Sakilu aweka rekodi ya Taifa, Simbu akikwama

Muktasari:
- Rekodi ya Taifa ya nusu marathoni kwa wanawake ilikuwa ikishikiliwa na Magdalena Shauri aliyoiweka mwaka 2020 alipokimbia kwa muda wa saa 01:06:37.
Dar es Salaam. Mwanariadha Jackline Sakilu ameshika nafasi ya tatu katika mbio za nusu marathoni za Ras Al Khaimah zilizofanyika leo huko Falme za Kiarabu, huku akifanikiwa kuvunja rekodi iliyowekwa na mwenzake, Magdalena Shauri miaka minne iliyopita.
Katika mbio za leo, Februari 24, 2024 Sakilu alikimbia kwa muda wa 1:06:04 ambao umemfanya aweke rekodi ya taifa na kuvunja ile iliyowahi kuwekwa na Magdalena Shauri mwaka 2020 ya kukimbia kwa muda wa 01:06:37 katika mbio hizohizo za Ras Al Khaimah.
Aliyeibuka mshindi katika mbio hizo upande wa wanawake leo ni Tsigie Gebreselama wa Ethiopia aliyekimbia kwa muda wa 01:05:14, huku mshindi wa pili akiwa Muethiopia mwenzake, Ababel Yeshaneh.
Wakenya wanne wameshindwa kufua dafu mbele ya Sakilu ambao ni Margaret Chelimo aliyemaliza katika nafasi ya nne, Evaline Chirchir aliyekuwa nafasi ya tano, Catherine Amanangole aliyemaliza wa sita na Peres Jepchirchir ambaye alifika nafasi ya saba.
Kwa kuibuka mshindi wa tatu kwenye mbio hizo, Sakilu amejihakikishia kupata Dola 7,000 za Marekani (Sh 17.8 milioni) wakati mshindi wa kwanza akipata Dola 15,000 na wa pili akipata Dola 10,000.
Wakati Sakilu akiitoa kimasomaso Tanzania upande wa wanawake, mambo hayakwenda vyema kwa Felix Simba aliyeshika nafasi ya 10 upande wa wanaume.
Wakenya walionekana kutawala mbio hizo upande wa wanaume ambapo walishika nafasi zote tatu za juu tofauti na kilichotokea upande wa wanawake.
Daniel Kibet Mateiko wa Kenya aliibuka mshindi, akifuatiwa na John Korir na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Isaia Lasoi.
Simbu hata hivyo hajaondoka patupu kwani amepata kiasi cha Dola 1000 (Sh 2.5 milioni) kwa kumaliza katika nafasi hiyo ya 10.