Wizi katika benki nchini unatisha, haukubaliki

kamanda ,Suleiman Kova.PICHA|MAKTABA
Muktasari:
Tunahoji kama polisi wanajua ni jinsi gani matukio hayo yanavyoratibiwa, mbinu zipi wahalifu wanatumia kupata taarifa muhimu za benki, zikiwamo za kuwajua watunza funguo za vyumba vya kuhifadhia fedha (au kiasi cha fedha kinachoingia benki katika siku husika na kama hawajui wamefanya nini kujua mbinu hizo na kuzidhibiti?
Kwa mara nyingine sekta ya fedha nchini, hususan benki, imeshuhudia tukio jingine la wizi wa fedha katika baada ya majambazi kupora fedha juzi jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo limekuja baada wizi mwingine kutokea sehemu kadhaa, hasa jijini Dar es Salaam kuanzia mwaka jana. Hakuna shaka, kama ilivyokuwa katika matukio ya awali, kiasi kikubwa cha fedha, ambazo ni amana, akiba za wateja au mali ya benki husika, zitakuwa zimeibwa.
Ni jambo la kusikitisha kuona matukio haya yakiendelea kutokea wakati huu ambao tulidhani benki au taasisi za fedha ndiko mahali salama pa wananchi au wateja wengi kutunza fedha zao.
Inashangaza kuona matukio haya yakitokea mchana kweupe na yamekuwa yakihusisha watu ambao huingia kirahisi katika maeneo ya benki, wengine wakiwa katika sare zinazofanana na zile za vyombo vyetu vya ulinzi, na wanawezaje kutoweka na magari katika mji kama huu wenye msongamano mkubwa. Tunasikitika kuona vitendo hivi vikiendelea licha ya kuhakikishiwa na Jeshi la Polisi, Kanda ya Polisi Dar es Salaam mwaka jana kuwa benki zilizopo jijini humo zitapewa ulinzi na askari polisi ili kuzuia wimbi la matukio ya ujambazi.
Kauli ya kamanda wake, Suleiman Kova kuwa kuna mtandao wa wizi unaohusisha baadhi ya watumishi wa benki hizo wasio waaminifu na kwamba ajira ziangaliwe upya, si ya kupuuzwa, sanjari na kuangalia ni jinsi gani wahalifu wanavyopata sare za polisi au vyombo vingine vya dola.
Kamishna Kova alikiri mwaka jana kuwa jeshi hilo limebaini ujambazi huo unafanyika kupitia mtandao wa wafanyakazi ambao hushirikiana na baadhi ya walinzi wa kampuni binafsi za ulinzi. Tunahoji ni hatua gani zimechukuliwa ili kuzuia matukio hayo?
Tunahoji kama polisi wanajua ni jinsi gani matukio hayo yanavyoratibiwa, mbinu zipi wahalifu wanatumia kupata taarifa muhimu za benki, zikiwamo za kuwajua watunza funguo za vyumba vya kuhifadhia fedha (au kiasi cha fedha kinachoingia benki katika siku husika na kama hawajui wamefanya nini kujua mbinu hizo na kuzidhibiti?
Tunajiuliza, je, liko wapi jukumu la msingi la polisi la kulinda maisha ya watu na mali zao kama majambazi wanaendelea kuvamia na kupora fedha kama ilivyotokea juzi jijini Dar es Salaam?
Pia, tunahoji, je, benki zinafuata kwa kiasi gani utaratibu uliowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuhakikisha siri zao (benki) hazivuji kirahisi kwa wahalifu kama ilivyo sasa?
Tunafahamu, BoT ndiyo mdhibiti mkuu wa taasisi za fedha nchini na imeweka kanuni zinazotaka wamiliki wa benki kuhakikisha suala la ulinzi linafanyika. Kwa nini wizi unazidi kutokea? Je, ni nini uhusiano baina ya vyombo vya ulinzi na usalama na unazingatiwa kwa kiasi gani na pande zote zinazohusika?
Tunajiuliza, ni kasoro zipi zilizoacha benki zikashindwa kujifunza kutokana na matukio hayo ya ujambazi yanayoongezeka? Je, ni wapi kuna udhaifu na kwa nini pande husika zishindwe kuweka mikakati ya kutosha katika kuzuia wizi huo?
Tunaishauri BoT izinduke katika kusimamia kwa umakini wa suala hili ili kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi za fedha vinatimiza wajibu wao ipasavyo.
BoT haina budi kusimama ipasavyo ili kuondoa udhaifu unaotoa mwanya kwa matukio ya uzembe yanayochochea uporaji na wizi kuendelea. kwenye benki zetu kwa kasi kiasi kikubwa.