Dakika 90 za kihistoria Twiga Stars
Lome,Togo. Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ leo inahitaji matokeo ya aina tatu dhidi ya wenyeji wao Togo ili ifuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) zitakazofanyika mwakani huko Morocco.
Ushindi wa mabao 3-0 ilioupata katika mechi ya kwanza nyumbani Alhamisi iliyopita unaifanya Twiga Stars ihitaji ushindi, sare au kupoteza kwa mabao yasiyozidi mawili ili itinge WAFCON.
Ikifuzu itamaliza kiu ambayo imekuwa nayo kwa miaka 13 ya kutamani kushiriki fainali hizo tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 2010 iliposhiriki fainali zilizofanyika Afrika Kusini na kushika mkia.
Baada ya hapo, Twiga Stars haijashiriki fainali za WAFCON kwa awamu tano mfululizo na mara kwa mara ilikuwa ikiishia katika raundi ya kwanza ya mashindano ya kufuzu ikikwama mbele ya Zambia, Namibia, Zimbabwe na Ethiopia.
Twiga Stars inaivaa Togo ikiwa katika nyakati bora zaidi ambayo ni kufanikiwa kutinga katika raundi ya tatu ya mashindano ya kuwania kufuzu Michezo ya Olimpiki mwakani na imepangwa kukutana na Afrika Kusini.
Opa Clement anayecheza soka la kulipwa katika Ligi Kuu ya Uturuki akiitumikia Besiktas, ndio tegemeo kubwa la Twiga Stars katika safu yake ya ushambuliaji leo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufumania nyavu ambao amekuwa nao.
Nyota huyo ambaye pia ndiye nahodha wa Twiga Stars, alikuwa chachu ya mafanikio ya timu hiyo katika mechi ya kwanza nyumbani akifunga mabao mawili huku akisababisha lingine ambalo Togo walijifunga.
Nyota wengine wa ushambuliaji ambao ni tegemeo la Twiga Stars leo ni Enekia Kasonga anayeitumikia Eastern Flames ya Saudi Arabia na Aisha Masaka ambaye anaichezea BK Hacken ya Sweden.
Masaka anapita katika nyakati bora kwa sasa na ametoka kucheza mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa Wanawake dhidi ya Paris FC na Real Madrid.
Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime alisema “Tuna dakika 90 mpya ugenini dhidi ya Togo ambazo tunaamini zitakuwa ngumu kwa vile tunakutana na timu bora na ngumu. Tumefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi hii.”