Uchumi wa buluu fursa ya kuuaga umasikini

Dhana nzima ya uchumi wa buluu ni shughuli zote za uendelezaji na ukuzaji wa uchumi, kupitia matumizi bora ya rasilimali maji kama bahari, mito na maziwa.

Shughuli za msingi zinazofanywa katika rasilimali hizi ni kama vile uvuvi, usafirishaji, utafutaji na uchimbaji wa madini na mafuta.

Pia hujumuisha shughuli zote za utafiti majini, burudani na michezo kandokando mwa bahari, shughuli za bandari kwa upana wake ikiwamo ujenzi wa vyombo vya majini.

Nikigusia kwa uchache, rasilimali bahari imechukua zaidi ya asilimia 70 ya dunia, huku sehemu ndogo iliyobaki ikiwa ndio ardhi tunayoishi.

Hii inamaanisha kwamba sehemu kubwa ya dunia imezungukwa na utajiri lakini tumeshindwa kuutumia kwa sababu ya kukosa maarifa ya kutosha ya kuutumia utajiri huo ipasavyo.

 Dk Tumaini Gurumo, Mkuu wa Chuo cha Bahari jijini Dar es Salaam katika kitabu chake: ‘Uchumi wa Bluu” anasisitiza juu ya fursa zilizopo kwenye uchumi huo na kuwahakikishia Watanzania kuwa elimu ndogo tu juu ya ujasiriamali kwenye shughuli zilizopo kwenye uchumi huu, unaweza kutengeneza mamilioni ya fedha.

Nitoe mifano. Je, unafahamu kijana Gustav Magnar Witzøe ni tajiri watatu mdogo zaidi duniani kama inavyotajwa na jarida la Forbes 2018 anayekadiriwa kuwa na utajiri wa dola bilioni tatu Kimarekani. Huyu amewekeza kwenye sekta ya uvuvi.

Unafahamu kuwa kijana Abiodun Eniola kutoka nchini Nigeria alikuwa mmoja wa waathirika wa kukosa ajira baada ya kumaliza masomo ya elimu ya juu, lakini akaamua kuwekeza takribani kwenye uvuvi na sasa anavuna mamilioni ya fedha na haitaji tena kuajiriwa?

Kwa kifupi ni kwamba, mafanikio yoyote ya binadamu ama utajiri wa mali huanza kwenye fikra.

Ukiweza kutumia fikira yako vizuri ukaweza kupambanua mambo, lazima mafanikio yatakufuata. Kinyume chake, ufinyu wa fikra utakuletea umasikini na kuishia kulalama.

Fursa si lazima ipitie mlangoni, inaweza kupitia hata dirishani, hivyo ni jukumu lako kuifuata.

Sambamba na hilo kupata mafanikio makubwa, huenda pamoja na kujiamini, kuthubutu na kujituma.

Leo nakufungua fikra rasmi ya kuuga umasikini na kukubainishia kuwa utajiri unaoutamani, upo karibu yako.

Yumkini ni kilomita chache tu kutoka hapo ulipo kuufikia, kilichobakia ni kufanya maamuzi na kunufaika nao.

Uchumi wa bluu ndio suluhisho la umasikini. Leo nitagusia kwa kina fursa ya ufugaji ama uvuvi wa samaki unavyoweza kubadilisha maisha yako.

Mathalani, kupitia ufugaji wa matango bahari au majongoo bahari, unaweza kutengeneza hadi Sh 18 milioni kwa kilo 100 tu.

Kwa sasa kilo moja ya majongoo bahari inafikia Sh180,000. Moja ya sifa ya majongoo hawa hawahitaji chakula cha gharama kabisa, kwa kuwa wanafyonza mchanga wa bahari ambacho ndio chakula chao.

Jongoo huyu anachukua muda wa miezi minane hadi 12 kukua na kuvunwa. Soko lake ni kubwa mno ndani na nje ya nchi.

Fursa nyingine ni kilimo cha mwani mnene na mwembamba ambao unastawi ukanda wote wa Bahari ya Hindi.

Pia uvuvi wa kamba miti na kamba kochi, pweza, ngisi, kaa, unaweza kutoa faida kubwa na haraka sababu soko lake ni la uhakika nje na ndani ya nchi.

Swali linakuja unawezaje kutumia fursa hii adhimu? Serikali imelipa uzito suala hili na kuwawezesha kwa kutoa huduma ya mikopo, kupunguza bei ya leseni na kutoa maeneo kwa ajili ya ufugaji wa samaki.

 Serikali ya awamu ya sita kupitia programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi (AFDP), imetenga takribani Sh29 bilioni mwaka 2022/2023 kwa ajili ya kuwezesha kiuchumi shughuli za uvuvi na mikopo kwa wananchi waliopo kwenye sekta hiyo pamoja na kukuza pato la Taifa ikijumuisha makundi ya vijana, kinamama na Watanzania wote wenye kutaka kufanya kazi ya uzalishaji mali kupitia fursa ya uchumi wa bluu.

Baadhi mifano michache ya vijana wenye uthubutu na wenye nia ya dhati ya kuuaga umasikini, wameanza kufaidika na mikopo hii inayotolewa na Serikali vikiwemo vikundi vya Catfish na Chapakazi ambavyo vilipata mkopo wao kupitia Halmashauri ya wilaya ya Ilemela.

 Vinatarajia kuvuna tani 16 za samaki wenye thamani ya Sh80 milioni kutoka katika kila kizimba kimoja tu cha samaki. Je, wewe kijana, mama, baba mwenye ndoto ya mafanikio, unasubiri nini kuchangamkia fursa hii?