Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wake za vigogo kulipwa mafao moja ya miswada mibaya kuwahi kutokea

Mbunge wa Mchinga, Mama Salma Kikwete, aliposimama bungeni mwaka jana na kushauri itungwe sheria ya mafao kwa wenza wa viongozi wakuu, wengi waliona kama anatania.

Wiki iliyopita wengi wamejua kauli ile ya Mama Salma haikuwa ya kuchangamsha Bunge tu, bali ilidhamiria kweli kuona watu wa aina yake wanapata mafao. Mtu unaweza kujiuliza, yeye na wenzake wamekutana na dhiki gani kiasi cha kuona sasa watengewe fungu maalumu kisheria?

Mama Salma anaelekea kufanikiwa baada ya watawala kupeleka muswada bungeni wakipendekeza [wakitaka], pamoja na mambo mengine, itungwe sheria kuhakikisha wake au waume wa viongozi wakuu wa nchi wanaendelea kufaidi hata baada ya wenza wao kuondoka madarakani na duniani.

Hiki kinachokusudiwa kufanywa na wabunge ni nyongeza tu kwenye sheria hiyo hiyo ambayo kwa kutumia fedha za umma, viongozi wakuu - rais, makamu wa rais na waziri mkuu - wanapostaafu wanatakiwa wajengewe nyumba za kuishi.

Kitu chochote ili kipate uhalali, lazima kuwe na maswali na majibu ya kuridhisha. Mfano, haya mafao kwa wenza yanalenga nini? Wenza wa rais, makamu wa rais na waziri mkuu mbona wanapata huduma zote? Mbona wana watumishi wote? Haya mafao ni kwa ajili ya nini? Ni asante kwa kuolewa au kuoa? Wamepungukiwa nini hasa hadi wapewe mafao asilimia 25?

Tunataka kufanya haya kwa sababu eti nchi kama Kenya au Namibia wenza wanalipwa mishahara na mafao. Kwa nini tanapinga? Kwanza, tunapinga kwa sababu sisi si hao wa mataifa mengine. Wananchi wanahoji kwa sababu si kila kinachofanywa katika mataifa mengine, basi nasi sharti tukiige hata kama hakina maana.

Wananchi wanapiga kelele kwa sababu uchumi wa nchi haujatoa ziada ya kuwezesha baadhi ya watu kufaidi mema ya nchi kuliko wengine. Wakinyamaza kwa hili, kuna siku watawala wataamua hata mishahara yao ifanane na ya Marekani, Uarabuni au kwingineko kwenye ukwasi.

Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na wakuu wengine katika dola ni watumishi wa umma. Ni waajiriwa. Kama ni waajiriwa, maana yake wanalipwa mishahara na stahiki nyingine za kisheria na zilizo nje ya sheria. Hakuna anayefanya kazi bure ili iwe sababu ya sisi kumuonea huruma kumsaidia yeye na familia yake pindi akiondoka madarakani. Muuza genge anajenga nyumba kwa fedha za genge, mke au mume wa rais anashindwaje kuishi au kujenga kutokana na fursa za kuishi ‘bure?’

Nchi hii ina maskini wengi wanaotaabika. Kuna watu hawana hakika ya kupata mlo wa siku. Wapo wasio na hakika ya matibabu na huduma nyingine za kijamii. Katika nchi yenye watu wengi wa aina hiyo, ni dharau na kejeli kuona wakubwa wakiwaza kulindana na kuifaidi nchi kwa kiwango kilichokusudiwa sasa.

Kama maisha ya wengi yangekuwa mazuri, hizi kelele za kulipana mafao zisingekuwapo. Kelele zinapigwa kwa sababu wananchi wanaona wananyonywa.

Mke au mume wa rais, makamu wa rais, au waziri mkuu, ukiacha masuala ya kawaida ya kifamilia, hana suluba zozote za kiuchumi zinazomkabili. Hajui malipo ya LUKU, chakula, suti, saluni au mvinyo. Hajui bei za mitumba, wala habahatishi matibabu ya miti shamba inayouzwa mitaani ambayo makabwela wengi kwa kukosa uchumi imara wanaitumia.

Hakuna rais, makamu wa rais, au waziri mkuu anayeshika wadhifa huo akiwa anaishi katika nyumba ya kupanga. Tanzania hatujampata, labda wale wa awamu ya kwanza waliokamatwa na Azimio la Arusha. Baada ya Azimio la Zanzibar hatuna kiongozi lofa wa mali. Hawa kuwajengea nyumba nyingine ilhali tayari walishakuwa nazo ni utapanyaji wa fedha za umma.

Tuangalie hali za watu wengine waliolitumikia taifa kwa nguvu, akili na mioyo yao yote - wana hali gani. Tunao wastaafu wa kuanzia mwaka 1998 kurudi nyuma pensheni yao ni Sh 100,000 kwa mwezi. Kuna majenerali waliostaafu kabla ya mwaka huo wanapokea Sh 100,000. Kuna maprofesa wanalipwa Sh 100,000 kwa mwezi. Wengi wanaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu na wasamaria wema. Wanatia huruma kweli kweli.

Kuna walimu wastaafu wanaohangaikia malipo ya Sh 100,000 kwa mwezi. Hawa ndio wametumika kuiandaa Tanzania ya wasomi tunaowaona leo, lakini thamani yao haitambuliwi. Tunao wakulima walioanza kulima wakiwa hawajabarehe au kuvunja ungo, lakini leo wamezeeka na kuchakazwa kwa dhiki. Wanaishi kwenye mabanda mabovu - mvua na jua - vyote vikiwa vyao.

Watu wa aina hii wenye mchango mkubwa kwa jamii na nchi wanaachwa waishi kwa shida kiasi hicho, badala yake tunaona wenza wa wanasiasa ndio muhimu. Hii si haki.

Tuchukue mfano halisi wa aliyeasisi wazo hili la mafao kwa wenza. Ana shida gani kuanzia mahali pa kulala, mlo, matibabu, usafiri na huduma nyingine za kibinadamu? Nani mwenye dhiki ya kupindukia katika familia za wanasiasa wakuu waliostaafu?

Kama washauri wa Rais wetu wangekuwa na nia njema, wasingeruhusu hili jambo likawa nyongeza kwenye mambo yanayoihangaisha serikali kwa sasa. Wasingeketi na kushereheka wakiona rais akisemwa vibaya mitaani.

Tujifunze kwa watu makini waliozipenda nchi na wananchi wao. Yupo Lee Kuan Yew - huyu alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Singapore na kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo, alikuwa na msimamo mkali kuhusu mafao kwa viongozi wa kisiasa. Alikuwa maarufu kwa kusimamia uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kwa kujitolea kwa kiasi kikubwa kwa utumishi wake wa umma bila kulipwa mafao makubwa.

Lee Kuan Yew alisisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kuwa na dhamira ya kuwatumikia wananchi wao na kuhakikisha kuwa wanajitolea kwa nia njema. Aliamini kuwa viongozi wa umma wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kujitolea kwa dhati kwa ustawi wa nchi yao. Kwa sababu hiyo, alipunguza mafao ya viongozi wa kisiasa na akasisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwa na motisha ya kuwatumikia wananchi wao kwa kujitolea zaidi.

Msimamo wake kuhusu suala hili uliakisi dhana ya kuweka masilahi ya umma mbele na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma. Lee Kuan Yew alikuwa na mtazamo wa kipekee kuhusu uongozi wa umma na jinsi viongozi wanavyopaswa kuonyesha dhamira yao ya dhati katika kuwahudumia wananchi wao.

Hivyo basi, ili kuhalalisha muswada huu kuwa sheria, tufanye mambo kadhaa. Mosi, tujiridhishe kama kweli wenza wa viongozi wakuu wastaafu wanakabiliwa na hali ngumu za kijamii na kiuchumi baada ya mume au mke kustaafu.

Pili, nchi maskini zinaweza kuwa na rasilimali za kifedha chache, na katika hali kama hii, kutoa mafao kwa wenza wa viongozi wakuu wastaafu kunaweza kusababisha mzigo mkubwa kwa hazina ya taifa. Kutajenga chuki miongoni mwa makundi ya wananchi ya walionacho na wasionacho.

Tatu, ni muhimu kusikiliza maoni ya wananchi na kufanya uamuzi unaozingatia hisia za watu. Kupitisha muswada kama huu kibabe au kwa jeuri tu ya kuwa wao ni watawala, kunawafanya wananchi wapunguze imani kwa viongozi wao. Kama kweli wabunge ni wawakilishi wa wananchi, na wanachokwenda kufanya bungeni huwa wametumwa na wananchi, basi waanzie kwa wananchi wawaulize kama wanaridhia huu ubaguzi unaokusudiwa kufanywa kupitia Bunge.

Nashauri muswada usitishwe. Usipitishwe kuwa sheria ya kutumika kwenye jamii ambayo watu wengi wanaishi katika dhiki. Kama ni lazima upitishwe, basi upanuliwe zaidi ili wazee wote wa nchi hii walipwe pensheni.

Nashauri viongozi wasome alama za nyakati. Wananchi wasipimwe imani kwa kupelekewa mambo yanayowakera. Wananchi wana haki na wajibu wa kuhoji, na hata kupinga wanayoona hayana faida kwa taifa.

Kuwa mwanasiasa hakumfanyi mtu kuwa na mahitaji zaidi ya kibinadamu kuliko mkulima, mfagizi, dereva wa bodaboda au mtu mwingine yeyote. Rasilimali za nchi sharti zitumiwe kwa usawa badala ya kundi la wachache kujiona wanayo haki ya kuzifaidi wao peke yao.

Tukiona Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakabiliwa na ukinzani mitaani, au serikali inasemwa vibaya, jueni miswada ya aina hii inachangia; maana katika hali ya kawaida unajiuliza, muswada huu una faida gani kwa umma?