Zitto: Faraja kwangu kukutana na Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe (kushoto) akisalimiana na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe katika kikao cha wajumbe wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) jijini Dar es Salaam

Muktasari:

  • Safari ya maridhiano imekuwa turufu ya kukutanisha wanasiasa mbalimbali nchini

Dar es Salaam. Safari ya maridhiano inaendelea kuwakutanisha wanasiasa mbalimbali nchini, ambao aghalabu ilikuwa nadra kushuhudiwa pamoja katika miaka ya hivi karibuni.

Jana, Machi 28, 2023 kilifanyika kikao cha vyama wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kilichohudhuriwa na viongozi wa juu wa vyama hivyo wenye wabunge.

Mbali na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana, kikao hicho kiliwakutanisha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.

Wawili hao waliwahi kuwa pamoja katika uongozi wa chama cha Chadema, kabla ya baadaye Zitto kufutwa uanachama na kuanzisha chama kingine ambacho ni ACT Wazalendo.

Wakati Mbowe akiwa mwenyekiti wa Chadema, Zitto alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara, kabla ya kutimuliwa.

Jana baada ya kikao hicho, Zitto alichapisha picha aliyoshikana mkono na Mbowe katika ukurasa wake wa twitter na kuandika: “Ilikuwa ni faraja sana leo jioni kukutana na kaka yangu Freeman Mbowe, mwenyekiti wa taifa wa Chadema katika Kikao cha Wakuu wa Vyama Wanachama wa TCD.

“Tulikuwa na kikao kizuri kilichosheheni mawazo ya kuendeleza mageuzi ya kisiasa nchini. Nina furaha sana kwamba vyama vyote vya TCD sasa vinafanya kazi pamoja kuimarisha utamaduni wa majadiliano,” aliandika katika ukurasa wake huo.