Januari si mbali, maandalizi Afcon yaanze

Taifa Stars imefanikiwa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023), mashindano ambayo yanatarajiwa kufanyika Januari 2024, nchini Ivory Coast.

Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kufuzu kwa fainali hizi, baada ya ile ya kwanza ya 1980, kisha 2019 na sasa 2023. Hakika ni mafanikio mazuri kuona nasi tunaanza kuzoea kutinga katika mashindano haya.

Kutoka 1980 hadi 2019 ilikuwa miaka mingi, umri wa mtu mzima mwenye familia wa miaka 39, tofauti na kipindi ambacho kimepita tangu mashindano ya 2019 na sasa.

Kutoka 2019 hadi 2023 ni miaka minne, hii inaonyesha kuwa tupo katika mwendelezo mzuri wa kucheza mashindano haya, hali ambayo awali ilikuwa ni kazi kubwa kuona japo tukikaribia tu kucheza.

Mazoea ya kuingia katika mashindano haya yanaanza kujengeka kwa wachezaji wa Tanzania na tutaanza kuona ni lazima kwa Taifa letu kuwa kwenye mashindano haya makubwa Afrika.

Kazi kubwa iliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Wallace Karia, Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Adel Amrouche na wadau wote wa soka nchini imelipa.

Tunajivunia timu hii kwa sasa, kwani mitandao ya kijamii ilichafuka kwa taarifa za kufuzu kwa Taifa Stars mara baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa Alhamisi usiku, nchini Algeria.

Hii inaonyesha kuwa kila Mtanzania kwa nafasi yake aliiombea timu hii kwa ajili ya kufika hapa ilipo sasa, lakini kazi haijaishia hapa.

Tunajua kuwa kazi kubwa ilifanyika hadi kupatikana kwa nafasi hii ya kuwa kati ya timu 24 zitakazokuwa nchini Ivory Coast Januari mwakani, lakini kuna mambo mengi ya kufanya ili kufika huko na kuwa na ushiriki bora.

Hii ni mara ya tatu tunashiriki, hivyo tumeanza kuondoa ule woga wa mashindano, kwa maana hiyo tunatakiwa kuwa na maandalizi mazuri kuonyesha mataifa mengine kuwa hatuko kwenye mashindano hayo kwa ajili ya kushiriki kama misimu iliyopita.

Tunatakiwa kujiandaa zaidi kwa mechi ngumu za mashindano haya ambayo yanapeleka timu mbili zilizofuzu kutoka katika kila kundi.

Hiyo inamaanisha kwamba hakutakuwa na mchezo rahisi, kwani kila timu itakayokuwa Ivory Coast itakuwa imefuzu baada ya mapambano mazito na ilistahili kuwa hapo kwa ubora wake.

Tukiliangalia hilo, tunaweza kupata chachu ya kuanza maandalizi mapema, kwani Januari si mbali kutoka sasa, tunahitaji kujua mapema mpango wetu ni upi na lengo la mashindano kwetu nui lipi.

Tunaamini kuwa mpango uliotumika mwanzo kuhakikisha tunafuzu utakuwa mara mbili ya ule ambao tutautumia katika ushiriki wetu kwenye Afcon.

Bila shaka Karia na timu yake wanajua matamanio ya Watanzania, tunajua kuwa inaweza kuwa ngumu kutwaa ubingwa wa fainali hizo, lakini tunahitaji kuweka alama kwa mashindano ya sasa.

Tumeshaanza kuonekana kwenye mashindano na hata baadhi ya wachezaji wapo na timu hii kuanzia ile iliyofuzu 2019; hivyo ama baadhi ya viongozi au wachezaji wazoefu kuelekea kwenye fainali za msimu huu. Hawa wanajua cha kufanya, ushauri wetu ni kwamba wawezeshwe kwa kila wanachohitaji ili kuiweka timu yetu kwenye nafasi nzuri.