watoto wake watatu peke yake kutokana na wakati mwingi mume wake kuwa mbali kwa majukumu yake ya kikazi.

Anasema malezi hayo yamemfanya kuwa hivi alivyo sasa.

Amepambana kuvunja minyororo ya mfumo dume hadi kuwa kiongozi wa juu wa Namibia; kuanzia kwenye chama chake cha Swapo hadi serikalini.

Kama mama, Nandi-Ndaitwah amekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za wanawake kwenye kila nafasi anayokuwepo. Alikuwa miongozi mwa watendaji mkuu katika mkutano wa wanawake uliofanyika Beijing, China, mwaka 1995.