Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MWIBA MDOGO -12

ILIPOISHIA JANA...

“...Mitego yake ukiiangalia vibaya utaiona ya kitoto, lakini imetegwa kwa akili kubwa sana, yataka utulivu wa hali ya juu,” alisema Maliki huku akifungua dirisha na kuchungulia nje. “Mkuu alitumia kama kuning’inia kutoka juu.”


ENDELEA...


“Muuaji ni mtu makini sana ambaye ana hesabu hatua zetu, tukitoa mguu yeye anakanyaga,” Chifu alisema.

“Lazima nimpe hongera zake, japo siamini anayefanya mauaji haya si huyo binti, bali mtu mwingine kabisa mwenye uzoefu na mauaji ya hesabu kali,” Queen aliongezea.

Wakiwa katikati ya mazungumzo Chifu Shila alikumbuka kukutana na Mtoto wa Marehemu.

“Jamani Mtoto wa Marehemu amepanga tuonane wakati huu ili tujue sababu ya yeye kufanya mauaji japokuwa inaonekana ni kisasi cha kuuliwa wazazi wake, pia kudhulumiwa pesa baada ya kuuza madini kwa kugawiana watu watano na mmoja kumtosa.

“Kuna imani tutajua sababu ya kifo cha baba na mama yake, pia uwezo mkubwa wa kijasusi ameupata wapi.”

Kabla ya uondoka alimpigia simu Mtoto wa Marehemu ambaye alipokea bila hofu yoyote ilionyesha anajiamini kupita kiasi kwa kuzungumza kwa kujiamini.

“Upo wapi binti yangu?”

“Nipo hapa ofisini mapokezi nakusubiri.”

“Sawa nakuja.”

“Vipi yupo wapi?” Maliki aliuliza.

“Yupo ofisini anatusubiri.”

“Mmh! Ni mtu wa aina gani anayejiamini kupita kiasi, natamani kumuona,” Queen alisema kwa shauku kuu.

Gari lilielekea makao makuu ya polisi, walitumia dakika kumi kufika.

Walipofika waliteremka na kuelekea ofisini, huku kila mmoja akiwa na shauku kumuona mgeni wao.

Walipofika mapokezi Chifu alishtuka kumuona binti yake ambaye alipotezana naye katika mazingira ya kutatanisha. Hakuwa binti yake wa kumzaa, bali rafiki kipenzi wa mwanaye Rashila ambaye kwa kipindi kile alikuwa mwanasheria wa kampuni ya mawasiliano.

Alishtuka kumuona amekaa pale lakini akili yake ilikuwa kwa mgeni wake, Mtoto wa Marehemu.

“We Diana mbona upo hapa, siku hizi upo Mwanza.”

“Ha..ha..pana..ba..” hakumalizia alikatwa kauli.

“Ni hivi mama, nina mazungumzo na mtu muhimu sana.”

“Ni ..mi...”

“Mama kwani kuna mtu umemfuata?”

“Ndiyo baba nimekufuata wewe.”

“Umejuaje nipo hapa, sasa ni hivi tuna muda mrefu wa kuzungumza tena kwa kituo uniambie nini kilichokutokea ukatoweka ghafla.”

“Ba..baa...”

“Diana nakuja,” alisema huku akielekea mapokezi kumuulizia mgeni wake.

Aliachana na Diana ili akamuone mgeni wake kisha amrudie wazungume kwa kituo.

Alipofika mapokezi alimuuliza binti aliyekuwa amevaa mavazi ya kijeshi.

“Mage kuna mgeni wangu tofauti na yule binti?”

“Hapana, yule ni mgeni wako anakusubiri Chifu.”

“Sawa,” alisema huku akitoa simu yake kumpigia Mtoto wa Marehemu simu ambayo iliita.

“Haloo...Haloo.”

Chifu alishangaa kumuona Diana akinyanyuka ameshika simu akimfuata.

“Ni mimi baba mgeni wako.”

“Diana, sio wewe, kuna binti mmoja anajiita mtoto wa marehemu.”

“Ni..ni...mi..,” Diana alipotaka kuzungumza Shila alimkatisha.

“Diana hebu subiri wewe tutazungumza, kuna mtu muhimu nataka kuonana naye kwanza ndiye aliyenitoa Dar kuja Mwanza.”

“Baba Mtoto wa Marehemu ni mimi.”

“Diana nipo kazini usilete utani, wewe huwezi kuwa Mtoto wa Marehemu.”

“Baba usichukulie kama mwanao kipenzi Diana bali Mtoto wa Marehemu muuaji anayejisalimisha kwako.”

“Hapana sio wewe Diana,” mkuu Shila alikataa katakata.

“Mkuu kwa nini tusiende kumsikiliza tutajua yeye au changa la macho,” Maliki alitoa wazo huku na yeye akiwa haamini binti mrembo kama yule kuwa muuaji na kusahau hata Queen naye mrembo lakini hatari.

“Hili changa la Macho huyu binti hawezi kuua hata nzi, namjua vizuri, nimemlea mwenyewe ana huruma sana.”

“Baba huruma iliisha baada ya mama kukaribia kufa na kunipa sababu ya yeye kuwa hospitali ya wagonjwa wa akili ambayo ilisababishwa na kukiona kifo cha baba chenye maumivu makali, ndiyo maana Balize nilimuua kwa kumchoma visu visivyo na idadi kama visu alivyomchoma baba yangu kupelekea mama yangu kuweweseka kila alipokumbuka tukio lile la kutisha lenye kuumiza kupelekea kuonekana mwendawazimu,” Diana alisema kwa uchungu mkubwa.

“Nakubali kwa shingo upande.”

Waliongozana kuelekea chumba maalumu cha mahojiano huku kila mmoja akimshangaa Diana, ambaye hakufanana na yaliyokuwa yakifanyika, wengi waliamini huenda kweli alifanyiwa unyama ule lakini muuaji siyo yeye.

Diana alikuwa amevalia vazi refu la heshima, uso wake aliupodoa na kuupaka wanja na kumfanya aonekane binti mrembo anayejiheshimu.

Baada ya kuingia kwenye chumba cha mahojiano, kila kitu kiliwekwa tayari kwa ajili ya mahojiano, ikiwemo video kamera mbele yake na kuambiwa ajiandae.

“Tunaomba ujiandae, hatutaki utani, kama sio wewe utueleze mapema tufanye kazi nyingine tuendelee kumtafuta muuaji.” Shila alisema kwa sauti isiyotaka masihara hata kidogo.

“Muuaji ni mimi, msinidharau kwa urembo wangu, nikibadilika hata Manka wa kwenye Operesheni Rwanda haniingii hata robo. Nimeamua kujisalimisha kwa ajili ya heshima ya baba yangu, bila hivyo ningewaua wote hakuna ambaye angenijua.”

“Haya mama anza kutueleza historia yako toka unazaliwa mpaka leo hii upo mbele yetu.”

“Kwanza kabla ya yote naomba niletewe chupa ya maji makubwa yawe ya baridi kiasi kwa vile nitakachokisema kitalichoma koo langu.

“Simulizi yangu imejaa maumivu na mateso kwa nini niishi kwa tabu, tena yatima, eti baba yangu walimtoa kafara ya damu ili wawe matajiri...kweli...kweli kazi kubwa aifanye yeye shukurani yake kumtoa kafara na kudhuluma haki yake japokuwa ilikuwa ya wizi.”

Kauli ya kafara ya damu ilimshtua Shila na kujikuta akiyakumbuka maneno ya marehemu Joseph kabla ya kufa juu ya kafara ya damu, kwa nini kafara ya damu. Ilibidi atulie kwani doti na doti za mazungumzo ya Joseph yanashabihiana na Diana.

“Siku zote mali ya haramu hugawiwa kihalali ili haramu ionekane ni halali, nimeishi maisha ya shida, nimebakwa nimeteswa nimevumilia maumivu, moyo wangu umekuwa unawaka moto toka kifo cha mama yangu cha mateso mazito...

“Yaani leo hii pesa za dhuluma za kutoa damu ya mtu wamekuwa matajiri wakubwa, wengine kujenga makanisa, misikiti na kuonekana watu wa maana mbele ya jamii, kumbe nyuma ya pazia ni mashetani wakubwa wanyonya damu.

“Yaani eti dereva hana haki, angeshikwa baba yangu wakati wa kuvusha ule mzigo nani angejitokeza kusema anahusika zaidi ya kumruka futi mia ha..ha..lafu wale mashetani wanaonekana malaika mbele ya macho ya watu baada ya kuitoa kafara damu ya baba yangu; inauma inauma.

“Mwanzo nilijua ilikuwa dhuluma kwa vile baba hakuwepo kwenye mpango wao zaidi ya kutumika kutoa mzigo mgodini na kuona hakuhusika sehemu kubwa kumbe, sivyo hivyo.

“Mama mpaka anakufa anajua baba alikufa kwa kuuawa kwa ajili ya dhuluma ya kupewa pesa kidogo kumbe sivyo. Vifo walivyokufa havifiki hata robo ya maumivu ya baba na mama yangu, kidogo maumivu yangetulia kama ningewakata viungo na kuwanywa supu si kuwaua vile, wamepata adhabu ndogo sana.”

Kila mmoja alimshangaa Diana, hakuwa yule binti mrembo aliyekuwa akizungumza kwa sauti tamu ya kasuku ambayo ilimshawishi mtu yeyote anayemuona kwa mara ya kwanza kumuona kama malaika ambaye hawezi hata kuua nzi.

Lakini uchungu, kuzungumza kwa hisia kali alibadilika kwa muda mfupi baada ya kutoa hijabu na kubakia kichwa wazi, mishipa ya damu kichwani na shingo ilikuwa imemsimama na macho kugeuka rangi kuwa mekundu kama simba jike mwenye hasira.

Uso wa Diana alionesha umejaa hasira kama kobra mwenye hasira aliyepandisha sumu na kuwa tayari kumshambulia adui yake. Hali aliyokuwa nayo ilibadili mtazamo wa kila moja kuamini Diana kageuka kiumbe kingine kabisa.

“Pole mwanangu, sasa mama najua umeumizwa, hebu teremsha jazba, shuka chini, zungumza kwa utulivu ili hata tukikupeleka mbele ya sheria uweze kupata haki yako,” Shila alisema kwa sauti ya chini ya upole.

“Baba, haki yangu nimeishaipata, pia sina haja ya kufungua kesi na mtu kwa vile mwenye pesa siku zote sheria ni yake. Hii kesi ningeipeleka polisi mwenye hatia ningekuwa mimi, ningefungwa au kunyongwa. Japo haipendezi nilichokifanya lakini niliamini uamuzi wangu ulikuwa sahihi.

Unaweza kufuatilia hadithi hii kupitia tovuti ya Mwananchi, pia Mwananchi Digital katika  Mtandao wa YouTube.


Itaendelea wiki ijayo