Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Khamis Kigwangala: Mbunge wa Jimbo la Nzega

Muktasari:

Dk Hamisi Andrea Kigwangalla alizaliwa Agosti 7, 1975 mkoani Kigoma, hivyo Agosti mwaka huu atafikisha umri wa miaka 40. Baba yake mzazi Nasser Kigwangalla alikuwa mfanyakazi wa benki na baadaye mwandishi wa habari, huku mama yake mzazi, Bagaile Lumola akiwa mwalimu na baadaye akaingia katika siasa ndani ya CCM.

Historia yake

Dk Hamisi Andrea Kigwangalla alizaliwa Agosti 7, 1975 mkoani Kigoma, hivyo Agosti mwaka huu atafikisha umri wa miaka 40. Baba yake mzazi Nasser Kigwangalla alikuwa mfanyakazi wa benki na baadaye mwandishi wa habari, huku mama yake mzazi, Bagaile Lumola akiwa mwalimu na baadaye akaingia katika siasa ndani ya CCM.

Baba na mama wa kijana huyu ni “Wanyamwezi” wa Tabora kwa asili, na kuzaliwa kwa ‘Kigwa’ mkoani Kigoma kulitokea kwa vile wazazi wake wote walikuwa waajiriwa huko.

Kigwangalla alitumia sehemu ya maisha yake ya utotoni katika maeneo ya Goweko na Mlimani yanayopatikana Wilaya ya Uyui mkoani Tabora na alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Kigoma kidato cha kwanza mpaka cha nne.

Baadaye alijiunga kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Shinyanga (Shy Bush) akichukua mchepuo wa PCB (Physics, Chemistry, Biology). Mwaka 1999 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alichukua masomo ya udaktari wa binadamu na alihitimu shahada yake mwaka 2004.

Watu waliosoma na Kigwangalla pale ‘Shybush’ na hata chuo kikuu, wanamtazama kama kijana wa Kitanzania mwenye juhudi, anayependa kujisomea, anayependa uongozi wa kujitolea na mwanamichezo mahiri.

Baada ya hapo Kigwangalla aliendelea na masomo ya juu zaidi katika Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge nchini Sweden ambako alisomea Shahada ya Uzamili ya Biashara (MBA). Pia, alijiunga katika Taasisi ya Karolinska ambako alisomea Shahada ya Uzamili ya Afya ya Jamii (MPH) “Public Health”. Taasisi zote hizi ziko nchini Sweden.

Baada ya kuhitimu masomo yake ya juu ughaibuni, Kigwangalla alirejea nchini na kuanza harakati za kazi za kujipatia kipato na kuendesha maisha ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wagonjwa kama daktari.

Alifanikiwa kuanzisha kampuni binafsi na kwa maoni yake ilimletea mafanikio makubwa ambayo yalisaidia katika safari yake nyingine, ambayo imekuwa ndoto yake ya muda mrefu – “safari ya kisiasa”. Kigwangalla ameoa na ana watoto wawili.

Mbio za ubunge

Kigwangalla ni mwana CCM tangu enzi za chipukizi alipokuwa shule ya msingi. Ni kati ya vijana waliokua na kulelewa na familia ambayo iliunga mkono chama hicho, hasa mama.

Wakati anaendelea na shughuli zake za ujasiriamali na kuongoza kampuni yake, aliamua kuweka nguvu za kisiasa katika Jimbo la Nzega, mahali alipokulia, na mwaka 2010 aliingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha kuusaka ubunge kupitia CCM.

Hakika, uamuzi wake wa kugombea ubunge katika jimbo hilo haukuonekana kama jambo la “mashiko” kwa wana CCM wa jimbo hilo. Kwanza, hakuwa anafahamika Nzega; pili, hakuwa chaguo la wana Nzega. Chaguo la wana Nzega lilikuwa Hussein Bashe, ambaye katika kura za maoni, alishinda na kuwaacha mbali mbunge aliyekuwa anamaliza muda wake Lucas Selelii huku Kigwangalla akishika nafasi ya tatu.

Vikao vya juu vya CCM vilipokutana Dodoma, tayari makundi ya ndani ya chama hicho yalikuwa yanashughulikiana na hivyo “kwa mizengwe ya hali ya juu” chama hicho kilimtosa Bashe. Aidha, CCM haikumchukua mshindi wa pili kwenye kura ya maoni yaani Seleli, kikamrukia mshindi wa tatu ambaye ni Kigwangalla.

Ni muhimu tukakumbushana kuwa Kigwangalla ni mtu mwenye bahati sana; kutoka kuwa mshindi wa tatu kwenye kura ya maoni ndani ya chama hadi kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho, kushinda ubunge katika mazingira ya kupingwa ndani ya chama na sasa kuwa mtangaza nia ya urais. Ni wanasiasa wachache sana wamepitia bahati kubwa kama hii.

Hadi ninapoandika uchambuzi huu, Kigwangalla ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Kijamii ambayo inafanya kazi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Mbio za urais

Kigwangalla aliingia katika orodha ya watangaza nia ya urais ndani ya CCM, Septemba 7, 2014 jijini Dar es Salaam. Alitoa hotuba ya kurasa 21 kwa vyombo vya habari akijieleza yeye ni nani, ametoka wapi na kwa nini anaitaka nafasi kubwa kabisa ya uongozi wa nchi.

Siku hiyo aliambatana na mke wake na watoto wake pamoja na wanafamilia wengine ili kuonyesha kuwa katika kuianza safari yake hiyo hayuko peke yake, kwani familia nzima inamuunga mkono.

Kigwangalla hajaonywa na chama chake kama wenzake sita na labda hiyo inatokana na aina ya mikakati yake ambayo haijavunja taratibu za chama hicho kikongwe.

Nguvu zake

Nguvu za Kigwangalla zinatokana na maarifa aliyopata katika elimu yake. Huyu ni kijana makini na mfuatiliaji wa kila jambo na hapendi kupitwa na lolote lile ambalo ana wasiwasi kama litamkwamisha au kuwakwamisha wengine mbeleni.

Shahada zake tatu za chuo kikuu ni moja ya mafanikio makubwa kwa kijana yeyote ambaye ana visheni pana siku za mbele. Elimu hii, akiichanganya na uzoefu wake katika ubunge anaweza kuwaeleza wana CCM kwamba yeye ni chaguo lao.

Ujana unaweza pia kuwa sababu muhimu kwake. Hatujui CCM itakuja na ‘gia’ gani katika uchaguzi huu, baada ya kukamilisha miaka 10 ya Rais Jakaya Kikwete. Mbinu inayoweza kutumika ni ya kutafuta mtu wa kizazi cha sasa na hilo likitokea itakipasa chama hicho kumfikiria yeye na vijana wengine walioomba ridhaa. Ujana ni silaha ambayo itamsaidia Kigwangalla pamoja na mambo mengine.

Nguvu nyingine ya Kigwangalla ni ung’ang’anizi. Kati ya vijana ambao hung’ang’ania jambo lao hadi liwe ni pamoja na Kigwangalla. Yeye mwenyewe anajitambua hivyo na anakumbuka enzi za nyuma akiwa shuleni ambavyo wenzake pia walimchukulia hivyo.

Faida ya uki-ng’ang’anizi ni mafanikio, lakini pia hasara yake huwa ni kung’angania hata yale ambayo hayapaswi kung’ang’aniwa. Viongozi ving’ang’anizi, mara zote, hufika mbali na huwa hawakati tamaa katika mipango yao hata wachekwe. Ndiyo maana pamoja na kujua kwamba Bashe ndiye ameiteka Nzega kiasi kile, bado alikwenda kuomba ridhaa na ikamletea bahati iliyompeleka bungeni. Asingekuwa king’ang’anizi na akaogopa vivuli vya Bashe na Selelii, hakika asingefika bungeni.

Udhaifu wake

Moja ya taswira za Kigwangalla na ambayo si salama kwake, ni majivuno. Kwa watu wanaomfahamu ni kijana anayejisikia sana na anadhani ni mwerevu kuliko watu wengine. Mfano, tulipokuwa katika Bunge Maalumu la Katiba, mara kadhaa, wabunge wenzake wa CCM na hata kundi la 201 walisikika wakimsema na ukiwauliza walikuwa wakisema ni; “mtu wa kujisikia”.

Inawezekana kabisa Kigwangalla akawa anatupiwa maneno yasiyo ya kweli, lakini masuala ya uongozi huathiriwa sana na mitazamo ya jamii juu ya kiongozi. Kama jamii inakuchukulia wewe si mtu msafi, basi jambo hilo ni hatari kwako. Kwa siasa za “nipe nikupe” ndani ya CCM mtu anayejisikia anakuwa na nafasi ndogo kwa sababu atashindwa kutimiza matakwa ya makundi ya chama hicho, ambacho kinajiendesha kwa siasa za kulipana hisani.

Udhaifu wake mwingine ni kutojijenga jimboni kwake Nzega. Siku chache baada ya yeye kukoswakoswa risasi katika harakati za kuwatetea wachimbaji wadogo wa Nzega, nilikuwa mjini Nzega. Nilipowauliza vijana juu ya mbunge wao huyo kijana walinijibu kuwa “…huyo ni wa wakubwa” na eti mbunge wa wana Nzega alipokonywa Dodoma.

Baadhi ya wana Nzega wanasisitiza kuwa Kigwangalla si mbunge wao wa moyoni jambo lenye maana kuwa hajajijenga kisiasa. Kama umekuwa mbunge na umeshindwa kujijenga jimboni mwako, huo ni udhaifu mkubwa sana ambao unakupunguzia alama za kuendelea na safari hiyo au ya juu zaidi.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?

Mambo mawili yanaweza kumfanya Kigwangalla apewe uzito na CCM. Jambo la kwanza ni elimu yake ambayo imechanganyika na utaalamu wa masuala ya biashara na kutibu binadamu. Nchi yoyote ile ingependa kuwa na rais ambaye moja ya sifa zake pia ni elimu nzuri, isiyo na mashaka mashaka na ambaye anaweza kutumia elimu na maarifa yake kulinufaisha taifa lake.

Kuongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ni sifa thabiti ambayo inamfanya Kigwangall awe na uzoefu wa kujivunia, ambao pengine raia na wanasiasa wengi hawataweza kuipitia. Uzoefu huu, japokuwa ni wa kawaida, una maana kubwa kwake katika safari yake hii.

Jambo la tatu, CCM inaweza kujikuta inahitaji mtu mwadilifu. Kigwangala hana rekodi ya kuwa kiongozi wa Serikali au ya kuwa mtendaji wa Serikali mwenye mamlaka makubwa. Jambo hilo linamfanya awe mbali na kashfa nyingi ambazo huwakumba watu wa namna hiyo. Kati ya wagombea urais wanaotajwa ndani ya CCM, huenda yeye ndiye anaweza kuwa miongoni mwa wasio na kashfa na jambo hili ni msingi mkubwa wa kuomba ridhaa.

Nini kinaweza kumwangusha?

Kukosa uzoefu na uongozi ndani ya chama chake ni jambo moja linaloweza kumwangusha kwenye mchujo wa urais. Ndani ya CCM, sifa hii ni muhimu na ukiikosa unapaswa walau kuwa na sifa nyingine zinazotajwa. Kwa bahati mbaya, Kigwangalla hana uzoefu wa kutosha wa uongozi wa ngazi ya juu ndani ya chama chake.

Vita ya urais ni jambo kubwa sana. Inataka maandalizi, utayari, historia ya muda mfupi au muda mrefu, rekodi mbalimbali n.k. Zaidi ya rekodi nzuri ya elimu pamoja na uongozi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kigwangalla hana rekodi nyingine kubwa ya masuala aliyoyasimamia katika nchi hii. Siyo kwa sababu hana uwezo wa kusimamia masuala hayo, la hasha! Ni kwa sababu aliingia katika siasa mwaka 2010, tena katika ngazi ya ubunge na miaka mitano baadaye anahitaji kuwa rais.

Pia, kukosa uzoefu wa uongozi serikalini ni tatizo lingine. Kigwangalla hakuwahi kufanya kazi serikalini kama mtu muhimu au kama kiongozi au mtendaji muhimu katika Serikali na kwa hivyo, hajashiriki ipasavyo katika “urasimu” wa Serikali na kujua nini kinaendelea ndani. Atakapopambanishwa na wenzake ataonekana kama chaguo la kubahatisha.

Sababu ya tatu inayoweza kumwangusha ni kukosa mvuto kwa vijana. Ikumbukwe kuwa ikiwa CCM itaamua kumsimamisha Rais kijana katika kinyang’anyiro cha mwaka huu, lengo litakuwa kusaka kura za vijana. Lakini CCM haiwezi tu kumweka kijana yeyote yule.

Kwa bahati mbaya, Kigwangalla hatazamwi vizuri na vijana wengi wa Tanzania na kipimo kidogo ni namna ambavyo vijana wengi wanamtolea maoni katika mitandao ya kijamii pale anapotoa maoni yake. Mara nyingi hupingwa na kusemwa vibaya. CCM itahitaji kura za urais na itahitaji kijana mwenye mvuto ikiwa itaamua kumweka kijana. Simwoni Kigwangalla katika “mvuto” huo unaoweza kuwashawishi wapiga kura.

Ukitaka kuwa rais kupitia chama chochote, lazima uwe unaungwa mkono vizuri katika chama chako, viongozi wenzako na watu wenye mamlaka katika vikao vya maamuzi. Upekuzi wangu umejiridhisha kuwa Kigwangalla hatajwi kabisa na viongozi mbalimbali wa chama chake na hata wanachama, linapokuja suala la kumfikiria katika nafasi hiyo nyeti. Kutoungwa mkono huku ndani ya chama ni sababu muhimu ya kutopitishwa kuwa mgombea.

Jambo la mwisho litakalomwangusha Kigwangalla ni kufanya mambo mengi peke yake na kukosa mtandao wa kutosha ndani ya CCM na wakati huo huo akiwa hana pesa za kutosha. Ndani ya CCM kama huna mtandao wa kutosha, waratibu wa kutosha na pesa za kutosha, urais unabakia ndotoni mwako na unaweza kuusaka milele.

Asipopitishwa (Mpango B)

Ninachokiona, Kigwangalla ametangaza safari ya urais huku akiwa hajui mbele kukoje. Namwona kama ni “parliamentary material” (anayefaa kwa ubunge) kuliko “Presidential Material” (anayefaa kwa urais) kwa wakati huu. Ikiwa hatachaguliwa kuipeperusha bendera ya urais, Kigwangalla atarudi kugombea ubunge japokuwa, hali ya kisiasa ndani ya CCM jimboni Nzega siyo nzuri.

Kigwangalla hadi sasa ana nafasi finyu sana ya kupenya kwenye tundu la kura ya maoni ndani ya CCM kusaka ubunge wa Nzega, kwa mara ya pili, achilia mbali mzigo mzito anaojipa wa kutaka kujitwisha urais.

Mpango wake mwingine unaweza ukawa kurudi chini na kuomba ridhaa ya uongozi ndani ya chama chake, kwa ngazi ya wilaya, mkoa au taifa na kujipanga kukitumikia chama hicho miaka mingine mitano, kuonyesha uwezo wake na kutumia fursa hiyo kuijua mifumo ya uendeshaji wa CCM, kuwa karibu na wanachama na kujiibua tena upya akitokea ndani ya chama kuomba ridhaa kubwa za kiserikali.

Hitimisho

Watu wenye historia ndefu duniani na ambao waliingia katika siasa na ndani ya muda mfupi wakakwaa ukubwa wa nchi ni pamoja na Rais Barack Obama wa Marekani. Obama alikuwa seneta na kisha akawa rais, lakini ukifuatilia utagundua ni Mmarekani mweusi aliyesimamia masuala makubwa sana nchini mwake tangu akiwa mwanafunzi wa sheria na hata ndani ya chama chake cha Democrat. Huenda Kigwangalla hana hata robo ya sifa za Obama kabla hajawa rais.

Ni vema muda mwingi anaotumia kusaka urais angeutumia kugeuza vichwa vya wana Nzega pamoja na wana CCM wenzake ili watathmini kazi aliyofanya kama mbunge na walau kumpa kipindi cha pili cha uongozi jimboni.

Ukiniambia nimpe alama rafiki yangu Kigwangalla, naweza kumpa alama chache sana kama uhakika wa kupenya vizingiti vya ndani ya CCM na kuteuliwa kukiwakilisha chama chake kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Hata hivyo, tunamtakia kila la heri katika kutimiza ndoto zake kisiasa.