Twiga Stars yaifungia kazi Banyana Banyana

Muktasari:

  • Katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika vyema, Twiga Stars ina majina ya nyota wanne wa Banyana Banyana ambao itahakikisha hawafurukuti katika mechi mbili baina yao, jambo ambalo litaifanya ipate matokeo mazuri yatakayoivusha kwenda raundi ya mwisho ya mashindano hayo

Benchi la ufundi na wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania 'Twiga Stars' wametamba watahakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya Afrika Kusini 'Banyana Banyana' katika mechi ya kuwania kufuzu michezo ya Olimpiki utakaochezwa kesho kuanzia saa 10 jioni katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Na katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika vyema, Twiga Stars ina majina ya nyota wanne wa Banyana Banyana ambao itahakikisha hawafurukuti katika mechi mbili baina yao, jambo ambalo litaifanya ipate matokeo mazuri yatakayoivusha kwenda raundi ya mwisho ya mashindano hayo.

Kocha Mkuu wa Twiga, Bakar Shime alisema, "Tumekaa kambini kwa siku 10, tunajua ni mechi ngumu dhidi ya Afrika Kusini tuna nia ya kufanya vizuri na matarajio yetu ni kupata kikosi imara ambacho kitacheza mashindano ya Olimpiki."

Kiungo Diana Msewa anayechezea Amed SK ya Uturuki alisema, "Nimefurahi kurejea tena nyumbani kwa sababu tuna mechi ngumu mbeleni dhidi ya Afrika Kusini mimi na wachezaji wenzangu tumejipanga vizuri na sio mgeni kwenye timu hivyo tutapambana."

Enekia Lunyamila anayecheza Ligi ya Saudia (Eastern Flames) alisema, "Tunajadili na wenzetu kwenye mashindano hayo nini cha kufanya ili kuhakikisha tunapata ushindi na tuwaahidi watanzania tutafanya vizuri."

Wachezaji wanne wa Banyana Banyana ambao Twiga Stars itawafungia kazi kesho ni Melinda Kgadiete, Thembi Kgatlana, Linda Motlhalo na Thubelihle Shamase.

Kgadiete anayechezea Mamelodi Sundowns, ana uwezo mkubwa wa kufumania nyavui ambapo mwaka 2021 alishinda tuzo ya kiatu cha dhahabu katika mechi za kufuzu Ligi ya mabingwa kwa wanawake ya COSAFA akifunga mabao matano.

Kgatlana anayeitumikia Tigres UANL ya Mexico akimudu nafasi ya winga na mshambuliaji wa kati, katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2016 na 2018 kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika alishinda tuzo ya mchezaji na mfungaji bora wa mashindano akifunga mabao matano.

Linda Motlhalo ambaye ni mchezaji wa Racing Louisville ya Marekani,  mbali na kucheza nafasi ya kiungo, ana uwezo wa kufunga na mwaka 2022, Motlhalo alikuwa mfungaji bora wa Afrika Kusini kwenye michuano ya  kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake  akifunga mabao matano katika mechi nne.