Mosimane apewa jukumu maalum Yanga
Muktasari:
- Pitso Mosimane ameshinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Klabu mbili tofauti. Mataji mawili ameshinda akiiongoza Al Ahly ya Misri na moja ametwaa akiwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Yanga imemkabidhi Pitso Mosimane jukumu la kuwanoa makocha wa Mpango wake maalum wa soka la vijana uitwao Yanga Soccer School ambao umezinduliwa leo Novemba 15, 2025 jijini Dar es Salaam.
Rais wa Yanga, Hersi Said amesema kuwa Pitso ambaye amewahi kuzinoa Mamelodi Sundowns na Al Ahly, atawapika makocha ambao watasimamia program hiyo.
“Tumeongea na Kocha Pitso Mosimane ambaye amekubali ombi letu la kutoa mafunzo kwa makocha wetu wa vijana. Lengo letu ni kutumia falsafa ya timu yake ya soka na kuimarisha falsafa yetu pia hapa. Tunamshukuru sana Kocha Mosimane kwa kukubali wito wa kujiunga nasi siku hii ya historia.
"Mradi wa 𝐘𝐚𝐧𝐠𝐚 𝐒𝐨𝐜𝐜𝐞𝐫 𝐒𝐜𝐡𝐨𝐨𝐥 ni mradi endelevu ambao tutachukua watoto wa U-11, U-13 na U-15. Hatutaishia mkoa wa Dar Es Salaam pekee yake bali tutatanua wigo kwa maeneo mbalimbali Tanzania. Jukwaa hili litatusaidia sana kwenye kuinua vipaji ambavyo tunaweza kuvitumia kwenye timu zetu za vijana," amesema Hersi.
Hersi amesema program hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa klabu ya Yanga na soka la Tanzania kiujumla.
"Niwapongeze sana wazazi ambao wametuamini na kuleta vijana wao kuwasijili kwenye 𝐘𝐚𝐧𝐠𝐚 𝐒𝐨𝐜𝐜𝐞𝐫 𝐒𝐜𝐡𝐨𝐨𝐥. Jukwaa hili ni jukwaa muhimu sana kwa ukuaji wa soka la kizazi cha kesho. Hawa watoto watakwenda kuwa msaada mkubwa kwa familia yao na kwa taifa kiujumla kupitia soka.
"Yanga Soccer School ni jukwaa ambalo linaleta watu wataaluma tofauti tofauti, vijana wanaotengenezwa hapa wataondoka wakiwa na maarifa ya kutosha. Tunatengeneza vijana wa kesho ambao wanapenda mpira lakini wanaujua vyema na jamii ya kesho itakwenda kuupenda mpira na kuushabikia," amesema Hersi.
Kwa upande wake Mosimane, amesema kuwa amekuwa akifurahishwa na mashabiki wa Yanga kwa namna wanavyoipenda timu yao.
“Siku ya mwananchi Day nilivutiwa sana na mwamko wa mashabiki. Tukiwa kwenye gari nikamwambia Rais wa Yanga anzisha Shule ya Soka. Nimefurahi sana hatimaye leo nipo kwenye uzinduzi. Namshukuru pia rafiki yangu Arafat Haji, amenipokea vizuri. Yanga ni familia yangu kwa muda mrefu.
“Namshukuru sana Rais wa Yanga SC, Mimi na Injinia ni marafiki wa muda mrefu sana. Niliwahi kuja hapa kwa ajili ya Mwananchi Day. Ama kwa hakika ni siku pekee na ya kufana sana. Mashabiki wa Yanga wanaipenda sana timu yao. Hongereni sana. Nyie ni mfano wa kuigwa.
“Siku ya mwananchi Day nilivutiwa sana na mwamko wa mashabiki. Tukiwa kwenye gari nikamwambia Rais wa Yanga anzisha Shule ya Soka. Nimefurahi sana hatimaye leo nipo kwenye uzinduzi. Namshukuru pia rafiki yangu Arafat Haji, amenipokea vizuri. Yanga ni familia yangu kwa muda mrefu," amesema Mosimane.