Salah na Liverpool sasa mambo safi

Muktasari:
- Vilevile kiujumla tangu ajiunge nao amefunga mabao 226 katika mechi 370 za michuano yote.
Liverpool, England. Baada ya mazungumzo ya muda, ripoti kutoka tovuti ya The Mirror zinadai mabosi wa Liverpool wamefikia makubaliano na wawakilishi wa Mohamed Salah kuhusu mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Kwa muda mrefu kulikuwa na uvumi kwamba staa huyu huenda akaondoka mwisho wa msimu kwani haikuonekana dalili ya kusaini dili jipya licha ya kubakisha miezi tu kabla ya mkataba wa sasa kumalizika.
Taarifa zinaeleza Salah atasaini mkataba wa miaka miwili kubakia Anfield ikiwa ni pungufu ya mwaka mmoja kutoka miaka mitatu aliyohitaji hapo awali.
Wakala wa staa huyu, Rammy Abbas, aliwaambia Liverpool kwamba alitaka mkataba wa miaka mitatu kwa mteja wake, lakini wamiliki wa majogoo awali walikuwa tayari kumpa mwaka mmoja tu.
Hata hivyo, makubaliano yamefikiwa muafaka na sasa Salah mwenye umri wa miaka 32, atasaini mkataba wa miaka miwili na timu hiyo aliyojiunga nayo mwaka 2017.

Salah ambaye kwa sasa anakunja Pauni 400,000 kwa wiki, katika mkataba wake huo mpya pia atakuwa akipata kiasi hicho.
Liverpool pia inatazamia kumpa mkataba mpya Virgil van Dijk na Trent Alexander-Arnold, kwani wote wanakaribia kumaliza mwaka wao wa mwisho wa mikataba yao ya sasa.
Mabosi wa Liverpool wamepambana kufikia makubakiano na Salah kutokana na ubora na umuhimu wake katika kikosi chao msimu huu akiwa amefunga mabao 13 na kutoa asisti nane kwenye mechi 14 za Ligi Kuu England.
Vilevile kiujumla tangu ajiunge nao amefunga mabao 226 katika mechi 370 za michuano yote.
Mwezi uliopita, Salah aliweka wazi kwamba anasikitishwa na kitendo cha mabosi wa timu hiyo kutompa ofa ya mkataba mpya licha ya ule wa sasa kuwa mbioni kumalizika na akaongeza kuwa yupo karibu kuondoka kuliko kubaki.
"Tunakaribia kuingia Desemba na sijapokea ofa yoyote ya kubaki klabuni. Labda nipo zaidi nje kuliko ndani. Mnafahamu nimekuwa klabuni kwa miaka mingi. Hakuna klabu kama hii. Lakini mwishowe suala la mkataba haliko mikononi mwangu. Kama nilivyosema, ni Desemba na sijapata chochote kuhusu mustakabali wangu," alisema Salah baada ya mchezo wa Liverpool dhidi ya Southampton uliochezwa Novemba 24 mwaka huu.
Salah ameisaidia Liverpool kufanya vizuri katika michuano yote msimu huu wakiwa wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, hadi sasa ndio wanapewa nafasi kubwa zaidi ya kuchukua taji la EPL msimu huu.
Licha ya kufikia makubaliano hayo, hadi sasa staa huyu hajasaini mkataba mpya na lolote linaweza kutokea kwani bado vigogo wengi ndani na nje ya Bara la Ulaya hususani timu za Saudi Arabia zinatamani sana kumsajili, hivyo zinaweza kuwasilisha ofa nono zaidi inayoweza kumshawishi fundi huyu wa kimataifa wa Misri akaachana na mpango wa kusaini dili jipya na kutua kwao.
Paris Saint-Germain ilikuwa moja kati ya timu zilizotajwa hivi karibuni na katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana Al Ittihad ya Saudi Arabia ilituma ofa inayofikia Euro 200 milioni kwa ajili ya kumsajili.