Kinachoisubiri Madrid UEFA hiki hapa

Muktasari:
- Baada ya mechi dhidi ya Atalanta, Madrid itabakiza michezo miwili ambapo Januari 22, 2024 itakuwa nyumbani dhidi ya RB Salzburg huku Januari 29, 2024 itacheza ugenini dhidi ya Brest.
Atalanta, Italia. Ligi ya Mabingwa Ulaya itaendelea tena leo Desemba 10, 2024 ambapo viwanja tisa vitakuwa vikitimua vumbi huku Mabingwa watetezi Real Madrid baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo watakuwa ugenini dhidi ya Atalanta.
Madrid inaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa ambapo ilifungwa mabao 3-1 ikiwa nyumbani dhidi ya AC Milan na mchezo uliofuata ilikubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield.
Kocha wa Madrid Carlo Ancelotti, ana kibarua kigumu cha kuhakikisha mabingwa hao wa msimu uliopita wanapata matokeo mazuri ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa ambapo Madrid inashika nafasi ya 24 ikiwa na pointi sita katika mechi tano walizocheza huku ikibakiza michezo mitatu ya kumaliza hatua ya makundi.
Endapo Madrid itashindwa kupata matokeo mazuri kwenye michezo mitatu iliyosalia inaweza kushindwa kufuzu katika hatua ya mtoano itakayohusisha timu 16 zilizomaliza nafasi ya tisa hadi 24 na timu nane zitakazopatikana zitaungana na zile timu nane zilizomaliza nafasi za juu kucheza hatua nyingine ya mtoano.
Atalanta inayoongozwa na kocha Gian Piero, imejiweka katika nafasi nzuri baada ya kupata ushindi kwenye mechi tatu huku ikitoa sare mechi mbili ambapo inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 11.
Baada ya mechi dhidi ya Atalanta, Madrid itabakiza michezo miwili ambapo Januari 22, 2024 itakuwa nyumbani dhidi ya RB Salzburg huku Januari 29, 2024 itacheza ugenini dhidi ya Brest.
Mechi nyingine za leo
Girona vs Liverpool
Dinamo Zagreb vs Celtic
Atalanta vs Real Madrid
Bayer Leverkusen vs Inter Milan
Club Brugge vs Sporting CP
Salzburg vs Paris Saint-Germain
Shakhtar Donetsk vs Bayern Munich
RB Leipzig vs Aston Villa
Brest vs PSV Eindhoven