KONA YA WASTAAFU: Mstaafu anapoutaka Muungano usiomtaka!

Mstaafu wetu si mwanasiasa. Kazi hiyo ina wenyewe. Lakini kwa vile anaamini kuwa mbali ya yeye kuwa mwananchi na Muungano sio wa waheshimiwa tu bali na wananchi walioujenga, anaona anapaswa kulisemea na kulikemea baada ya kuona linataka kustaafishwa na waheshimiwa wa nchi hii kama alivyostaafishwa yeye bila kuheshimiwa wala kukumbukwa.


Mumsamehe kwa kuwa mwanasiasa, angalau kwa kona hii tu!

Aprili mwaka 64, miaka mingi iliyopita mstaafu wetu alikuwa dogo dogo wa miaka mitano tu wakati nchi hii ikisherehekea kuungana na nchi nyingine. Alikuwa hajaanza hata kuwa ‘denti’ wa shule na alikuwa yuko ‘shule ya vidudu’ ya wamisionari wa Kijerumani waliokuwa wanajenga hospitali kubwa kijijini kwa mstaafu milima ya Usambara.

Ndiyo, shule ya vidudu kwa watoto wadogo ambao hawajaanza shule rasmi ambayo nyinyi sasa mmeipandisha chati na kuuita Kindergaten, Academy, Fountain na kadhalika, kwa ada ya mamilioni ya shilingi ili watoto wenu wapate kuweka sawa akili zao kabla hawajakuwa ‘madenti’. Mstaafu wetu anasema wao waliziweka sawa akili zao bure bileshi. Na waliziweka sawa kweli!

Angalau bado mnawapa chati ‘wadudu’ hawa kwa kuwashirikisha kwenye maandamano ya siku ya wafanyakazi, May Day, wastaafu wakiachwa kwenye mataa kama hawahusiki, huku mkifikia hata kuwaapisha ‘wadudu’ kuwa ‘sungusungu’ wa kulinda usalama wa mkoa, kama ilivyofanyika kule Arusha. Haieleweki kwa nini wastaafu hawakaribishwi kwenye maandamano ya May Day, kana kwamba ukistaafu wewe sio mfanyakazi tena.

Mstaafu wetu akiwa na miaka mitano tu ni mmoja kati walioshangilia siku ya kuzaliwa Muungano, japo alikuwa bado hajui chochote au lolote kuhusu Muungano huo. Ni wazee na kaka zao wakubwa waliowafahamisha ‘shule ya vidudu’ hao maana ya Muungano kwamba pamoja na mambo mengine mengi, walikuwa wameungana na nchi nyingine iliyokuwa ni kisiwa karibu yetu kwa ajili ya usalama wao na wetu iwapo nchi hiyo itashambuliwa au kuingiliwa na maadui, huku ‘wanogesha stori’ wengine wa vijiwe vya kijijini vya wakati huo wakiwachanganya zaidi ‘shule ya vidudu hao kwa kuwaambia kwamba nchi tuliyoungana nayo zamani za kale ilikuwa moja na nchi yetu lakini ikamomonyolewa na kupelekwa mbali baharini hivyo tumerudiana tena.

Kwa vile 1964 hiyo wengi tulikuwa hatujui bahari wala kisiwa vilivyo, tukaishia kuchanganyikiwa zaidi na kung’aa macho tu, lakini tulisherehekea Muungano.

Mstaafu wetu anasema ndivyo walivyotambulishwa kwa Muungano na kuanzia hapo kila mwaka wakapata dezo ya siku moja ya kutokwenda shule wakiadhimisha Muungano, dezo ya siku moja kwenye miaka 40 yote ya ajira yake na dezo ya kudumu kwenye ustaafu wake wa hiari.

Naam. Mstaafu anasema wakabaki kuudumisha muungano wetu na kuanzia miaka ya 60, 70 na ya mwanzoni mwa 80 kukajengwa utamaduni wakati wa Pasaka wa kutembeleana watu wa Bara na wa Visiwani, Pasaka ya mwaka huu wale wa visiwani wanakuja huku Bara kushindana kwenye mpira na muziki, hasa ule wa taarabu asili, Pasaka ya mwaka unaofuata inakuwa zamu ya watu wa Dar kwenda visiwani kushindana. Ndipo tukazijua timu kama Vikokotoni ya Visiwani na Good Hope ya Temeke, Dar.

Mstaafu anasema ni 1974, miaka 50 iliyopita, ndipo baadhi walipoanza kushituka, kwamba Muungano wetu hauko kama unavyoonekana na hii ilitokana zaidi na ndugu zetu wa Visiwani kuwa na televisheni, tena ya rangi, na kuifanya nchi ya kwanza kabisa kwenye bara zima la Afrika kuwa na televisheni ya rangi, huku sisi ndugu zao wa Bara hatuna hata ya ‘Black and White’ (kama vile nyeusi na nyeupe sio rangi).

Ikawabidi wa Bara wangoje mpaka 1994, miaka 20 baadaye, ndipo televisheni ipige hodi kwao. Miaka 20, upande mmoja wa Muungano uwe na televisheni ya rangi Afrika nzima huku upande wa pili wa Muungano wenye watu wengi ukiwa hauna hata mitambo ya kuonyesha televisheni ya rangi ya ndugu zao wa Visiwani. Achilia mbali ‘tartan track’, uwanja maalumu wa kukimbilia, kwa wanamichezo wa Visiwani, huku wa Bara wakikimbilia lami au changarawe tu, mstaafu wetu naye akajiunga na wa Bara wengi walioanza kujiuliza mno kuhusu Muungano wetu.

Kwenye ajira sasa. Mstaafu sasa anaishia kushangaa tu kwamba mheshimiwa mkubwa wa Visiwani kila May Day lazima awape wafanyakazi wake nyongeza inayoeleweka. Mwaka jana alifanya hivyo na mwaka huu ameongeza posho inayoeleweka, sio asilimia bali ametamka wazi shilingi anazoongeza, huku hawa wa Bara mwaka jana wameishia ‘tuna jambo letu’ na hatimaye lilipotekelezwa asilimia iliyoongezwa haikuleta matumaini yaliyotegemewa na waajiriwa hao.

Mwaka huu tena waajiriwa wa Bara wameishia palepale pa mheshimiwa wetu kuagiza kwamba ‘tuna jambo letu’ kutegemea kwisha kwa vita ya Russia na Ukraine, sijui vinahusikaje hapo na havihusiki kwenye Siri-kali kutumia bilioni 5 kununulia magari waheshimiwa wake, wakiwaacha solemba wastaafu wake ambao wana miaka 19 sasa bila nyongeza ya pensheni yao, kama vile wao hawahusiki na May Day 19 zilizopita.

Mstaafu anasema tuujadili wazi Muungano wetu bila unafiki. Hawa vijana waliopewa jukumu la kuulinda Muungano wetu na kero zake wasije wakafika mahali wakaona hauna faida kwao na wakaamua kila mtu aondoke na mbao zake. Tutahadhari.