Mashindano ya gofu NCBA yamfungulia ukurasa Magombe

Dar es Salaam. Nyota wa gofu upande wa wanawake, Ayne Magombe amesema mashindano ya NCBA Series yamempa somo na uzoefu mkubwa na kuahidi kufanya vizuri mashindano yajayo.
Mchezaji kutoka Morogoro, Seif Mcharo aliiwakilisha nchi kwa upande wa wanaume katika mashindano hayo yaliyoshirikisha wachezaji 108.
Magombe alisema ushindani ulikuwa mkubwa sana na kila mchezaji aliwania nafasi ya kwanza.
Mbali ya Tanzania, Uganda na Rwanda nazo zilishirikisha wachezaji wawili wawili huku Kenya ikiwakilishwa na wachezaji kutoka klabu 23.
“Yalikuwa mashindano ya aina yake, yenye ushindani na msisimko mkubwa. Nawapongeza waandaaji na wadhamini, Benki ya NCBA kwa kudhamini mashindano haya kupitia kauli mbiu ya “Maisha ni Hesabu”,” alisema Magombe.
Alisema mashindano hayo pia yalikuwa sehemu ya kukutana na wadau mbalimbali wa mchezo huo wa Afrika Mashariki na kubadilishana mawazo.
Mkurugenzi Mkuu wa benki ya NCBA Claver Serumaga alisema mashindano hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuahidi kuendelea kuandaa na kudhamini.
“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati na heri njema kwa washiriki wa mashindano kwa kuweza kuiwakilisha nchi kwa mara ya kwanza, Benki ya NCBA Tanzania itaendelea kuwa mdau halisi wa mchezo huu kupitia kauli mbiu yetu ‘Maisha ni Hesabu’ - maisha ni juu ya kufanya hesabu sahihi kwa mustakabali wenye mafanikio” alisema Serumaga.