Ramsdale atoa neno kuhusu Arteta

Muktasari:
- Katika msimu uliopita Raya alishinda tuzo ya kipa bora , huku Ramsdale akiishia kucheza sehemu ndogo ya mechi za timu hiyo iliyomaliza nafasi yapili.
Kipa wa zamani wa Arsenal, Aaron Ramsdale amefunguka kuhusu uhusiano wake na kocha wa timu hiyo Mikel Arteta.
Ramsdale ambaye kwa sasa anaichezea Southampton alipoteza nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza baada ya Arsenal kumsajili David Raya kutoka Brentford kwa mkopo uliodumu kwa msimu mmoja kabla ya kumsainisha mkataba wa kudumu.
Katika msimu uliopita Raya alishinda tuzo ya kipa bora , huku Ramsdale akiishia kucheza sehemu ndogo ya mechi za timu hiyo iliyomaliza nafasi yapili.
Baada ya kuona mambo yanazidi kuwa magumu Ramsdale aliamua kujiunga na Soton katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa ajili ya kupata nafasi kubwa ya kucheza.
Licha ya kuwekwa nje muda mwingi Ramsdale amesema hana kinyongo na Arteta na kusisitiza kwamba alifanya kila linalowezekana kumshwishi kocha huyo katika kiwanja cha mazoezi lakini ilishindikana hivyo ana heshimu uamuzi wake.
"Nilijaribu kila niwezalo kubadili mtamzamo wake juu yangu ili anirudishe kuwa namba moja . Akili yake ilikuwa tayari inamwamini David ambaye kwa wakati huo alikuwa na msimu mzuri. Ilikuwa ngumu sana kwangu, lakini nimepata timu mpya na ninatazamia kucheza tena, naamini nilipitia yale ili kunirudisha katika mstari, ulikuwa msimu mgumu, yalikuwa ni mapito tu ya mpira wa miguu na kwa sasa nina furaha juu ya hapa nilipo."
Tangu kuanza kwa msimu huu Ramsdale amecheza mechi mbili za Ligi Kuu England na kuruhusu mabao sita.