Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mifumo ya dijitali itapunguza rushwa kwa askari barabarani

Tatizo la rushwa miongoni mwa askari wa usalama barabarani na madereva limekuwa kikwazo kikubwa katika juhudi za kuboresha usalama na ufanisi wa usafiri nchini Tanzania. Ripoti maalumu iliyofanywa na gazeti la Mwananchi hivi karibuni imeibua hali ya ukubwa wa tatizo hili.

Rushwa siyo tu kwamba inaharibu uadilifu wa taasisi za umma, lakini pia inasababisha upotevu wa mapato ya Serikali na kuleta usumbufu kwa raia. Hata hivyo, matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaweza kuwa suluhisho la kudumu katika kupunguza rushwa kwa askari wa usalama barabarani.

Katika uchambuzi huu nitajadili kwa kiasi namna mifumo ya kidijitali inavyoweza kupunguza rushwa, kuongeza mapato ya Serikali, na kuboresha usimamizi wa sheria za barabarani, nikirejea kinachofanyika katika mataifa yaliyoendelea.

Kwanza mifumo ya kidijitali inapunguza rushwa kwa kupunguza mwingiliano wa moja kwa moja kati ya askari wa usalama barabarani na madereva. Kwa kutumia teknolojia kama kamera za barabarani na vifaa vya kurekodi video kwenye magari ya polisi, udhibiti wa sheria za barabarani unaweza kufanyika bila mawasiliano ya moja kwa moja.

Kamera hizi zinaweza kurekodi makosa yote ya barabarani kama vile mwendo kasi, kutovaa mikanda na kupita maeneo yasiyoruhusiwa. Picha na video hizi zinaweza kutumwa moja kwa moja kwenye kituo cha udhibiti wa trafiki, ambapo faini inaandikwa moja kwa moja kwa gari na dereva/mmiliki kujulishwa kwa njia ya simu.

Utaratibu huu unatumika katika mataifa mengi, unapunguza nafasi ya askari wa barabarani kudai rushwa kwa sababu hakuna mawasiliano ya ana kwa ana na madereva lakini pia nguvu kazi ya askari inaelekezwa katika maeneo mengine.

Pili matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaweza kupunguza gharama za uendeshaji kwa Serikali na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sheria za barabarani. Kwa mfano, tiketi za makosa zikitolewa kwa njia ya kidijitali, Serikali itapunguza gharama za uchapishaji wa faini za karatasi na kuajiri askari wengi wa barabarani.

Vilevile, mifumo ya kidijitali inaweza kusaidia katika kutambua na kuondoa madereva wenye rekodi mbaya za makosa ya barabarani, hivyo kuboresha usalama wa barabara kwa ujumla.

Tatu, mifumo ya kidijitali pia inaweza kuongeza uwajibikaji na uadilifu kwa askari wa usalama barabarani. Kwa kutumia teknolojia ya GPS na vifaa vya kufuatilia magari ya polisi, kituo cha udhibiti kinaweza kujua maeneo na shughuli za askari wakati wote.

Hii ina maana kwamba askari hawawezi tena kujihusisha na vitendo vya rushwa bila kugundulika. Aidha, taarifa zote za makosa na tiketi zinaweza kuhifadhiwa kwenye hifadhidata ya kidijitali, hivyo kutoa ushahidi wa wazi endapo kutakuwa na tuhuma za rushwa au ukiukwaji wa sheria.

Nne, matumizi ya mifumo ya kidijitali pia yanaweza kuongeza mapato ya Serikali kwa kuhakikisha ukusanyaji wa kodi na faini unafanyika kwa njia salama na ya uhakika. Mfumo wa kidijitali unaweza kufuatilia na kuhifadhi taarifa zote za malipo, hivyo kuzuia upotevu wa mapato unaosababishwa na rushwa.

Kwa mfano, dereva akipokea tiketi ya kidijitali, atalazimika kulipa faini hiyo kupitia njia za malipo ya kielektroniki kama vile M-Pesa, Tigo Pesa, au benki. Hii inamaanisha kuwa hakuna nafasi ya dereva kutoa pesa taslimu kwa askari ili kuepuka faini. Mapato yote yanakusanywa moja kwa moja na kuingizwa kwenye mfumo wa serikali, hivyo kuongeza uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Pamoja na hayo, ufungaji wa kamera za barabarani utasaidia kurekodi makosa yote ya barabarani kwa wakati halisi, hivyo kusaidia katika utoaji wa tiketi za makosa bila upendeleo.

Kamera hizi zinaweza kuwekwa kwenye maeneo yenye msongamano wa magari na barabara kuu ili kufuatilia mienendo ya madereva. Mbali na kamera, matumizi ya roboti katika usimamizi wa sheria za barabarani yanaweza kuongeza ufanisi.

Matumizi ya roboti katika uongozaji wa magari kama ilivyo kwa taa za barabarani zinaweza kusimamia sehemu za kupita kwa miguu, kuongoza trafiki, na hata kutoa tiketi kwa madereva wanaovunja sheria. Hii inapunguza kabisa nafasi ya rushwa kwa sababu roboti hazina hisia wala tamaa za kibinadamu.

Sasa kama kuna nia ya dhati kumaliza vitendo vya rushwa, Serikali na taasisi husika hawana budi kuwekeza katika mifumo ya kidijitali ili kuboresha usalama barabarani na kupambana na rushwa kwa ufanisi.

Mwandishi anapatikana kupitia barua pepe: [email protected]