Ashley Young, mwanawe kuweka rekodi mpya England leo
Liverpool, England. Leo usiku huenda ikatimia ndoto ya Ashley Young na mwanawe Tyler Young ya kuweka rekodi ya kucheza timu tofauti katika mechi moja pale Everton itakapokutana na Peterborough United kwenye michuano ya Kombe la FA.
Historia inaonyesha hakuna hata mwaka mmoja ambapo baba na mwana wamewahi kucheza dhidi ya kila mmoja katika miaka 154 ya mashindano hayo, lakini hilo linatarajiwa kubadilika kwenye mechi hii ya raundi ya tatu itakayochezwa Uwanja wa Goodison Park kuanzia saa 4:45 usiku.
Ashley, mwenye umri wa miaka 39, alitoa maoni muda mfupi baada ya droo iliyochezeshwa kuonyesha Everton inakutana na timu hiyo anayoichezea mwanawe mwenye umri wa miaka 18 inayoshiriki League One akisema anaisubiri kwa hamu siku hii ifike.
Hata hivyo, kutimia kwa ndoto na rekodi hii kutategemea na uamuzi wa kocha wa Peterborough, Darren Ferguson, ambaye ni mtoto wa Sir Alex Ferguson.
"Tyler atakuwa benchi lakini siwezi kuhakikisha kuwa atacheza," alisema Darren katika mkutano na waandishi wa habari jana na kuongeza.
"Nafikiri mwelekeo wa mchezo ndio utaamua hilo. Yeye ni kijana mwenye kipaji. Anaweza kuchukua mfano wa baba yake ambaye bado anacheza akiwa karibu na miaka 40. Kufanya hivyo, unahitaji kuwa na bidii kila siku."
Ashley Young ni mmoja kati ya mastaa wenye historia kubwa katika soka la England akicheza kwa mafanikio zaidi akiwa na Manchester United kabla ya kwenda Inter Milan, kisha Astona Villa na sasa Everton. Pia alikuwa sehemu ya timu ya England iliyofika nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018.
Wakati hayo yakisubiriwa, kwa upande mwingine imewahi kushuhudiwa baba na mwana wakicheza pamoja katia timu moja.
Mwaka 2014 katika kikosi cha Mogi Mirim huko Brazil, mkongwe Rivaldo wakati akiwa na miaka 41, alicheza sambamba na mwanawe, Rivaldinho aliyekuwa na miaka 18.
Wengine ni George Eastham Sr na George Eastham Jr (Ards FC mwaka 1954), wakati Alexei Eremenko Sr akifanikiwa kucheza na wanawe wawili, kwanza Alexei Eremenko Jr katika kikosi cha HJK Helsinki mwaka 2003, kisha Roman Eremenko mwaka 2004 katika kikosi cha FF Jaro.