Gomes aleta sapraizi Dar, kosi lake hili hapa

Muktasari:

  • SIMBA tayari wapo kwenye ardhi ya Dar es Salaam. Walifanya mazoezi ya mwisho jana Jumamosi, Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao watautumia kwa ajili ya mechi kimataifa ya kirafiki na TP Mazembe. Lakini kuna sapraizi inakuja kutoka kwa Kocha wa makombe, Didier Gomes.


SIMBA tayari wapo kwenye ardhi ya Dar es Salaam. Walifanya mazoezi ya mwisho jana Jumamosi, Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao watautumia kwa ajili ya mechi kimataifa ya kirafiki na TP Mazembe. Lakini kuna sapraizi inakuja kutoka kwa Kocha wa makombe, Didier Gomes.

Kulingana na aina ya mazoezi aliyowafanyisha mastaa wake Morocco na Arusha wataingia katika mechi na TP Mazembe na mfumo mpya kabisa wa 3-5-2, ambao tangu Gomes amechukua mikoba ya kiufundisha timu hiyo mwaka jana hakuwahi kuutumia. Ni mfumo ambao kitaalamu timu inaupiga mwingi sana.

Gomes amekuwa akitumia mifumo mitatu ambayo ni (4-2-3-1, 4-3-3 na 4-4-2).

Mfumo wa 3-5-2, ni mabeki wa kati wataanza watatu, viungo watano ambao asilia watakuwa watatu pamoja na mabeki wa pembeni watakuwa katika eneo hilo huku washambuliaji watakuwa wawili.

Kikosi ambacho kitaanza kipa, Aishi Manula mabeki watatu wa kati Pascal Wawa, Joash Onyango na Erasto Nyoni, viungo watano, Jonas Mkude, Sadio Kanoute, Pape Ousmane Sakho, Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Washambuliaji wawili wataanza, Morrison aliyefunga bao katika mechi ya kirafiki iliyopita dhidi ya Aigle Noir pamoja na Chris Mugalu ambaye amekuwa akifanya vizuri kwenye mazoezi ya kufunga.

ADVERTISEMENT
Mfumo huu kwa mara ya kwanza unafundishwa au kutumiwa ndani ya kikosi cha Simba ilikuwa mwaka 2018, wakati huo kikosi hicho kikinolewa na kocha, Mfaransa Pierre Lechantre.

Gomes alisema anaimani kubwa na kila mchezaji kutokana na kujituma, kutimiza majukumu yake kila anapokuwa uwanjani pamoja na programu nyingine ambayo huwapatia.

“Wachezaji wote wapo na morali nzuri hawa wapya na waliokuwepo msimu uliopita wameonyesha kuwa na vipaji vikubwa zaidi hiyo matumaini yangu makubwa msimu ujao tutakuwa na kikosi bora zaidi,” alisema Gomes na kuongeza;

“Ushindani ndani ya kikosi umekuwa mkubwa mno si wale wachezaji wapya au tuliomaliza nao msimu kila mmoja anafanya kila kilicho bora ili aaminiwe na kupewa nafasi zaidi jambo ambalo ni zuri kwetu katika suala la kuandaa timu pamoja na ufundi.”