Rais kusikiliza kero za wananchi sawa, lakini…

Hivi karibuni, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda aliutangazia umma kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ametenga siku moja ya mwezi kuanza kusikiliza kero za mwananchi mmoja mmoja.

Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita jijini Dar es Salaam. Akasema utaratibu huo utakuwa ukifanyika katika Ofisi ya Chama (CCM), Lumumba Dar es Salaam, Dodoma au Zanzibar kulingala na mahali atakapokuwapo Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho tawala.

Alisema anafanya hivyo kama kumuenzi Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi aliyefariki Februari 29, mwaka huu na kuzikwa Zanzibar, Machi 2.

Sina tatizo na dhana ya kiongozi kusikiliza wananchi waliomchagua, lakini najiuliza sababu ya Rais kuanza kusikiliza mtu mmoja mmoja, halafu utatuzi wake utakuwaje? Je, kama ni mashauri ya kisheria, atayatatua kama mtawala au kama Mahakama au atatoa matamko ili kuwapatia suluhu wananchi?

Rais ni kiongozi mkuu wa nchi na Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Chini yake kuna wasaidizi wa kila aina; kuna mawaziri, kuna wakuu wa mikoa, kuna wakuu wa wilaya na watendaji wa taasisi zikiwamo majeshi ya ulinzi na usalama, kuna vyombo vya uchunguzi.
Vilevile, kuna serikali za mitaa ambako kuna viongozi na watendaji wa Serikali na kuna viongozi wa vitongoji, vijiji na madiwani.

Ukija kwenye mifumo ya utoaji haki, Mahakama ndiyo chombo pekee cha kutoa haki ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande mwingine, kuna Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo linawakilisha wananchi. Moja ya kazi ya wabunge ni kuwakilisha wananchi bungeni.

Sasa watendaji na viongozi wa siasa wote hao, wameshindwa kuwaskiliza wananchi kero zao, hadi tena Rais aingilie kati?

Tukumbuke, CCM ilishinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 kwa zaidi ya asilimia 90.

Uchaguzi huo pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ulilalamikiwa na wadau vikiwemo vyama vya siasa, kwamba haukuwa sifa ya kuitwa uchaguzi.

Hata Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana alipohutubia mkutano mkuu wa ACT Wazalendo Machi 5, 2024, aliahidi chaguzi zijazo zitakuwa huru na haki na alisema wenye hofu ya kauli hiyo wana haki kwa sababu wanakumbuka yaliyotokea mwaka 2019 na 2020.

Sasa kwa chaguzi hizo zilizoipa CCM ushindi wa mafuriko, tangu vitongoji, vijiji na mitaa, madiwani, wabunge na hapo hapo kuna viongozi walioteuliwa na Rais tangu ngazi za wilaya, mikoa na ngazi za Taifa, kote huko wameshindwa kusikiliza wananchi na kutatua kero zao?

Hao wote ni wasaidizi wa Rais katika kutekeleza majukumu yake. Halafu utasikia kwamba wananchi wanadhulumiwa haki zao; wanadhulumiwaje?
Tafsiri yake ni kwamba viongozi hao wa kuchaguliwa wameshindwa kazi na ndio maana Rais mwenyewe anaingilia kati kusikiliza wananchi? Kama wameshindwa wamechukuliwa hatua gani?

Vinginevyo, utaratibu huu wa Rais kuanza kusikiliza kero za wananchi unaweza kuwa umeandaliwa kisiasa ili kutafuta huruma za wananchi, kwamba viongozi wako karibu na wananchi.

Lakini ieleweke kwamba, kinachotakiwa ni wananchi kupata majawabu ya uhakika katika maisha yao.

CCM ndio chama chenye Serikali yenye mamlaka na mambo yote ya utekelezaji. Kinachosubiriwa ni utekelezaji, sio tena kuja kwa wananchi kusikiliza kero.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 walitoa ahadi mbalimbali, hivyo tunatarajia wakati huu wazitekeleze, sio tena kutuambia kuna dhuluma, kuna kero.

Nchi yetu ina tatizo la kumtanguliza mtu katika utawala, kwa mfano utasikia Rais katoa fedha za mradi huu, Rais kajenga hiki, Rais amefanya hili na lile, lakini tujue Rais ni kiongozi aliyepewa dhamana na wananchi.

Wananchi ndiyo walipakodi na kodi hiyo hutumika kuendesha Serikali, hivyo yanayofanywa na Serikali ni nguvu ya wananchi.

Nadhani njia sahihi ni kujenga mfumo wa kitaasisi ili wananchi watatuliwe kero zao kwa mifumo hiyo, bila kujali mtu aliyepo madarakani.

Hapa ndipo tunapoona haja ya kuwa na mabadiliko ya Katiba yatakayotoa nguvu ya mifumo ya kitaasisi tangu ngazi za chini hadi juu.

Tunapaswa kujenga mifumo ya kitaasisi itakayosimamia haki za wananchi katika ngazi zote. Rais baki kuwa msimamizi wa mifumo hiyo na msimamizi wa watendaji wanaowajibika chini yake.

Rais hawezi kuwa kama babu wa Loliondo anayegawa kikombe cha dawa kwa kila mtu, kwamba bila babu huyo kukupa mwenyewe kikombe cha dawa, hautapona.

Elias Msuya ni mwandishi mwandamizi wa Mwananchi – 0754897287